Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, November 4, 2015

Kivumbi kijacho baada ya uchaguzi!


Na Ahmed Rajab
NINAYAANDIKA makala haya nikiwa gizani.Giza totoro lenye kunitotora akili. Giza la kutojua matokeo kamili, na rasmi, ya Uchaguzi Mkuu wa Jumapili iliyopita. Kura zilipigwa baada ya siku 64 za kampeni, za mchuano mkali baina ya vyama vya siasa.

Tatizo nililo nalo ni kwamba ninapoyaandika haya bado kura hazijamalizwa kuhesabiwa. Hadi sasa ni Dk. John Magufuli, mgombea urais wa Tanzania kutokea Chama cha Mapinduzi (CCM), ndiye anayeongoza katika matokeo ya majimbo yaliyokwishatangazwa rasmi na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (Nec). Uwezekano uliopo ni kwamba yeye ndiye atayeibuka mshindi.

Kwa upande wa Zanzibar, dalili zinaonesha kwamba mshindi wa urais wa huko ni mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad. Mgombea huyo wa CUF akiungwa mkono na vyama vingine vitatu vilivyo katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Juu ya yote hayo, sina uhakika nini hasa kitachotokea Visiwani wakati gazeti hili likiwa mitamboni. Je, wale waliozoea kujigamba kwamba hawatoitoa serikali ya Zanzibar kwa karatasi, yaani kwa kura, wataendelea kuushika uzi wao huo huo?
Watakuwa na ubavu kweli wa kufanya dhulma na kwenda kinyume cha matakwa ya wananchi mbele ya macho ya ulimwengu?

Tayari tunasikia kwamba viongozi wa CCM/Zanzibar wamekuwa wakilalamika wakiyakataa matokeo hayo na huenda kwa ukaidi wao wakaamua kutoitoa serikali. Hatua hiyo bila ya shaka itauhatarisha mchakato mzima wa demokrasia nchini na huenda ikahatarisha hali ya amani, utulivu na hata maisha ya watu.

Rais Ali Mohamed Shein, aliyekuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi huo, alikwishajitwika dhima ya kuwa yeye ni muadilifu alipoahidi kwamba uchaguzi utakuwa wa haki. Heshima yake itaanguka asipotenda haki na akageuka kuwa mtu asiyeaminika.

Hatari iliyopo ni kwamba endapo hatua yake ya kuyakataa matokeo ya uchaguzi itasababisha umwagaji wa damu basi anaweza akafikishwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) mjini Hague, Uholanzi. Si yeye tu bali yeyote yule atayebainika kwamba ni mchochezi wa mauaji ya kisiasa.

Ni matumaini ya wengi kwamba Shein ataepusha vurugu kwa kuyakubali matokeo na kushika wadhifa wa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama Katiba ya Zanzibar inavyoainisha.

Kwa sasa sina uhakika ni watu wangapi hasa walioitumia haki yao ya kikatiba kwenda kupiga kura.
Ninajuwa kwamba waliosajiliwa kuwa na sifa zinazohitajiwa, na kwa hivyo kuwa na haki hiyo ya kupiga kura, walikuwa watu milioni 22 na laki saba ushei. Hata hivyo, idadi hasa ya waliotumbukiza karatasi zao za kura kwenye masanduku ya kura bado siijui.

Nijuavyo ni kwamba walikuwa wengi, tena wengi sana katika nchi zote mbili zilizo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wengi wao walikuwa vijana.
Hilo halikunishangaza kwa sababu uchaguzi huu uliwatia watu jazba na hamasa isiyo kifani. Tena wananchi wameonesha kuwa wana mwamko mkubwa wa kisiasa. Walipikwa, wakapikika.

Vyama vya siasa ndivyo vilivyokuwa wapishi. Kwa kiwango kikubwa, vilifanikiwa katika kampeni zao za muda wa miaka mitano za kuwaelimisha na kuwashawishi Watanzania.

Kwa mara ya kwanza tangu ukomeshwe mfumo wa chama kimoja cha siasa, safari hii mchuano ulizidi kuwa mkali kati ya vyama vya siasa. Kuna Watanzania wengi, hususan vijana, walioamini kwamba kulikuwa na uwezekano wa kweli wa kupatikana mabadiliko ya watawala wa taifa hili.Uwezekano huo ulikuwa mkubwa zaidi Zanzibar.

Kwa kipindi kirefu sana Chama cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa kama ng’ombe mtakatifu katika siasa za Tanzania. Tumetoka naye mbali ng’ombe huyu, yeye na wazazi wake, Tanganyika African National Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP). Kwa muda mwingi tukivicha vyama hivyo vilivyokuwa vikitawala bila ya ushindani wowote uliokuwa halali katika Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

Kwa kipindi chote hicho, vyama hivyo vilikuwa juu ya serikali za nchi zao.Kwa hakika, vikizikalia vichwani serikali hizo. Hazikuweza kufurukuta.

Hali ilikuwa hiyo hiyo, vyama hivyo vilipooana na kuzaliwa Chama cha Mapinduzi (CCM) 1984. Nacho pia kilitawala bila ya upinzani wowote wa halali. 

Kilijifanya kuwa ni adhimu kushinda serikali au taasisi yoyote ile nchini. Wakati mwingine kikijifanya kuwa kama ndio serikali kwa kuyatwaa madaraka ya serikali. Hatutakosea tukisema kwamba chama kilikuwa na udikteta wa aina yake, udikteta wa chama kimoja.

Ndipo wengi wa Watanzania walipozidi kukiona Chama hiki, CCM kama ng’ombe mtakatifu, wakiona itakuwa sawa na kufanya dhambi kumkemea au kujaribu kumuongoza. Alikuwa ng’ombe wa ajabu kwa sababu yeye ndiye aliyekuwa akiwatia watu shemere, wayafuate ayatakayo.

Aliyethubutu kukipinga chama hadharani akionekana kama ni haini si wa chama tu bali hata wa taifa zima. Waliokuwa na ujasiri wa kupinga walipinga chini kwa chini. Hawalaumiki kwani wakiyahofia maisha yao. Hofu iliwavaa kwa vile wakikabiliwa na upanga wa sheria ya kuwaweka watu kizuizini bila ya kuwafikisha mbele ya mahakama.

Sheria hiyo ikitumika Bara tangu siku ambapo Tanganyika ikitawaliwa na TANU. Zanzibar ndo usiseme tena; huko hata sheria haikuweko. Watu wakitumbukizwa tu gerezani, wakiteswa, wakiuliwa na wengine wamepotea hadi leo hawajulikani walipo.

Hakuna aliyethubutu kukisemesha au kukigusa chama cha ASP. Kutamalaki kwa CCM kulisaidia, kwa kiwango kikubwa, kupunguza ukatili wa watawala wa Zanzibar. Hata hivyo, bado chama kilikuwa adhimu, kilikuwa juu ya serikali seuze watu wa kawaida.

Hali ya mambo ilianza kubadilika katika mwisho wa miaka ya 80, na mwanzoni mwa miaka ya 90, pale upinzani uliokuwa ukifukuta chini kwa chini ulipoanza kujichomoza. Watanzania wakaanza kumuangalia yule ng’ombe mtakatifu kwa jicho jengine.

Walipomuona hasa alivyo wakaanza kumtoa maanani. Walitanabahi kuwa kumbe hana lake jambo, kwamba hana utakatifu wowote isipokuwa ufisadi na ukiritimba wa kisiasa. Enzi zake za heshima na taadhima zilikuwa zimekwisha na chama chenyewe kilipitwa na wakati. Kumbukumbu bado hazijachakaa katika ukumbi wa historia ya mchuano wa siasa za vyama nchini Tanzania.

Kumbukumbu hizo zinaonesha jinsi mfumo wa chama kimoja ulivyozalisha ubazazi wa kisiasa na jinsi ulivyokuwa kizingiti kikubwa cha kuleta maendeleo nchini. Chama kilichokuwa kikitawala katika mfumo huo kilijisahau na kilijiona kwamba kinaweza kufanya kitakavyo bila ya kuwajibishwa.

Kwa bahati mbaya, hali hiyo iliendelea baada ya CCM kushinda katika chaguzi zote nne zilizopita. Upinzani haukuweza kukiondosha madarakani kwa sababu ulikuwa umegawika na kwa sababu hiyo ulikuwa dhaifu. CCM nusura kikione chake mwaka huu kwa vile kwa mara ya kwanza kilikabiliwa na upinzani ulioungana.

Hamna shaka yoyote kwamba chama hicho kilitaharaki bila ya kiasi hasa baada ya kuibuka kwa waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa kuwa mgombea wa urais wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema) akiungwa mkono na vyama vingine vitatu vilivyo katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

CCM kikaamua kuitoa mizinga yake ikiwa katika umbo la wastaafu — toka marais Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa na mstaafu mtarajiwa Jakaya Kikwete — hadi mawaziri wakuu Joseph Warioba, Cleopa Msuya na Salim Ahmed Salim. Wote walijitokeza kumnadi na kumpigia “debe” mgombea wao Dk. John Magufuli. Hiyo ndiyo iliyokuwa kete ya mwisho ya CCM kujinusuru.

Mchuano huo baina ya Lowassa na Magufuli ndio uliowachangamsha na kuwahamasisha zaidi wananchi. Matokeo yake, ambayo hayatotangazwa rasmi hadi kesho, ndiyo yatayotujulisha rasmi hatima ya ng’ombe mtakatifu.

Hadi sasahaioneshi kwamba ng’ombe huyo ameweza kuchinjwa. Nionavyo ni kuwa amefanikiwa kuwapiga mateke waliothubutu kujaribu kumlaza.

Kwa vile ameponea chupuchupu basi itabidi tukubali kwamba ng’ombe huyo si ng’ombe wa kawaida, bali ni gombe sugu, licha ya kwamba ndama wake wa Zanzibar ameweza kuchinjwa.

Uchaguzi huu umeyafungua macho yetu kwa mengi. Moja lililo muhimu ni kwamba umetudhihirishia jinsi chama kinachotawala chenyewe kisivyojiamini. 

Kitaifa, kililazimika kuendesha kampeni zake kwa nguvu kubwa zaidi na ustadi wa hali ya juu. 

Ninasema hivi kwa jinsi kilivyojaribu kuzitilia sana mkazo sifa za Magufuli kushinda mafanikio au sifa za chama.

Magufuli naye alijaribu kujiweka mbali na chama chake. Zaidi ya mara moja aliishambulia serikali ya chama hicho pamoja na chama chenyewe kwa maovu kadhaa yakiwa pamoja na ufisadi.

Aliposimama kwenye jukwaa wakati wa kuifunga kampeni yake alithubutu kumlaumu hadharani mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete kwa kuwapa uongozi watu wasiofaa. Alijigamba kwamba serikali yake itakuwa tofauti kwa kuwa “itakuwa kazi tu”. 

Kwa kusema hayo, alimaanisha kwamba serikali ya Kikwete haikuwa ikifanya kazi.

Aidha alikiri kwamba mna mafisadi ndani ya CCM kwani aliwataka wajiondoe wenyewe kabla hajapambana nao atapoapishwa.

Baada ya uchaguzi huu vyama vya siasa vitakabiliwa na changamoto nyingi. CCM hakitokuwa makini ikiwa kitaendelea kuendesha shughuli zake kama ilivyo kawaida yake. Mtikiso uliokikumba katika uchaguzi huu lazima ukiamshe na kitambue kwamba kiburi hakisaidii kitu. Lazima pia kiwe na ubavu wa kuyafufua yale maadili ya uongozi ambayo zamani yalikifanya chama hicho kionekana kuwa ni chama chenye uadilifu.

Ndani ya CCM/Zanzibar tayari viongozi wake wamekwishaanza kutupiana lawama baada ya Shein kushindwa kuunyakua urais wa Zanzibar.

Vyama vilivyo katika Ukawa navyo vitabidi viutathmini upya umoja wao na viandae mikakata mipya ya kupambana na CCM miaka mitano kutoka sasa.

Changamoto kubwa ni ile itayolikabili taifaMagufuli akiwa Rais mpya wa Tanzania na Maalim Seif Rais mpya wa Zanzibar. Changamoto hiyo itakuwa ni namna ya kulitanzua suala tete la Katiba mpya ya Tanzania na hasa suala la Muungano.

Hili ni suala ambalo lazima litazua mvutano mkubwa baina ya marais hao wawili. Kivumbi hicho kitazidi kupamba moto ikiwa idadi ya wapinzani itakuwa kubwa katika Bunge la Muungano.

- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/kivumbi-kijacho-baada-ya-uchaguzi#sthash.NdWuxUq2.dpuf

No comments :

Post a Comment