Maalim Seif pia alikuwa Mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu uliofanyika Oktoba 25.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana jioni, ilieleza kuwa viongozi hao walikutana jana Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa viongozi hao wawili walikutana kwa takribani saa moja Ikulu, kuzungumzia hali ya kisiasa Zanzibar kufuatia ombi la Maalim Seif kutaka kukutana na kuzungumza na Rais Kikwete.
“Viongozi hao wamekubaliana kuwa mashauriano yaendelee kufanyika baina ya pande zote zinazohusika na hali ya kisiasa Zanzibar,” taarifa hiyo ilieleza kwa kifupi.
Zanzibar inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa, baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) kufuta matokeo ya Uchaguzi wa Rais na uwakilishi wa Zanzibar, kwa maelezo kuwa ilibaini kuwapo kwa kasoro kadhaa kisiwani Pemba.
Uamuzi wa kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu ulitangazwa na Mwenyekiti wa Zec, Jesha Salim Jecha, Oktoba 28, mwaka huu na kuibua mgogoro.Katika tangazo la kufuta matokeo hayo, Jecha alisema uchaguzi huo utarudiwa, lakini Maalim Seif, viongozi na wafuasi wa CUF wanapinga kurudiwa kwa uchaguzi huo na kusisitiza kwamba Maalim Seif anapaswa kuapishwa.
Waangalizi wa kimataifa na wa ndani pia walieleza kushangazwa kwao na hatua ya Jecha kufuta matokeo hayo wakati hawakushuhudia kasoro zozote wakati wa upigaji kura kisiwani Pemba hadi baada ya kutoa taarifa yao ya kwanza.
Mataifa kadhaa ya nje yakiwamo Uingereza, Ireland na Marekani pia yalieleza kushangazwa na uamuzi wa wao na kushauri Zec iendelee na mchakato wa kutangaza matokeo.
Hata hivyo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa taarifa za kukubaliana na uamuzi wa Zec wa kufuta matokeo na kutaka uitishwe uchaguzi mpya.
Kabla Maalim Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar hajakutana na Rais Kikwete jana, alilalamika kwamba alikuwa akiwapigia simu pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, bila kuzipokea kwa lengo la kutaka kutafuta suluhisho la mgogoro huo.
Wadau kadhaa wameshaingilia kati kusaka suluhu kwa kukutana na pande zinazohusika. Miongoni mwao mi Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, viongozi wa dini na viongozi wastaafu.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment