Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete jana aliongoza waombolezaji kuuaga mwili wa mgombea ubunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe ambaye wanasiasa wametakiwa kuvaa ‘viatu vyake’ kuiga mema aliyokuwa anayatenda.
Filikunjombe na wenzake watatu walifariki dunia Alhamisi kwenye ajali ya helikopta iliyotokea katika Hifadhi ya Selous mkoani Morogoro. Wengine waliofariki kwenye ajali hiyo ni rubani Kepteni William Silaa, Francis Nkwera na Pladsus Ngabuma Haule.
Walioagwa jana pamoja na Filikunjombe ni Nkwera na Haule. Kepteni Silaa ambaye ni baba mzazi wa Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa, naye anatarajiwa kuzikwa leo.
Wakitoa salamu za rambirambi katika Hospitali ya Lugalo, viongozi mbalimbali walioambatana na Rais Kikwete kuaga miili hiyo, walisema Filikunjombe alikuwa mpiganaji, mpenda haki na mwenye upendo, hivyo viongozi waliobaki wanatakiwa kuvaa viatu vyake.
Spika Anne Makinda alisema viongozi na wananchi wote kuishi kwa upendo kwa kuwa duniani wote ni wapitaji, huku akihimiza familia yake kuiga tabia njema aliyokuwa nayo marehemu.
“Fanyeni aliyotaka Deo, msibadilishe, mtakuwa mnamchukiza huko aliko, pia niwaambie ndugu zangu mliopo hapa, hii dunia ni mapito, tuache roho za chuki na kufitiniana, tuishi kwa kupendana kwani hapa duniani tunapita,” alisema.
“Alikuwa mtu wa msimamo, alifanya kazi na watu wote hata vyama vya upinzani katika kusimamia masilahi ya umma, aliwapenda watu na Taifa lake, hakika ni wa kuigwa kwa aliyoyafanya,” alisema January Makamba wakati akitoa salamu kwa niaba ya CCM.
Makamba alisema hili ni pengo kwa CCM, wabunge waliopo na watakaokuja ‘wavae viatu’ vya Filikunjombe katika kueleta maendeleo ndani ya Taifa la Tanzania kwa kupigania masilahi ya wananchi.
Mgombea ubunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila alisema Filikunjombe alikuwa mtu muhimu katika Bunge la Tanzania, alionyesha mfano wa wabunge wanaohitajika nchini hasa katika sakata la uchotwaji wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
“Hatuna namna nyingine ya kumuenzi Deo zaidi ya kuendeleza yale aliyokuwa ameanza kuyapanda, niseme kwamba Tanzania tumepoteza kiongozi,” alisema Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kwa niaba ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali waliyokuwa wanaiongoza pamoja na Filikunjombe.
Hali ilivyokuwa
Miili hiyo mitatu iliagwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, saa 5:00 asubuhi na baada ya kuagwa ilipelekwa nyumbani kwa marehemu Filikunjombe, Mtoni Kijichi wilayani Temeke, kwa ajili ya ibada kabla ya kusafirishwa kwenda Ludewa kwa mazishi yatakayo fanyika leo.
“Tumefiwa, kwa heri Deo,” Ni kauli zilizosikika katika Hospitali ya Lugalo na nyumbani kwa marehemu na viongozi mbalimbali walitoa salamu, huku wakionyesha kuumizwa na kifo cha mpendwa wao.
Kijichi wamlilia
“Deo hana muda mrefu tangu ahamie kwenye nyumba yake, lakini alikuwa mtu wa watu, aliwajali majirani, hatuna cha kusema zaidi ya kusema tumefiwa,” alisema Elisia Bernado, mkazi wa Kijichi.
“Amekufa Deo basi tuamini hivyo, maana hakuna jinsi, ila kifo chake kimeniumiza, siyo mimi pekee hata wakazi wa Kijichi,” alisema Asia Juma.
Mwananchi.
No comments :
Post a Comment