Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, October 4, 2015

Serikali kuburuzwa mahakamani

Image result for Independent Power Tanzania Limited (IPTL)
Na Joseph MihangwaILIKWISHASEMWA na kufafanuliwa kwa kina; kwamba mkataba wa kitapeli wa miaka 20 kati ya kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na serikali kupitia shirika lake la umeme nchini (Tanesco) ,uliofikiwa mwaka 1994, utafilisi nchi tukiangalia kwa kuchekelea kama mazuzu.
Hadi sasa serikali “imelizwa” mara nne kwa maumivu ya uchumi wa nchi na kwa maisha ya Watanzania, kila mara tukipozwa kwa maelezo na ghiliba zenye kuficha ufisadi unaojirudia. Imekuwa kwa kila awamu ya serikali madarakani, ulaji mpya kwa “kiwanja” kile kile. Kulikoni?.
Agosti 1994, serikali ilifikia makubaliano (MoU) na Kampuni ya IPTL yaliyohusisha ujenzi na usimikaji wa mtambo wa kufua umeme pale Tegeta, jijini Dar es Salaam, ujenzi wa nyumba na miundombinu [Engineering Procurement and Construction Contract] – EPC; na uuzaji/ununuzi wa umeme (Power Purchasing Agreement) – PPA. Na kama tutakavyoona baadaye, chini ya makubaliano hayo, serikali ilianza kulipia umeme na matumizi ya mtambo (capacity charges) kabla hata mtambo haujasimikwa wala kuzalisha umeme
Mkataba huo wa miaka 20 kuanzia mwaka 1994 ulihusu kununua mtambo wa megawati 100 aina ya Slow Speed Diesel (SSD) kwa gharama ya dola za Marekani milioni 163.5 (bei halisi dukani Finland ilikuwa dola milioni 63); gharama za ujenzi na usimikaji wa mtambo (EPC) dola milioni126.39, tozo kwa matumizi ya mtambo (capacity charges) dola milioni 4.2 kwa mwezi na malipo ya senti 3.25 za Marekani kwa kilowati (kWh) ya umeme utakaozalishwa.

Tozo la dola milioni 4.2 kwa mwezi halibadiliki, IPTL iwe imezalisha au haikuzalisha umeme; na Tanesco iwe imetumia umeme au haikutumia, lazima lilipwe.
IPTL ni ubia ulioundwa mwaka 1994, kati ya Shirika la Mechmar (Malaysia) Bhd, lenye hisa asilimia 70, na Kampuni ya VIP Engineering and Marketing (VIPEM) ya hapa nchini, yenye asilimia 30 ya hisa.
Mhimili mwanzilishi wa VIPEM alikuwa marehemu Bakri Somji na kurithiwa na mwanae, Riaz Somji, lakini kiranja mkuu wake ametajwa kuwa Ananis Mamdan. Haifahamiki jinsi mmiliki wa sasa wa kampuni hiyo, James Rugemalila, alivyoingia.
Februari 1997, baada ya kutiwa sahihi mkataba kati ya IPTL/Tanesco, Mechmar/IPTL walichukua mkopo wa miaka 10 wa dola za Marekani milioni 105 kutoka Benki za Sime Bank ya Singapore na Bank Bumiputra (Malaysia) Bhd (BBMB) kwa ajili ya kununulia na kusimika mtambo pale Tegeta.
Lakini, tofauti na tulivyoona chini ya mkataba huo,ambapo mtambo huo umepewa thamani kubwa kupindukia ya dola 163.5, na kazi ya usimikaji na ujenzi (EPC) dola milioni 126.39; ukweli mradi mzima usingechukua zaidi ya dola milioni 105 ambazo IPTL ilikopa kutoka benki mbili hizo. Hapo ndipo tulipoanza kulizwa kwa mara ya kwanza. Waliopitia na kuidhinisha mkataba huo wa kitapeli wanajua, wengine bado wamo madarakani.
Mara ya pili ilikuwa Januari 1996, pale IPTL ilipobadilisha kinyemela aina ya mtambo uliokusudiwa kusimikwa pamoja na idadi ya miundombinu; kutoka mtambo imara aina ya Slow Speed Diesel (SSD) na kusimikwa mtambo hafifu na mkweche aina ya Medium Speed Diesel (MSD) na gharama za EPC kuongezwa kinyemela kwa asilimia 33 (Angalia ushahidi wa Tanesco kwenye Mahakama – ICSID, 2000:41).
Lengo la IPTL kwa ulaghai huo lilikuwa ni kuongeza thamani ya uwekezaji ili hatimaye iuze umeme kwa bei ya juu zaidi ya asilimia 50 ya bei halisi kwa kuzingatia thamani bandia ya mradi. Ni kwa sababu hiyo kwamba, wakati beiya umeme kwa mlaji ilitakiwa kuwa senti za Kimarekani kati ya 6 na 8kwa uniti moja, IPTL iliuza kwa senti 13, ikiwa ni faida ya zaidi ya asilimia 100.
Na ndivyo imekuwa hivyo, kwamba, kwa miaka 20 mfululizo, Tanesco na Watanzania wamelazimika kulipa IPTL zaidi ya 5.6bn/= kwa mwezi kama gharama za umeme na matumizi ya mtambo (capacity charge) kwa umeme wa kudunduliza.
Hata serikali ilipothibitisha hivyo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) Februari 2001, na Mahakama hiyo kuridhia kwamba mradi huo uliongezwa thamani kinyemela, na kwamba bei ya umeme iliyotoza IPTL ilikuwa haramu na kuagiza ifunguliwe (Tegeta) “Akaunti ya Escrow” kwa ajili ya tozo la ziada ililokuwa ikilipa Tanesco hadi hapo hesabu sahihi itakaporidhiwa na pande zote mbili ili Tanesco irudishiwe; serikali haikuchukua hatua, hadi fedha hizo zimekwapuliwa kijanja na mmiliki mpya wa IPTL, - Harbinder Sethi Singh wa Kampuni ya Pan African Power Solution (PAP).
Na kwa ujinga wetu, tulifurahi na kushangilia “ujasiri” wake huo wa kifisadi, likiwamo Bunge, ambalo lilisimama kidete kumtetea fisadi huyo kuwa fedha hizo hazikuwa za umma, licha ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuthibitisha bila ya shaka yoyote kuwa zilikuwa za umma.
Kufikia hapo, taifa limehujumiwa mara nne, kama ifuatavyo: (a) limeuziwa na kulipia mtambo mkweche na kwa bei ya juu kwa zaidi ya asilimia 150(b) limeuziwa umeme kwa bei kubwa kuliko nchi yoyote Afrika Mashariki na Kati kwa miaka 20mfululizo, hadisasa (c) Nchi imetupwa gizani na uchumi kuathirika kwa umeme wa kusuasua kwa miaka 20 kutokana na Mkataba huo wa kilaghai (d) Taifa limeporwa zaidi ya 320bn/= na “mwekezaji” mpya (PAP) anayedai kununua mali na madeni ya IPTL, fedha ambazo Tanesco ilipaswa kurejeshewa na IPTL.
Serikali, kwa kujua au kutojua, imeagiza mkataba na “mwekezaji” huyo mpya uendelezwe; safari hii si kwa kuuziana umeme wa megawati 100 kama ilivyokuwa na IPTL, bali megawati 500, ili tuzidi kukaangwa kwa mafuta yetu.
Kashfa ya Akaunti ya Escrow, Tegeta imefyeka vichwa vya mawaziri waandamizi watatu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), huku watendaji waandamizi wengine wakiachwa viporo (kwa nini?) kutokana na kupokea fedha kubwa kutoka kwa mmiliki wa PAP kama aksante ya kuwezesha uporaji huo.
Akiongea na wazee wa Dar es Salaam, Desemba 22, 2014 juu ya tuhuma ya uchotwaji wa 320bn/= hizo na PAP, Rais Jakaya Kikwete aliwapoza Watanzania kwa kueleza kwamba fedha hizo hazikuwa za umma bali za IPTL, na kwamba uuzaji wa IPTL kwa PAP ulikuwa halali na sahihi, akaelekeza serikali/Tanesco iendelee kufanya mazungumzo na PAP juu ya kuendeleza mkataba.
Kama hivyo ndivyo itakavyokuwa, PAP, kwa kuuza umeme kwa senti za Marekani 6 hadi 8, ambayo ndiyo bei iliyopashwa kuwa tangu mwaka 1994 badala ya senti 13; itavuna bilioni 3/= kila mwezi kama “capacity charge” kwa uwekezaji ambao haijafanya.
Wakati wino wa kalamu ya Rais Kikwete haujakauka, hivi karibuni, imejitokeza Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB –HK) na kutishia kuishitaki serikali kwa kuilipa PAP 320bn/=bila kustahili na kinyume cha utaratibu kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow. Standard Chartered inadai ilinunua deni la dola milioni 105, la IPTL kwa Sime Bank na Bank Bimuputra, na hivyo inataka ilipwe.
Katika barua ya notisi kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ya Septemba 15, 2015 iliyotiwa sahihi na Mkurugenzi Mtendaji wake, Joe Casson, Benki hiyo inakusudia kuifikisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) ya mjini London, kutaka iiamrishe serikali iilipe deni la dola za Marekani milioni 126 (277bn/=) linalotokana na mkopo wa dola milioni 105 zilizokopwa na IPTL mwaka 1994 kwa ajili ya kununulia na usimikaji wa mtambo wa IPTL, Tegeta.
Benki hiyo imedai kuwa, Serikali ya Tanzania ilikosea kuwalipa PAP 320bn/= kutoka akaunti ya Escrow badala ya kuilipa IPTL ambayo ndiye mmiliki halali wa fedha hizo, hivi kwamba kitendo hicho cha Serikali kimesababisha Benki hiyo ipoteze fedha hizo.
Kama kesi hiyo itafunguliwa na serikali ikashindwa; kwa mara nyingine tena, tunakabiliwa na hatari ya kulipa zaidi ya 280bn/= mbali na riba pamoja na gharama za kesi kwa kashfa zile zile za IPTL zinazojirudia.
Lakini je, serikali haikuliambia Bunge na umma kwa ujumla kwamba mmiliki wa PAP, Harbinder Sethi Singh, ndiye mmiliki halali wa IPTL, aliyerithi mali na madeni ya IPTL; na kwamba alilipwa fedha za Akaunti ya Escrow ili alipe madeni ya IPTL? Kama hivyo ndivyo, kwa nini Benki isimdai Harbinder Sethi Singh?. Je, Benki haitambui kununuliwa kwa IPTL na PAP? Kama sivyo, kwa nini PAP asiunganishwe kwenye mashtaka na Serikali kama mnufaikaji na mauzo hayo?. Hapa tunanusa kitu: tumetapeliwa; hakuna uuzaji halali uliofanyika.
Kama ni hivyo, basi, sisi malofa, “wajinga ndio waliwao”, tumeliwa na IPTL kwa mara ya tano, na tutaendelea hivyo kila awamu mpya ya utawala wa nchi inapoingia madarakani.
Tulianza na serikali ya awamu ya pili, ya Rais Ali Hassan Mwinyi iliyoruhusu mazingira ya kuingiwa mkataba huo wa kitapeli; watu wakachukua chao mapema, mkataba ukatiwa sahihi na Serikali kuanza kulipia mtambo na umeme ambao ulikuwa haujaanza kuzalishwa.
Ikaingia Awamu ya tatu, ya Rais Benjamin Mkapa, mwaka 1995; ikapokea mtambo mkweche na gharama za mradi kuongezwa maradufu ili watu wale; serikali ikaendelea kulipia umeme ambao ulikuwa haujaanza kuzalishwa wakati nchi ikigwaya kwa giza na uchumi kuathirika.
Awamu ya nne, ya Rais Jakaya Kikwete iliendelea kukingia kifua ufisadi huu, sio tu kwa serikali kulipia umeme “hewa” na mitambo mkweche, bali pia imehitimisha kwa kusimamia ukwapuliwaji wa 320bn/= na kumpa ulaji mpya tapeli mpya – PAP, kwa ufisadi mpya na mkubwa zaidi.
Naye Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano ajaye (ya Magufuli?) tayari ameandaliwa ulaji mkubwa zaidi chini ya mkataba wa PAP na kwa utapeli wa kutaka kukwapua zaidi ya 280bn/= kwa mashitaka ya Benki ya Standard Chartered. Hayo yote yanasimamiwa na mtandao huo huo wa IPTL, PAP na VIPEM.
Sakata la Akaunti ya Escrow, haliwezi kueleweka bila kujiridhisha nini kilitokea katika idhini ya utoaji hizo 320bn/= kwa PAP na ubabaishaji uliofuata.
Hukumu ya Mahakama Kuu (Jaji John Utamwa) katika kesi Misc Civil Cause No. 254 ya 2012, ambayo hatuna sababu hapa ya kuirejea kwa kirefu; ilielekeza, pamoja na mambo mengine, Kampuni ya PAP iliyonunua hisa za IPTL [pamoja na za VIPEM] na mtambo, kuwalipa wadai wote wa IPTLna kukabidhiwa mambo (affairs) ya IPTL, kikiwamo kiwanda.
Mahakama haikutamka lolote kuhusu Akaunti ya Escrow ikifahamu kwamba, akaunti hiyo haikuwa sehemu ya vitu vilivyonunuliwa na PAP na kulikuwa na kesi ikiendelea ICSID juu yake kati ya Tanesco na IPTL, kesi ambayo AG, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Waziri wa Nishati na Madini, walitaka ifutwe haraka ili Tanesco ipoteze kwa manufaa ya IPTL na PAP.
Wakati kesi hiyo ikiwa bado ingali hai, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi, aliingia Makubaliano na IPTL kwa niaba ya serikali, Oktoba 21, 2013, ya kulipwa kwa fedha hizo; na siku hiyo hiyo akamwagiza Gavana wa Benki Kuu (BoT), kwa barua Kumb: Na. SAB.88/417/01/5, ahamishie fedha yote ya Akaunti ya Escrow kwenye akaunti ya PAP haraka iwezekanavyo ili “kuwezesha IPTL (ya Harbinder Singh) kulipa wadai wake halali”.
Agizo hili kwa Gavana wa BoT kutoa fedha hizo lilitolewa kwa nguvu turufu, baada ya gavana huyo, Profesa Benno Ndulu, kupinga hatua hiyo kwa maelezo thabiti kwa Maswi na kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Servacius Likwelile, akisema, “….kwa kuzingatia unyeti wa suala hili na ukubwa wa malipo husika, Waziri wa Fedha apate fursa ya kuwajulisha Rais na Waziri Mkuu, ili waeleze kama wanaridhia au la; na serikali iombe kupata kinga dhidi ya madai yanayoweza kujitokeza baada ya malipo hayo kufanyika”.
Pamoja na hayo, Profesa Ndullu alipoomba uthibitisho wa PAP kununua hisa za Mechmar/IPTL, alipewa “Hati ya [Harbinder Sethi Singh] kupewa mamlaka” (Deed of Assignment) ambayo hakuna hata Afisa mmoja wa Serikali aliyethubutu kujiridhisha na uhalali wake kwa kuogopa nguvu iliyokuwa nyuma ya sakata hili.
Wakati Maswi akishinikiza hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alishinikiza kwa nguvu zaidi kiasi cha kuwaita waliopinga “mawakala wa shetani”, akisema: “Uamuzi huu wa Mahakama Kuu umetupa sasa fursa ya kuhakikisha kwamba suala hili linamalizika. Hii ni bahati ya Mtende kwetu; tunatakiwa kuchukua hatua sasa badala ya kuwa mawakala wa Shetani”.
Watanzania bado wanayo kumbukumbu, jinsi zaidi ya 133bn/= za Akaunti ya Malipo ya Fedha za Kigeni (EPA) zilivyochotwa mwaka 2005/2006 kwa kutumia “Deed of Assignment”, mtindo ambao umetumika pia kwa Tegeta Escrow. Moja ya kampuni (hewa?) zilizolipwa mabilioni hayo ni Kampuni ya “Kagoda Agricultural” ambayo hadi sasa haijulikani mmiliki wake, licha ya kwamba haipo.
Tunaendelea kuchezewa mchezo mchafu na mtandao wa kiovu unaoshirikisha watendaji wakuu serikalini. Hebu angalia: tunaambiwa Kampuni ya Pipelink ndiyo iliyonunua hisa 70 za IPTL kwa 6m/= na kumuuzia PAP kwa dola 300,000, sawa na 500m/=.
Wakati huo huo tunaelezwa VIPEM aliuza hisa zake 30 kwa PAP kwa dola milioni 75, sawa na 123bn/=; lakini wakati huo huo mmiliki wa VIPEM, James Rugemarila, anakiri kutokuwa na ushahidi wala kuhusishwa na mbia mwenzake – IPTL, katika uuzwaji wa hisa za IPTL. Kama huu si mchezo mchafu, ni nini?
Ukweli, mtandao huu wa kiovu unaundwa na Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa IPTL, Datuk Baharuden Majid, Issa Rueih wa Oman, rafiki mkubwa wa Baharuden ambaye ndiye aliyejitambulisha kama Pipelink, na Harbinder Sethi Singh, anayejitapa kuiweka Serikali mfukoni. Tutaendelea kuumia kwa ulaghai wa aina hii hadi lini?.
Tunasubiri kesi ya Benki ya Standard Chartered iive na Serikali iingie kizimbani kwa kuatamia ufisadi nchini. Safari hii hatutakubali kulainika; wale waliopuuza hoja za Profesa Ndulu wa BOT, lazima wajibu hoja na wawajibishwe hadharani kwa matendo yao. Tutataka wakubwa wa Serikali na “Bunge dhalimu”wakae mbali; waangalie kindumbwendumbwe kitakavyokuwa.

- See more at: http://raiamwema.co.tz/serikali-kuburuzwa-mahakamani#sthash.M8rtKLXt.dpuf

No comments :

Post a Comment