“Ndani ya miaka mitano ya kwanza tu ya Mzee Mwinyi, Tanzania ikashuhudia anguko kubwa la viwanda, mashirika na kampuni za umma. Mfumuko wa bei ukapanda kwa kasi, Tanzania ikashahudia serikali ikiingiza noti ya Sh 5,000 kama moja ya mkakati wa kudhibiti mfumuko huo wa bei, kabla ya kuingizwa kwa noti ya Sh 10,000 katika awamu ya pili na ya mwisho ya miaka yake mingine mitano.”
Usahihi ni kwamba Mzee Mwinyi alikabidhiwa nchi hii mwaka 1985, noti kubwa ya fedha za Tanzania ikiwa ni noti ya Sh 100 na si Sh 2,000 kama nilivyoeleza katika makala ile ya wiki iliyopita. Baadhi ya wasomaji wangu wenye kumbukumbu nzuri wamenikumbusha kwamba wakati Baba wa Taifa anang’atuka uongozi wa taifa hili na kumkabidhi Mzee Mwinyi mwaka 1985, taifa lilikuwa na noti nne tu za Sh 5.00, Sh 10.00, Sh 20.00 na Sh 100, ambapo katika mwaka wake wa mwisho huo wa 1985, noti ya Sh 5.00 iliondolewa na badala yake ikaletwa sarafu ya Sh 5.00, maarufu wakati ule kwa jina la Gwala au Dala (dola), ikiwa na alama ya trekta, ishara ya nchi inayotegemea uchumi wa kilimo cha kisasa.
Sarafu hiyo ya Sh 5.00 au Gwala au Dala, ilikuwa sawa na dola moja ya Kimarekani, ndiyo maana vijana wa mijini wakaiita Dala, wakiwa na maana ya dola, lakini pia Sh 5.00 hiyo ndiyo iliyokuwa bei ya nauli kwa mtu mmoja kwenye mabasi ya mijini, na ndicho kisa cha mabasi hayo ya mijini kuitwa daladala kwa sababu ya nauli yake hiyo ya wakati ule. Kwa upande wa sarafu, wenye kumbukumbu sahihi wamenikumbusha kwamba Mwalimu aliacha sarafu tano tu, kwa maana ya sarafu ya senti 5.00 iliyokuwa na alama ya samaki, sarafu za senti 10 iliyokuwa na alama ya pundamilia, sarafu ya senti 20 iliyokuwa na alama ya ndege aina ya mbuni, sarafu ya senti 50 au thumani, iliyokuwa na alama ya sungura na Shilingi moja iliyokuwa na alama ya Mwenge.
Kwa mujibu wa wasomaji wangu hao wenye kumbukumbu bado za tangu wakati ule, takriban miaka 30 iliyopita, bei ya kinywaji baridi aina ya soda, ilikuwa ikiuzwa kwa shilingi moja na thumuni (Sh 1.50) katika karibu maduka yote nchi nzima. Nimekumbushwa pia na wasomaji wangu hao kwamba noti za 200, Sh 500, 1,000, 2,000 na 5,000 ziliingizwa na Serikali ya Mzee Mwinyi katika kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano tu, kati ya mwaka 1985 na 1990, wakati noti ya Sh 10,000 iliingia katika kipindi chake cha pili cha kati ya mwaka 1990 hadi 1995!
Sababu za kuongeza noti zenye thamani kubwa tano hizo ndani ya miaka yake hiyo mitano ya kwanza, zimetajwa kwamba ni kutokana na hatua ya serikali hiyo ya Mzee Mwinyi kukubali kutii na kutekeleza masharti ya Benki ya Dunia pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa Duniani (IMF), yaliyotaka, pamoja na mambo mengine, kushushwa kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania, jambo ambalo Baba wa Taifa alilipinga kwa nguvu zake zote. Nichukue fursa hii kuwaomba radhi wasomaji wangu wote kwa upungufu huo wa kumbukumbu za kitakwimu kuhusiana na sarafu na noti katika kipindi kile cha taifa hili kutoka mikononi mwa Mwalimu kwenda mikononi mwa Mzee Mwinyi.
Mada ya leo imebebwa na maneno; ugomvi wa Lowassa na Kikwete wawapumbaza Watanzania. Hili nimelipata sehemu fulani kwenye kijiwe cha mijadala ya kisiasa, inayojadili hali ya kisiasa ndani ya nchi hii, hasa katika kipindi hiki cha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu. Kijiwe hicho ni maarufu kwa kahawa na michezo ya bao na karata.
Kinapatikana wilayani Kinondoni, katika Jimbo la Kawe. Mzee mmoja wa makamo, baada ya kusikiliza ubishi wa kisiasa juu ya nani zaidi kati ya mgombea wa CCM, Dk John Pombe Magufuli na mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, aliinuka kutoka kwenye benchi alilokuwa amekalia na kutamka: “Ninyi wote hapo ni wajinga tu. Mngekuwa mnafahamu kuwa mnachokishabikia kwa sasa ni ugomvi binafsi wa madaraka kati ya Mkwere na Mmasai, msingepoteza muda wenu kumjadili Lowassa.”
Katika kutoa ufafanuzi wake juu ya kauli yake hiyo, Mzee huyo anasema Lowassa ana hasira sana na Kikwete, hasa baada ya Mwenyekiti huyo wa CCM kuzuia jina lake lisifikishwe hata ndani ya kikao cha Kamati Kuu mjini Dodoma ili lijadiliwe na wajumbe wa kikao hicho na hatimaye wajumbe wenyewe waamue hatima yake.
Anasema hasira hizo zinazotokana na kitendo hicho cha Rais Kikwete, cha kutumia nguvu nyingi kuzuia jina la Lowassa kufikishwa katika vikao vya uamuzi vya chama chake, ndizo zilizomwongezea ghadhabu na chuki zaidi Lowassa, hivyo kuachana na CCM na kuhamia Chadema ili tu kumuonyesha Rais na Mwenyekiti Kikwete, ni nani zaidi katika siasa za nchi hii kati yao hao wawili. Kwa mujibu wa Mzee huyo, tukio lile la Dodoma la jina la Lowassa kushindwa kufikishwa ndani ya vikao vikuu vya uamuzi vya Chama, lilikuwa ni tukio la tatu kwa mwanasiasa huyo kutoshwa na swahiba wake mkuu huyo, Rais Kikwete, jambo lililompandisha hasira Lowassa, hivyo kuamua potelea mbali, liwalo na liwe! Binafsi, nakubaliana na hoja hizo za Mzee huyo.
Watanzania tumejikuta hapa tulipo sasa, kutokana na kukumbwa na upepo wa ugomvi wa madaraka wa watu hawa wawili; Rais Kikwete na Lowassa, si kitu kingine! Kwa haiba na heshima aliyokuwa nayo Lowassa ndani ya CCM, chama kilichomlea na kumjenga kisiasa hadi kumfikisha hapo alipo, isingekuwa kazi rahisi kwa mbunge huyu wa Monduli kuchukua uamuzi mgumu huo alioufanya wa kuamua kuachana na chama chake hicho na kujiunga na Chadema, chama ambacho kwa karibu miongo miwili, viongozi wake walikuwa wakimchafua na kumdhalilisha mbele ya jamii ya Watanzania.
Binafsi, naamini hata uamuzi wa Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, wa kuamua kuondoka ndani ya CCM na kujiunga na upinzani, hautokani na chuki na kukerwa na hatua ya chama hicho kukata jina lake katika mbio zake za urais mwaka huu mjini Dodoma, bali ni chuki na hasira dhidi ya Rais na Mwenyekiti Kikwete. Nitaeleza. Imesemwa na bado inaendelea kusemwa kwamba Lowassa na Rais Kikwete ni marafiki wakubwa.
Ni kutokana na urafiki huo, uliowafanya wawili hao, mwanzoni mwa miaka ya 2000 waingie katika makubaliano ya kirafiki ya kuachiana awamu za utawala wa nchi hii kwa kuungana mkono na kuunganisha nguvu zao za kisiasa. Ni makubaliano hayo ya kirafiki kati ya wawili hao, yalishuhudiwa bila shaka na wapambe wao wa karibu, ndiyo yaliyomhakikishia na kumwaminisha Lowassa kwamba baada ya Rais Kikwete, yeye ndiye angekuwa mrithi wake, Rais wa Awamu ya Tano ya uongozi wa taifa hili. Katikati kujiamini huko kwa Lowassa, kunakotokana na makubaliano hayo ya kirafiki, ya yeye kumwachia na kumuunga mkono rafiki yake 2005 ili itakapofika mwaka 2015 achukue yeye nafasi kwa kuungwa mkono pia na rafiki yake huyo, ndiko kulikompa jeuri hadi kufikia kukiambia chama chake kwamba ndani yake hakuna yeyote mwenye uthubutu wowote wa kukata jina lake.
Lowassa hakutegemea kabisa kuona Rais na Mwenyekiti Kikwete anayejua makubaliano yao hayo, anaweza akamgeuka na kuwa upande wa wanachama wenzao kina Samuel Sitta, Bernard Membe na wangineo waliokuwa hawataki kabisa kusikia jina la Lowassa likiteuliwa na chama chao kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Hatua hiyo ya Rais na Mwenyekiti Kikwete, kuongoza na kusimamia mikakati ya kuhakikisha jina la Lowassa halipitishwi na chama chake kuwa mgombea mteule wa urais, lilikuwa ni pigo la tatu na mwisho kwa mwanasiasa huyo lililotonesha madonda ya mapigo mengine mawili ya huko nyuma, ambayo nayo yalisimamiwa na rafiki yake huyo.
La kwanza lilikuwa ni lile la mwaka 2008, pale Lowassa akiwa Waziri Mkuu, alipojikuta akijiuzulu wadhifa wake huo katika mazingira ya fedheha, aibu na udhalili. Naamini, kabla ya kupatwa na mkasa huo wa kujiuzulu, Lowassa hakuwa amewahi kukaa chini na kufikiria dhamana ya nafasi hiyo aliyokuwa amepewa ya kuwa waziri mkuu, wala hakuwahi kufikiria kuwa ingeweza kutokea akakwamia njiani kabla ya 2015 kwa sababu kuamini katika dhana ya ‘ushakaji’ na Rais Kikwete. Lowassa alijiamini na kujawa na jeuri ya hali ya juu katika utendaji wake wa uwaziri mkuu, akijua kwamba hakuna yeyote, awe mteuzi wake mwenyewe Rais Kikwete au mwingine yeyote yule anayeweza kumwondolea uwaziri mkuu wake kwa sababu ya makubaliano yao ya kirafiki ya wawili hao.
Alijua, hata akifanya chochote kile kibaya kwa serikali yao, angefumbiwa macho tu na mamlaka yake ya uteuzi kutokana na ‘ushikaji’ wao. Akasau kitu kimoja muhimu katika uongozi wa nchi. Dhamana! Ni nani kati ya Lowassa na Rais Kikwete mwenye dhamana na nchi hii na mwenye dhamana na serikali yao. Lowassa akasahau kwamba mambo yakiharibika, atakayeulizwa na kulaumiwa na umma wa Watanzania ni mkuu wa nchi, si yeye. Imani yake hiyo ya ‘kiushikaji’ ilimfikisha mahali akatenda kinyume hata cha maelekezo ya serikali kupitia vikao vya Baraza la Mawaziri, hasa lilipokuja suala la kupata mitambo ya kufua umeme wa dharura kwa njia sahihi na salama kwa Serikali.
Lowassa akasimama kidete, kwa kutumia mamlaka yake ya uwaziri mkuu, huku akijua fika kuwa mamlaka ya juu yake ni ya ‘kishikaji’ akahakikisha kwamba bila Richmond, bora nchi iingie gizani kwa kukosa umeme! Alikataa ushauri wa Mamlaka ya Udhibiti na Manunuzi ya Umma (PPRA), akakataa ushauri wa Bodi ya Zabuni ya Tanesco, akasema hapa ni Richmond tu! Kwa hiyo, hata baada ya kupatwa na mkasa huo wa Richmond baada ya Bunge, kupitia Kamati Teule ya Dk Harrison Mwakyembe, kumkalia kooni na kumtaka ajitathimini na kujipima kama anastahili kuendelea na uwaziri mkuu wake huo, kwa vyovyote vile, Lowassa alitegemea kuwa atalindwa, atapiganiwa na kukingiwa kifua na Rais Kikwete.
Haikuwa hivyo, Rais Kikwete alimtosa likawa pigo kuu la kwanza kwa Lowassa! Pigo la pili kwa Lowassa lilikuwa lile la uamuzi wa chama chake, ukiongozwa na Rais na Mwenyekiti Kikwete na mitume 12 wa CCM, waliokuwa wakimtaka Lowassa na washirika wake wajivue gamba kwa kujiondoa wenyewe kwa hiyari yao ndani ya chama hicho, kutokana na kuandamwa na tuhuma za ufisadi kila kona. Lowassa akawekwa kati. Kule viongozi wa Chadema, huku viongozi wa CCM, wakiongozwa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Lowassa akala ganzi, akajikausha huku akijenga hoja za utetezi ndani ya vikao vikuu vya chama chake akitegemea kuungwa mkono kwa kupata utetezi wa Rais na Mwenyekiti Kikwete ndani ya vikao vyao hivyo, lakini haikuwa hivyo! Ni baada ya pigo hili la tatu mjini Dodoma, la Lowassa kukatwa jina lake katika mazingira yenye utata, ndipo hapo amefunguka akili na kubaini kwamba kumbe rafiki yake huyo alikwishampuuza na kuvunja urafiki wao pamoja na makubaliano yao yote ya kupeana utawala wa nchi hii kama mali yao. Lowassa, baada ya kufunguka akili na kubaini hali hiyo, ameamua kumtangazia vita ya kisiasa Kikwete. Kuhakikisha anatumia rasilimali zake zote, kuing’oa CCM madarakani ikiwa mikononi mwa Kikwete bado! Kama ilivyo kwa Sumaye, mgomvi wa Lowassa si CCM, bali ni Kikwete.
Ugomvi wa Kikwete na Sumaye, ulianza mwaka 2005 wakati wa mchakato wa kusaka mgombea mteule wa urais ndani ya chama hicho. Kwa wenye kumbukumbu Sumaye alifikia hatua ya kumwambia Kikwete kwamba mtu yeyote anayetafuta urais kwa kuwaua washindani wake kwa kalamu (magazeti), akipata urais ataua kwa risasi! Chuki ile ya Sumaye ya mwaka 2005 dhidi ya Kikwete, bado anayo hadi leo baada ya jina lake kukatwa mjini Dodoma chini ya usimamizi wa Rais na Mwenyekiti Kikwete, ndiyo maana waziri mkuu huyo mstaafu ameamua, katika hilo la ‘kumshughulikia’ Kikwete, azike tofauti zake na misimamo yake dhidi ya Lowassa na kuungana na Lowassa.
Hapo ndipo Tanzania imefikishwa, hapo ndipo CCM imefikishwa, na zaidi, hapo ndipo Watanzania walipofikishwa na wanasiasa hao watatu. Hivi ugomvi huo wa mafahari wawili hawa, Lowassa na Kikwete una tija gani yoyote kwa taifa hili, kiasi cha kuwavuta baadhi ya Watanzania wenzetu kujitoa akili na kumshabikia mtu mwenye hasira na chuki zake aliyedhamiria kununua urais kwa gharama yoyote ili kuwakomoa na kulipa visasi kwa wagomvi wake?
Nihitimishe makala haya kwa kusema kwamba wote wanaomshabikia Lowassa, kama anavyoonya mzee yule wa kwenye kijiwe cha kahawa, wameamua kununua ugomvi usiokuwa wa kwao. Ni vema wakakumbuka kuwa siku zote mwenye kisu kikali, ndiye mwenye kula nyama. Katika ugomvi huu, Lowassa ameshika makali, yatamkata tu!
- See more at: http://raiamwema.co.tz/ugomvi-wa-lowassa-na-kikwete-wawapumbaza-watanzania-1#sthash.Jb4C264B.dpuf
No comments :
Post a Comment