Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, October 18, 2015

Uzinduzi wa ajenda ya CUF ya kuigeuza Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika Mashariki

 Baadhi ya vijana wa vyuo vikuu walioshiriki uzinduzi huo wa ajenda ya CUF ya kuigeuza Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika Mashariki. (Picha na Salmin Said, OMKR)
 Baadhi ya vijana wa vyuo vikuu walioshiriki uzinduzi huo wa ajenda ya CUF ya kuigeuza Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika Mashariki. (Picha na Salmin Said, OMKR)
 Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akionesha filamu yenye ajenda ya kuigeuza Zanzibar kuwa Singapore, baada ya kuizindua rasmi katika ukumbi wa Majid, Kiembesamaki.
 Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akijibu maswali ya wanafunzi wa vyuo vikuu baada ya kuzindua  ajenda ya CUF ya kuigeuza Zanzibar kuwa Singapore.
   Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akijibu maswali ya wanafunzi wa vyuo vikuu baada ya kuzindua  ajenda ya CUF ya kuigeuza Zanzibar kuwa Singapore.
Na: Hassan Hamad, OMKR
Chama Cha Wananchi CUF kimezindua rasmi ajenda yake ya kuigeuza Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika Mashariki, na kusema kuwa tayari kimeweka mikakati imara ya kufikia hatua hiyo.

Akizindua ajenda hiyo iliyowasilishwa kwa njia ya filamu katika ukumbi wa Majid Kiembesamaki, Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama hicho Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ametaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuimarisha shughuli za biashara, baada ya kurekebisha mfumo wa bandari na viwanja vya ndege.

Amesema iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar atahakikisha kuwa anajenga bandari mpya ya kibiashara ambayo itaruhusu meli kubwa kuweza kufunga gati na kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa njia ya bahari katika mwambao wa Afrika Mashariki.“Bandari hii ya kibiashara itafanya kazi kwa saa 24, ni dhahiri kuwa kupitia eneo hili tu vijana wengi wataweza kujipatia ajira na kuongeza kipato chao”, alieleza.

Sambamba na hilo Maalim Seif amesema anakusudia kuimarisha huduma za viwanja vya ndege kwa kujenga sehemu ya mizigo ya kimataifa (cargo terminal), ili kuziwezesha ndege kubwa za mizigo kuweza kutua na kupakua mizigo Zanzibar.

Katika uzinduzi huo ambao uliwashirikisha wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, Maalim Seif amesema tayari wameshazungumza na makampuni makubwa ya kigeni ambayo yameahidi kushirikiana nae kukuza uchumi wa Zanzibar iwapo atachaguliwa kuwa kuwa Rais.

Amefahamisha kuwa sekta ya utalii pia inaweza kutoa mchango mkubwa kufikia azma hiyo, kwa vile wanakusudia kuwashajiisha watalii wa daraja la juu na kuimarisha miundombinu ya sekta hiyo ili kuvutia watalii ya wawekezaji wengi zaidi.

Amesema mapato ya ndani pia yanaweza kuongezeka iwapo kutakuwa na mipango imara ya uzalishaji na ukusanyaji wa mapato, sambamba na kupiga vita vitendo vya rushwa.

Maalim Seif pia amezungumzia sekta ya mafuta na gesi asilia ambayo amesema ndio sekta mama ya kuibadilisha Zanzibar kwa kipindi kifupi iwapo atapata ridhaa ya kuingoza Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu.

Amesema ndani ya siku mia moja za mwanzo za uongozi wake atahakikisha kuwa sera na sheria ya mafuta zinakamilika, na hatimaye kuweza kutoa tenda kwa kampuni za uchimbaji wa rasilimali hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Kupitia filamu hiyo ya “ajenda ya CUF kuigeuza Zanzibar kuwa Singapore”, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa timu ya ushindi CUF Mhe. Ismail Jussa Ladhu amesema kutokana na nafasi ya Zanzibar kijiografia, inaweza kuwa mfano mzuri kwa nchi za Afrika Mashariki.

Amesema Zanzibar inaweza kuunganishwa kwa njia ya Anga na Bahari na kuirejeshea Zanzibar hadhi yake ya kuwa kituo kikuu cha biashara kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Wakichangia ajenda hiyo baadhi ya vijana hao wa vyuo vikuu ambao pia waliuliza maswali mbali mbali kuhusiana na mpango huo wamesema inawezekana kuibadilisha Zanzibar iwapo viongozi hawatoweka mbele matashi ya kisiasa.

Hivyo wameahidi kuifikisha taaluma hiyo kwa wananchi wengine ili waweze kuchangia kufikia mabadiliko hayo.

ZanziNews.

No comments :

Post a Comment