Wakati akiomba kura kwa wananchi, Dk. Magufuli aliyekuwa akipeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) alitoa ahadi kadhaa za kuvutia chini ya kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Mwishowe, baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, Magufuli alitangazwa mshindi wa asilimia zaidi ya 58 ya kura halali zilizopigwa na kuwapiku wapinzani wake saba, akiwamo Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo aliyekuwa akiwakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Mbali na Chadema, Ukawa huundwa pia na Chama cha Wananchi (CUF), nccr-Mageuzi na NLD.
Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wananchi walisema wana hamu kubwa ya kuona Magufuli akiapishwa na kuingia Ikulu kwani kufanya hivyo kutamuwezesha kuanza rasmi kutekeleza yale aliyokuwa amewaahidi Watanzania.“Hii ni siku muhimu kwa hatma ya taifa. Ni kwa sababu Magufuli akishaapishwa kesho (leo) na kukabidhiwa ofisi na Rais Jakaya Kikwete, atakuwa ni kama amepewa rungu la kuashiria mwanzo mpya wa uongozi chini ya usimamizi wake,” alisema mkazi mmoja wa Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina moja la Beatrice.
Mkazi mwingine wa Kinondoni aitwaye Shafii Iddi, aliiambia Nipashe kuwa siku ya kuapishwa kwa Magufuli (leo) ni muhimu zaidi kwani ndiyo mwanzo wa kuanza kazi kwa serikali ya awamu ya tano na hivyo kupata nafasi ya kuona Watanzania wakipata elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne.
“Kwakweli hivi sasa hali ni ngumu. Serikali inayoondoka imejitahidi kufanya mengi lakini bado kuna mambo hayaendi vizuri… maji shida, dawa hospitalini hakuna, wagonjwa wengi wanalala chini, michango imekuwa mingi na thamani ya shilingi inashuka kila siku. Naamini Magufuli akianza tasmi kazi haya yote yatakwisha kama alivyotuahidi,” alisema Shafii.
AHADI ZA TRILIONI 63/-
Uchunguzi wa Nipashe uliofanywa kwa kutumia rejea mbalimbali za ahadi za wagombea wakati wa kampeni ulibaini kuwa Magufuli alikuwa ni miongoni mwa wale waliokuwa wakitoa ahadi zilizotoa matumaini makubwa kwa Watanzania, huku ufafanuzi wake juu ya namna ya kuzitekeleza na kuondoa kero mbalimbali pindi akiingia madarakani ukiwavutia wengi karibu katika kila mkutano aliofanya.
Kupitia uchunguzi wake huo, Nipashe ilibaini kuwapo kwa ahadi kubwa tano zilizokuwa maarufu na kutoa matumaini makubwa kwa wananchi juu ya kuwapo kwa mabadiliko ya kweli kupitia Magufuli. Ahadi hizo ni zile zilizohusiana na elimu, afya, miundombinu ya reli na barabara, ununuaji wa meli na pia kushirikisha wananchi katika shughuli za uchumi kwa kuahidi kugawa Sh. Milioni 50 kwa kila kijiji na kila mtaa.
Uchunguzi ulibaini kuwa, ikiwa ahadi za Magufuli zitatekelezwa kwa asilimia 100, Tanzania itaondokana na hali duni ya upatikanaji wa baadhi ya huduma za kijamii na pengine kuonekana kama mojawapo ya nchi zilizoendelea barani Ulaya.
Kwa ujumla, serikali ya Magufuli inatarajiwa kutumia wastani wa Sh. trilioni 63.64 ili kutimiza ahadi zake kuu tano katika kipindi cha miaka mitano ya kuwa madarakani. Wastani wa gharama hizo za ahadi tano za Magufuli (Sh. trilioni 63.64) ni sawa na asilimia 56.58 ya bajeti ya sasa ya Serikali kwa miaka mitano (Sh. trilioni 112.475), ikiwa kiwango chake kitabaki mara zote kuwa kama cha bajeti ya mwaka 2015/16, ambayo ni Sh. trilioni 22.495 kama ilivyowasilishwa na kupitishwa na bunge Juni mwaka huu mjini Dodoma.
1. ZAHANATI, VITUO VYA AFYA (Sh. trilioni 29.15)
Kwa vyovyote vile, ahadi ya Magufuli kuhusiana na kuboresha hufuma za afya ilichangia kwa kiasi kikubwa ushindi wake.
Alisisitiza kuwa akiingia Ikulu, atahakikisha anajenga zahanati katika kila kijiji, kituo cha Afya katika kila kata, hospitali katika kila wilaya na hospitali ya rufaa katika kila mkoa.
Kwa mujibu wa msemaji wa iliyokuwa kamati ya kampeni ya CCM, January Makamba, hadi sasa asilimia 40 ya vijiji nchini tayari vina zahanati na hivyo, kazi ya serikali itakayoongozwa na Magufuli itakuwa ni kumalizia ujenzi katika asilimia 60 ya vijiji vyote nchini.
Takwimu za Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na nyingine zilizofikishwa kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ajili ya uchaguzi mkuu Oktoba 25, idadi ya vijiji vyote nchini ni 19,200; idadi ya kata ni 3,957; idadi ya wilaya ni 133 na idadi ya mikoa ni 31. Hivyo, ili kutimiza ahadi ya kuwa na zahanati katika kila kijiji, serikali ya Dk. Magufuli italazimika kujenga zahanati mpya 11,520, ambayo ni asilimia 60 ya idadi ya vijiji ambavyo bado havijawa na zahanati.
Taarifa ambazo gazeti hili ilizipata kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia uchunguzi wake uliochapishwa katika toleo la Nipashe la Oktoba 15, 2015, zilibainisha kuwa wastani wa kujenga zahanati moja yenye sifa zinazostahili hadi kukamilika kwake ni Sh. bilioni 1.3; kituo cha afya ni Sh. bilioni 5.5; Hospitali ya Wilaya Sh. bilioni 30 na hospitali ya mkoa kuwa na hadhi ya rufaa ni Sh. bilioni 80. Hata hivyo, inaelezwa kuwa gharama hizi zaweza kupungua au kuongezeka kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za mahala husika na nguvu ya soko.
Kwa sababu hiyo, gharama za jumla ambazo serikali ya Magufuli inatarajiwa kuzibeba baada ya kuapishwa leo kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika vijiji 11,520 ni Sh. trilioni 14.98.
Kadhalika, Nipashe inatambua kuwa baadhi ya kata nchini tayari zina vituo vya afya, kama ilivyo kwa wilaya ambazo baadhi tayari zina hospitali zake na pia baadhi ya mikoa tayari ina hospitali zenye hadhi ya rufaa. Kwa sababu hiyo, ikiwa itakadiriwa kuwa serikali ya awamu ya tano ya Magufuli itawekeza katika kufanikisha upatikanaji wa vituo vya afya walau katika nusu ya kata zote nchini, yaani kata 1,979, maana yake italazimika kutumia Sh. trilioni 10.88.
Ikiwa itakadiriwa kuwa nusu ya idadi ya wilaya zitajengewa hospitali za hadhi yake, yaani wilaya 67, maana yake serikali ya Magufuli itatumia Sh. trilioni 2.01 kukamilisha miradi hiyo. Aidha, serikali ya Dk. Magufuli italazimika pia kutumia Sh. trilioni 1.28 ikiwa walau nusu ya idadi ya mikoa yote nchini (mikoa 16) itawezeshwa kuwa na hospitali zake za rufaa kwa gharama ya Sh. bilioni 80 kwa kila moja.
Kwa ujumla, makadirio haya yanaonyesha kuwa serikali ya Rais Dk. Magufuli itatumia Sh. trilioni 29.15 ili kutimiza ahadi ya kujenga zahanati kwa kila kijiji, kituo cha afya kwa kila kata, hospitali ya wilaya kwa kila wilaya na hospitali ya rufaa kwa kila mkoa.
Aidha, Magufuli ameahidi pia kujaza dawa na vifaa tiba katika taasisi zote za afya za serikali ili kuwaondolea wananchi usumbufu wa sasa wanaoupata kwa kuandikiwa tu cheti na kuambiwa wakanunue dawa kwenye maduka binafsi.
2. RELI MPYA, BARABARA, FLYOVERS (Sh. trilioni 19.86)
Ahadi hii iliwahi pia kutolewa na serikali ya Rais Kikwete inayomaliza muda wake baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25. Ikitekelezwa kwa uhakika kutokana na kile anachoahidi Magufuli, ni wazi kuwa serikali ya Dk. Magufuli itakuwa imefanya kazi ya kihistoria.
Akizungumza katika mkutano wake mmoja wa kampeni kwenye viwanja vya Kawawa mkoani Kigoma, Magufuli alisema atajenga reli mpya ya kati (kiwango cha standard gauge) itakayoondoa matatizo ya usafiri kwa wakazi wa mkoa huo na mingine ya kanda za Magharibi, Kati na Ziwa. Kwa mujibu wa mtandao wa a4architect.com, Reli ya kiwango hicho (standard gauge), huwa na upana wa mita 1.435 na siyo mita 1.067 kama ilivyo kwa reli zilizojengwa enzi za ukoloni.
Mtandao huo (a4architect.com) unaonyesha kuwa kampuni ya ujenzi ya China Communications Construction Limited (CCC LTD), imetoa makadirio ya gharama za kujenga reli ya kiwango cha 'standard gauge' kutoka Kenya,Uganda hadi Rwanda kuwa kilomita moja ni shilingi za Kenya milioni 413, sawa na Sh. bilioni 8.4 za Tanzania. Na kwa mujibu wa kikokotozi cha mtandao wa Distancefrom, makadirio ya umbali wa barabara kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma ni kilomita 1,367.
Kwa sababu hiyo, ili kutekeleza ahadi ya Magufuli kwa kujenga reli ya 'standard gauge' kwa kiwango sawa na mradi wa reli ya Kenya - Uganda hadi Rwanda, maana yake zitahitajika takriban Sh. trilioni 11.48.
Kadhalika, kikokotozi cha mtandao wa Distance from kinaonyesha zaidi kuwa makadirio ya umbali wa ardhini kutoka Tabora hadi Mpanda ni Kilomita 244 na pia kutoka Tabora hadi Mwanza ni Kilomita 278. Hivyo, jumla ya umbali wa reli mpya kutoka Tabora hadi Mwanza na nyingine ya kuelekea Mpanda ni kilomita 522. Ikijengwa reli ya kiwango kama cha Kenya, Uganda na Rwanda, maana yake serikali ya Rais Dk. Magufuli itagharimia kiasi kingine cha Sh. trilioni 4.38.
Kadhalika, Magufuli mwenyewe ameahidi pia kuongeza mtandao wa barabara za lami nchini kutoka kilomita 17,000 zilizopo sasa hadi kufikia zaidi ya kilomita 21,000. Hii maana yake ni kwamba serikali itakayokuwa ya Magufuli itajenga barabara moja ya urefu wa Kilomita 4,000. Ikiwa wastani wa kujenga Kilomita moja ya barabara ya lami ni Sh. bilioni moja, maana yake serikali ya Magufuli italazimika kutumia takriban Sh. trilioni 4 kutimiza ahadi hii.
Hivyo, ili kukamilisha miradi yote ya reli mpya kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma,Tabora - Mpanda na Tabora - Mwanza na pia kutandaza barabara za lami, serikali ya Magufuli italazimika kutumia Sh. trilioni 19.86.
3. ELIMU BURE HADI KIDATO CHA NNE (Sh. trilioni 5.14)
Karibu katika mikutano yake yote, Magufuli alisisitiza kuwa serikali yake itatoa elimu bure kwa kila mtoto wa Tanzania hadi kufikia kidato cha nne.
Hivi sasa, elimu ya msingi hutolewa bure pia ingawa wapo wazazi hulalamika kuwa wingi wa michango ni mzigo mkubwa, pengine kuliko hata ada. Serikali ya Rais Magufuli inatarajiwa kumaliza pia kero hii ya mlolongo wa michango.
Katika hotuba yake wakati wa kilele cha maadhimisho ya pili kitaifa ya wiki ya elimu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Mei 15 mwaka huu, Rais Kikwete alisema hadi kufikia mwaka 2014, idadi ya wanafunzi wa shule za msingi nchini ilikuwa ni milioni 8.23 na idadi ya wanafunzi wa shule za sekondari ni 1,804,056.
Katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwa wastani wa gharama za michango kwa kila mwanafunzi kwa mwaka katika Shule ya Msingi Tumaini iliyopo Iringa ni Sh. 70,000, hii ikijumuisha umeme, maji na ulinzi. Kwa sababu hiyo, ikiwa kila mwanafunzi wa shule ya msingi nchini atakuwa akilipia michango ya kiwango sawa na shule hiyo ya Tumaini ya Iringa, maana yake ni kwamba gharama za jumla kwa wanafunzi wote ni Sh. bilioni 576.1 na kwa miaka mitano ya kuwa madarakani, serikali ya Magufuli itatumia Sh. trilioni 2.88.
Kadhalika, uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa licha ya kuwapo kwa ada nafuu ya Sh. 20,000 kwa shule za kutwa na Sh. 70,000 kwa shule za sekondari, bado michango imekuwa tatizo kubwa. Kwa mfano, mwanafunzi aliyeanza kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya kutwa ya Kihesa iliyopo Iringa mwaka huu alitakiwa kulipa takriban Sh. 250,000 kwa ajili ya ada, michango mbalimbali na vifaa kama panga, kwanja na jembe. Hata hivyo, haya ni makadirio tu kwani Nipashe inatambua kuwa michango hutofautiana kati ya shule moja na nyingine kutokana na sababu mbalimbali.
Ikiwa kila mwanafunzi wa sekondari nchini atakuwa akitozwa ada na michango kwa kiwango sawa na wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza wa shule hiyo ya Kihesa, maana yake gharama zote zitakazokuwa zikibebwa na serikali ya Magufuli kwa mwaka zitakuwa ni Sh. bilioni 451.01, hivyo kwa miaka mitano itakuwa Sh. trilioni 2.26.
Kwa sababu hiyo, gharama zitakazolipwa na serikali ya Magufuli ili kutekeleza ahadi ya elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne kwa miaka mitano ya kuwa madarakani itakuwa ni Sh. trilioni 5.14.
4. MILIONI 50 KILA KIJIJI, MTAA (Sh. trilioni 1.15)
Magufuli aliahidi tangu siku ya kwanza ya kampeni zake, kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam, Jumapili ya Agosti 22 kwamba atagawa milioni 50 kwa kila kijiji na kila mtaa.
Lengo la fedha hizo ni kwa ajili ya kuwapa mikopo vijana na kina mama ili ziwasaidie kwa shughuli za ujasiriamali.
Kwa mujibu wa Tamisemi, mbali na kuwapo kwa vijiji 19,200, pia kuna mitaa 3,741. Kwa sababu hiyo, serikali ya Rais Magufuli italazimika kutumia fedha hizo katika maeneo 22,941 (jumla ya vijiji na mitaa), hivyo gharama zote kufikia takriban Sh. trilioni 1.15.
5. MELI MPYA MAZIWA MAKUU (Sh. bilioni 833.7)
Akiwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Magufuli alisema atatimiza ahadi zilizowahi kutolewa na Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake kwani zote hizo ni sawa na 'amri'. Miongoni mwa ahadi alizozikumbushia Magufuli ni ununuzi wa meli mpya katika maziwa makubwa nchini ya Victoria, Tanganyika na Nyasa, lengo likiwa ni kumaliza kero ya usafiri katika maeneo ya mikoa yenye maziwa hayo.
Kwa mujibu wa mtandao wa ships4ever.com, bei ya meli ya mtumba iliyotengenezwa mwaka 2001, ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 850 ni euro milioni 115, sawa na Sh. bilioni 277.9. Kwa sababu hiyo, ikiwa maziwa yote matatu yatanunuliwa meli za sifa hii, maana yake serikali ya Rais Dk. Magufuli itatimiza ahadi hii kwa kutumia Sh. bilioni 833.7 ndani ya miaka yake mitano.
TATHMINI YA WASOMI
Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma) wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mtakatifu Stefano Moshi (SMMUCo), Dk. Gasper Mpehongwa, aliwahi kuiambia Nipashe kuwa baadhi ya ahadi zinatekelezeka iwapo kutakuwa na matumizi mazuri ya fedha na kuongeza makusanyo ya kodi.
"Kwa mfano, wakurugenzi wa halmashauri wanatumia mashangingi (magari aina ya Land Cruiser) ya gharama kubwa... kukiwapo udhibiti wa matumizi ya fedha za serikali, ahadi nyingi zinazotolewa zinaweza kutekelezeka,” alisema Dk. Mpehongwa.
Mhadhiri wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe (Dar es Salaam), Profesa Prosper Ngowi, aliwahi pia kuiambia Nipashe kuwa ahadi kama za Magufuli zinawezekana kutekelezwa iwapo kutakuwa na misingi iliyo imara ya kupata fedha hizo.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment