Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, October 3, 2015

MAGUFULI APOTEZA MWELEKEO!

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amejivurugia nguvu za ushindi wake na juhudi za dharura zinahitajika kukabili hali hiyo.

Magufuli ambaye amedhihirisha kukubalika zaidi kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa, mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na mikoa ya Kanda ya Kati, ushindi wake sasa unaweza kuathiriwa na kauli yake, ambayo kwa mara ya kwanza aliitoa mkoani Geita, wiki iliyopita kwenye mkutano wake wa hadhara kuhusu wanaCCM wasaliti, kauli ambayo hata hivyo, kwa baadhi ya wanaCCM ni ya kishujaa inayobeba ujasiri dhidi ya uovu.


Akiwa mkoani Geita wiki hiyo iliyopita katika moja ya mikutano yake ya kampeni, alitamka; “..baadhi ya viongozi wa CCM ni wana-CCM mchana na usiku wanageuka kuwa wana-Ukawa.” Kauli hiyo sasa, kwa uchunguzi wa Raia Mwema, imezua tafrani kubwa kwa chama hicho, na hasa baada ya mgombea huyo wa CCM anayesifika kwa uchapakazi, kuirejea tena akiwa kwenye mkutano wa kampeni mkoani Shinyanga mwishoni mwa wiki iliyopita.


Akihutubia wakazi wa mji wa Shinyanga waliofurika kwenye uwanja wa CCM, Kambarage, akitokea wilayani Kahama, Septemba 26, mwaka huu, akiomba wampigie kura, Dk. Magufuli aliahidi kuwafanyia makubwa Watanzania kama watamchagua, ikiwamo kuimarisha uchumi wa nchi na mambo mengine ambayo hayakuweza kukamilishwa, kutekelezwa au kuanzishwa na Serikali ya Awamu ya Nne inayomaliza muda wake.

Ahadi zingine alizotoa mjini hapo ni pamoja na kujenga Chuo cha Madini na kiwanda cha nyama cha Mkoa wa Shinyanga, pamoja na kuondoa kero kwa wananchi na kuboresha maslahi ya wanyonge na kuahidi pia kupambana kwa “kula sahani moja” na mafisadi ambao alisema wameanza kumkimbia.

Hata hivyo, mbali na ahadi hizo nzuri na zenye kuweza kushawishi wananchi, Magufuli anadaiwa kuzua tafrani, tafrani ambayo inahusishwa na siasa za mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, ambaye kabla ya kujiondoa CCM, alipandikiza mtandao wa kumpa ushindi katika safari yake ya kuwania urais, ambayo akiwa huko CCM aliipachika jina la “Safari ya Matumaini na sasa katika Chadema, ameipachika jina la Mabadiliko.


Kauli tata ilivyozua tafrani

Dk. Magufuli aliwaonya wanaCCM aliowaita ndumilakuwili ambao mchana hujipambanua kama makada wa CCM lakini usiku wanatumikia na kufadhili vyama vya upinzani – Ukawa.


“Tunawajua kwa majina. Niwataje nisiwataje?” aliuliza Magufuli na mara baada ya wananchi kumtaka awataje, alimtaja moja kwa moja mmoja wa wana-CCM mashuhuri, si tu Mkoa wa Shinyanga bali kanda yote ya ziwa, Gasper Kileo, maarufu kwa jina “GAKI” na kuzua taharuki dakika 25 kabla ya kuhitimisha hotuba yake.


Gasper Kileo ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM - taifa na Mhazini ngazi ya mkoa kwa chama hicho; ni mfanyabiashara mkubwa mwenye kumiliki viwanda vya pamba Kanda ya Ziwa, biashara za uchukuzi na biashara nyingine chini ya kampuni inayoitwa GAKI INVESTMENTS.


Kileo pia ni mfadhili mkubwa wa CCM wa muda mrefu, na ndiye anayedaiwa kutoa usafiri kwa baadhi watu kutoka wilaya za mkoa huo kuja kumsikiliza mgombea huyo siku ya hiyo, pamoja na gari la matangazo linalotumika kwa kampeni katika mkoa huo.


Dk. Magufuli alipotaja jina hilo, mkutano uliguna kuashiria kutoamini kilichosemwa.
Katika hali ya kushangazwa na tamko la Magufuli, kwa hasira ya mlipuko huku akimkodolea macho Mbunge wa Shinyanga Mjini aliyemaliza muda wake na Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Stephen Masele, ambaye pia anawania ubunge wa jimbo hilo kwa mara ya pili, Gasper Kileo alihama meza kuu ya jukwaa alipokuwa akihutubia mgombea urais na kurudi viti vya nyuma na kujiinamia, huku akionesha hasira ya dhahiri kwa Masele (mgombea ubunge) na kupozwa na makada.


Hatua hiyo ilizua tafrani safu ya mbele ya jukwaa dakika hizo za mwisho, kumfanya Magufuli afadhaike na kumtambulisha kwa haraka Stephen Masele pekee kati ya wagombea nafasi za ubunge kwa wilaya za Shinyanga na Kishapu, na kuwasahau wengine, huku akiondoka jukwaani haraka kuepusha ghasia zaidi.


Waliosahauliwa kutambulishwa ni mgombea ubunge Jimbo la Solwa, Ahmed Salum; Nchambi wa Jimbo la Kishapu na wagombea wanne wa viti maalumu wa wilaya za Shinyanga na Kishapu.


Ingawa zimekuwapo taarifa kwamba Magufuli ametamka hayo kwa msukumo wa Masele, lakini taarifa za kiuchunguzi za gazeti hili zinabainisha kwamba, Magufuli amepata taarifa hizo kutoka katika mfumo wa kiintelijensia wa chama chake, CCM, mfumo ambao umekuwa ukifuatilia kwa karibu nyendo za kila mwanasiasa hasa wale waliokuwa karibu na Lowassa, kabla kuhamia Chadema.


Kwa upande mwingine, wachunguzi wa mambo ya kisiasa mkoani hapa wanaona, kitendo cha Magufuli kumdhalilisha hadharani mjumbe wa NEC na Mhazini wa Chama hicho, mkoa ni ishara ya kukosa subira na uvumilivu kwa mgombea huyo. Inadaiwa kwamba kitendo hicho kimezua mtikisiko, mgawanyiko na kukijeruhi Chama katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25, mwaka huu.


Kitendo hicho kinadaiwa kuacha maswali mengi kuliko majibu kama vile: “Hivi, ilikuwa lazima kwa Dk. Magufuli kuyasema hayo jukwaani badala ya kuitana faragha kama viongozi?”


Akizungumzia tukio hilo, Gaspar Kileo, alisema kwa kifupi; “Yote mmeyashuhudia; sina la kusema lakini sitishiki, nitaendelea kuwa mwaminifu kwa Chama changu, siasa za maji taka hazina nafasi kwangu”.


Naye Masele katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Raia Mwema alisema kwa kifupi; “Sihusiki na suala hilo na kwa kweli, nisingependa kulizungumzia. Nimekuwa nikitoa ushirikiano kwa kadiri ninavyoweza kwa wenzangu wote ndani ya CCM.”


“Najua ushindi kwa CCM Shinyanga Mjini ni dhahiri, naungwa mkono na makundi yote ya vijana, wazee na wanawake, na zaidi, naungwa mkono na wenzangu ndani ya CCM jimboni, mkoani na ngazi ya taifa kwa sababu ya utiifu na upendo wangu kwa wenzangu wote,” aliongeza kusema Masele.


Tatizo ni uhasama wa kale
Katika sakata hili kufikia Dk. Magufuli kumtaja Gaspar Kileo, kidole ananyooshewa mgombea ubunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele, ambapo wawili hao wana historia fupi ya uhasama, chimbuko lake ni kinyang’anyiro cha ubunge na urais.


Inafahamika kwamba, kabla na baada ya Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya ufisadi wa kampuni tata ya Richmond, Edward Lowassa, kutangaza nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano, wawili hao, Masele na Kileo, na vigogo wengine wengi wa CCM mkoani Shinyanga, wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Chama hicho aliyejiuzulu na kuhamia Chadema, Hamis Mgeja, walijipambanua wazi wazi na kambi ya Lowassa, maarufu kama “Team Lowassa”, kwa hali na mali.


Siku Lowassa alipokwenda Shinyanga kutafuta wadhamini, ni Mgeja, Kileo, Masele na baadhi ya wengine, walioandaa “mafuriko” ya wadhamini hata kumwezesha mtia nia huyo wa CCM kupata rekodi ya wadhamini zaidi ya 22,000. Kabla ya hapo, vigogo hawa na wapambe wao walihudhuria sherehe ya Lowassa ya kutangaza nia huko Monduli wakiwa wamesheheni viashiria vya uwezesho kwake kwa hali na mali.


Kati ya mawaziri na naibu waziri wa Serikali ya Jakaya Kikwete, ni Stephen Masele pekee aliyethubutu kuvunja (kwa kuelewa au kutoelewa), miiko ya utawala kwa mtu wa ngazi yake, alipojipambanua hadharani na kambi ya mgombea urais (Lowassa), alipowasili Shinyanga kutafuta wadhamini, kwamba yeye (Masele), hakuona mwana-CCM bora zaidi wa kumrithi Kikwete ila Lowassa pekee.


Ushirikiano huo kati ya Kileo na Masele chini ya “Team Lowassa”, ulifuta uhasama wa awali wa wawili hao, kutokana na fununu kwamba Kileo alikusudia kuwania Jimbo la Shinyanga Mjini na kuzua hasira ya Masele kufikia kutishiana maisha.


Ushindi wa Masele gumzo
Ndani ya Jimbo la Shinyanga Mjini kumekuwapo na taarifa za mkanganyiko kuhusu nani hasa anaweza kuibuka mshindi wa nafasi ya ubunge kwenye jimbo hilo.


Wakati katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mgombea wao wa ubunge, Patrobas Katambi, wakiamini wanaweza kushinda dhidi ya Masele wa CCM, Masele naye anaamini anao uwezo wa kutosha wa kushinda, kwa sababu kadhaa.


Mojawapo ya sababu za ushindi wa Masele zinatajwa kuwa ni ushiriki wake katika kuisaidia timu ya Soka ya Shinyanga, maarufu kama Stand United, kusaidia kupata mikopo vikundi kadhaa vya ujasiriamali vya wanawake na makundi ya vijana.


Lakini bia, wapo wachambuzi wa siasa za Shinyanga Mjini wanaohusisha uenyeji wa Masele na Katambi, wakisema Katambi ni mwenyeji wa Jimbo la Sengerema, tofauti na mshindani wake huyo, ambaye ni mwenyeji wa hapo, japo kwa siasa za sasa, uenyeji wa eneo si kigezo muhimu.


Hata hivyo, inaelezwa kwamba ndani ya Chadema kuna minyukano inayotokana na uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema kumpitisha mgombea wa sasa kuwania ubunge badala ya yule aliyeshinda kura za maoni, lakini pia, inaelezwa kwamba kwa sasa, kuna uwezekano wa Masele kukabiliwa na nguvu kinzani kutoka ndani ya CCM, hasa baada ya Gaspar Kileo kuonesha moja kwa moja, yeye binafsi au wapambe wake kukerwa na kauli ya Magufuli inayohusishwa na Masele na baadhi ya wanasiasa wa Shinyanga Mjini.


Wanasiasa hao wanadai kwamba Masele alimfuata Magufuli kumlaki Geita kabla ya kuingia Mkoa wa Shinyanga na kumwelezea kwa faragha hali ya Chama mkoani na vituko alivyokuwa akitendewa, taarifa inayotajwa kumkera Magufuli na kuanza kuifanyia kazi angali Geita na Kahama, kabla ya kuingia Shinyanga, juu ya aliowaita ndumilakuwili.


Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, Masele aliponea tundu la sindano kwa kumzidi kura moja mpinzani wake kutoka Chadema, Mwanabyula Shelembi, aliyepinga matokeo hayo Mahakama Kuu lakini alifariki dunia kabla ya kesi kuanza kusikilizwa.


Kauli kipimo cha uongozi
Wakati makada wengi wakimhukumu Masele kwa kupandikiza chuki ndani ya Chama, baadhi ya wananchi nao wametupa lawama kwa Magufuli kwa hulka ya kukosa subira na tafakuri ya mambo kabla ya kutenda wakisema, hulka kama hiyo inaweza kuzaa udikteta na uamuzi usio na mantiki akiingia madarakani kama hatabadilika.


Na kwa hali ya kisiasa ya mkoa ilivyo sasa, mwenendo wa Masele na kauli ya Magufuli ambayo vimeibua chuki miongoni mwa wapiga kura na kutikisa mshikamano ndani ya Chama; hali inayomweka katika nafasi mbaya zaidi mgombea huyo wa ubunge wa Jimbo la Shinyanga mjini dhidi ya upinzani. 


- See more at: http://raiamwema.co.tz/magufuli-apoteza-mwelekeo#sthash.LPraOlQL.dpuf

No comments :

Post a Comment