Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Mizengo Pinda, jana alitumia Ibada ya Shukrani iliyofanyika katika Parokia ya Hananasifu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, kumshukuru Mungu kwa kumwezesha kulitumikia Taifa kwa zaidi ya miaka 15 na kuwaomba Watanzania wamsamehe kwa matamshi aliyoyatoa akiwa kiongozi, huenda yaliwakwaza baadhi yao.
Pinda ambaye amekuwa Waziri Mkuu kwa miaka minane na miezi tisa, Waziri kwa miaka miwili na nusu na Naibu Waziri kwa miaka mitano, alisema anasikia fahari kumaliza uongozi wake kwa furaha na amani.
Moja ya kauli tata zilizowahi kutolewa na kiongozi huyo iliyozua sintofahamu ni ile ya Juni 29, 2013 katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma alipoviagiza vyombo vya dola kuwashughulikia kwa kuwapiga wale watakaokataa kutii amri wakati wakifanya vitendo vya uvunjifu wa amani.
Kauli nyingine tata ni ile ya mwaka 2009 baada ya kuwaeleza wanaoua watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) pamoja na vikongwe hawana budi kuuawa kwa kuwa wakisubiri mahakama kuwahukumu, watakuwa wanakosea.
“Katika ibada hii ya shukrani, nimemuomba Mungu anisamehe kwa matamshi niliyoyatoa nikiwa kiongozi yanaweza kuwa yaliwaudhi watu bila mimi kujua.
“Uwaziri Mkuu ni kazi ngumu yenye changamoto nyingi. Nitakuwa mtu wa ajabu nisipomshukuru Mungu kwa uongozi wake katika kipindi chote hicho tangu nikiwa naibu waziri hadi kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu,” alisema.
Pinda alisema katika utumishi wake kwa umma amejifunza mambo mengi lakini kikubwa zaidi ni kujua jinsi ya kuishi na watu.
Katika hatua nyingine, Abate Thadei Mhagama wa Abasia ya Hanga, aliwataka waumini nchini wazidishe maombi kwa kufunga na kuomba kwa siku sita zilizobaki kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.
“Ninawaomba waumini wote tuzidishe sala ili nchi iendelee kuwa na amani na upendo, tumwombe Mungu pia atuwezeshe kupata viongozi aliowandaa kwa yeye kwa maana ya rais, wabunge na madiwani,” alisema Mhagama.
Alisema uchaguzi wa mwaka huu ni wa aina yake kwani demokrasia imekuwa miongoni mwa Watanzania.
“Sote ni mashahidi, tumeona kwenye mikutano kila mgombea akija sote tunajaa huko. Hii ni kwa sababu hatujui yupi ni yupi, ndiyo maana nasisitiza kuwa tumuombe Mungu atuletee yule ambaye amemuandaa yeye,” alisisitiza.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Baraza la Walei katika parokia hiyo, Arbogasti Warioba alisema:
“Sote tunatambua kuwa kazi aliyoifanya Waziri Mkuu Pinda ilikuwa ngumu, misafara ilikuwa ni mingi na wakati mwingine ilikuwa ya mwendo mkali, lakini Mungu alimtetea na kumlinda hadi leo yuko salama. Tunakushukuru pia kwa ushirikiano ulioendelea kutuonyesha wakati ukiwa madarakani na tunakuombea uendelee kuwa na ucha Mungu katika maisha yako ya uraiani.”
No comments :
Post a Comment