Akizungumza na Nipashe Mjini Zanzibar jana, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Zanzibar, Hamida Cheo, mgawanyo wa viti maalum ndani ya chama hicho umeibua malalamiko ya wanachama upande wa Zanzibar.
Alisema kuna wanachama wanahoji utaratibu uliotumika Zanzibar kupewa nafasi mbili tu kati na 36 za ubunge wa viti maalum ilizopata Chadema.
Alisema baada ya uchaguzi mkuu kukamilika Chadema imefanikiwa kupata viti 35 vya ubunge wa majimbo na 36 vya viti maalum, lakini Zanzibar imepata nafasi mbili kati ya majina yaliyokuwa yamependekezwa kabla ya kufanyika mgawo.
“Kumejitokeza malalamiko, kuna wanachama wanadai Zanzibar imepunjwa mgawo wa viti maalum baada ya kupewa nafasi mbili kutoka nafasi nne mwaka 2010,” alisema Cheo.
Hata hivyo alisema kwamba malalamiko hayo yameanza kufanyiwa kazi kwa kutumia taratibu za kichama na kuwataka wanachama hao kuwa na moyo wa subira kabla ya kupatikana muafaka.
Kwa upande wake, Mratibu wa Bawacha mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Nasra Baruan, alisema Zanzibar ni nchi na siyo mkoa, hivyo haikuwa muafaka kupewa nafasi mbili kati ya 36 za viti maalum.
Alisema kutokana na mafanikio iliyopata Chadema katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, walitarajia katika hesabu za harakaharaka Zanzibar ingepata viti visivyopungua vitano.
Alisema vyama vya upinzani vinatakiwa kuwa mfano katika kuweka usawa baina ya pande mbili za muungano badala ya kuongeza kero baina ya pande hizo.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment