Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti mjini Zanzibar jana, wananchi hao walisema kuwa, Rais Magufuli amewakuna kutokana na kazi nzuri anayofanya ya kufuatilia kwa vitendo kero za wananchi hasa katika maeneo nyeti ya upatikanaji wa huduma za kijamii na kujenga misingi ya uwajibikaji kwa watumishi wa umma.
Mmoja wa wananchi hao, Asha Seif Makame, mkazi wa Mkunazini alisema kitendo cha Rais kutembelea maeneo yenye kero katika upatikanaji wa huduma za jamii ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wanyoge ambao wamekuwa wakishindwa kupata huduma nzuri kutokana na umasikini.
Alisema wananchi wanyonge wamekuwa wakiteseka na wakati mwingine kufa kutokana na kushamiri kwa michango na rushwa katika maeneo ya upatikanaji wa huduma muhimu za jamii ikiwamo matibabu.
Mwananchi mwingine, Juma Shaame Ali, mkazi wa Mbweni alisema Mungu amesikia kilio cha Watanzania kwa kuwapatia kiongozi anayejali matatizo ya wananchi hasa wanyonge.“Mungu amesikia kilio cha Watanzania shida yetu kubwa ilikuwa kupata kiongozi mwenye uwezo wa kuondoa kero katika huduma za jamii,” alisema Ali. Akimtaka Rais Magufuli kuhakikisha kasi yake ya kukagua maeneo yenye kero katika upatikanaji wa huduma za jamii iwe ya kudumu na viongozi na watendaji wote wafuate nyayo zake.
“Rais Magufuli hawezi kumaliza tatizo la rushwa na ukosefu wa uwajibikaji peke yake bila ya kuungwa mkono na viongozi na watendaji wake,” alisema Ali.
Naye Mwajuma Mrisho Issa, mkazi wa Tunguu, alisema wananchi wamekuwa wakiteseka kuanzia ngazi za vijiji, wilaya hadi mkoa katika upatikanaji wa huduma bora kutokana na matatizo ya rushwa, kukithiri kwa michango na utendaji mbovu.
Alisema wagonjwa wanaopewa rufaa kutoka Zanzibar wengi wamekuwa wakiteseka na wakati mwingine kufa kutokana na kushindwa kumudu gharama za matibabu ikiwamo rushwa na michago.
Mwajuma alitaka kasi ya kuondoa kero isiishie Tanzania Bara, bali pia ifike Zanzibar kutokana na taasisi nyingi za muungano kukabiliwa na tatizo la rushwa, michango na urasimu kama polisi, uhamiaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Hata hivyo, Said Suleiman Kibonge, mkazi wa Kikwajuni alisema hana matumaini makubwa na utendaji wa Rais Magufuli kwa vile viongozi wengi waliomtagulia walianza vizuri na kushindwa kuendeleza mabadiliko wanayoyataka wananchi wao.
“Tume shuhudi ahadi nyingi lakini hakuna utekelezaji hadi serikali ya awamu ya nne imemaliza muda wake, ndiyo maana nasema isije kuwa nguvu ya soda,” alisema.
Alisema kazi ya kupambana na rushwa, uwajibikaji na kuondoa urasimu inatakiwa iwe ajenda ya pamoja ya viongozi wote na watendaji wakuu badala ya Rais peke yake.
Utendaji wa Rais Magufuli umeibua mjadala mkubwa katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar na kufufua matumaini kwa wananchi ya kuondokana na kero katika upatikanaji wa huduma za kijamii.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment