- Jinsi Mbowe alivyoipa CCM ushindi
- Mchango mkubwa wa Slaa, Lipumba
- Ngumu kuwaamini Sumaye, Ngombale
Mtazamo wa wakati huo ulikuwa kwamba kwa kumpokea Edward Lowassa, kama mgombea wa Chadema na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wangeweza kuishinda CCM kwa kuwa Lowassa alidhaniwa kuwa na nguvu kubwa ndani ya CCM na kuondoka kwake kungeweza kukisambaratisha, na hasa tambo zake kwamba angehama na viongozi wengi waandamizi wa CCM.
Kuingia 2015, na siku chache kabla ya harakati za uchaguzi kuanza, Chadema kilijipambanua kama chama makini kikikubalika kwa Watanzania wengi hasa kwa jinsi wabunge wake walioingia bungeni mwaka 2000, walivyoibana serikali kwa kuibua kashfa mbalimbali za ufisadi. Kwa taratibu na kwa uhakika, kilijijengea umaarufu kwa wananchi.
Hadi 2010, Chadema kilikuwa kimejipambanua kama kilichokuwa kimedhamiria kupambana na ufisadi bila suluhu na kwa hiyo kikawa tumaini la Watanzania waliochoshwa na udhaifu wa Serikali ya CCM kupinga ufisadi.
Kwa upande mwingine, kukosekana kwa dhamira ya dhati ya kupambana na vitendo vya kifisadi ndani ya chama tawala na kuendelea kukumbatia makada wake maarufu waliokuwa wakituhumiwa kwa rushwa kuliipa Chadema sura ya jukwaa la kupambana na ufisadi na kama chama mbadala kwenye vita dhidi ya ufisadi.
Hata hatua ya CCM kushindwa kujivua gamba ilizidi kufunua udhaifu wa chama hicho katika kupambana na ufisadi, hali iliyokiongezea Chadema heshima miongoni mwa Watanzania kuwa ndicho pekee chenye uwezo wa kupambana na ufisadi.
Mazingira hayo yaliwafanya Watanzania ambao walikuwa wamechoshwa na ufisadi serikalini kukiona Chadema kuwa ni chama mkombozi wao. Chenyewe kikaichukua ajenda hiyo kuwa ndio utambulisho wake, kiasi cha kukifikisha CCM katika kuanza kuwabagua wakada wake waliokuwa wanatuhumiwa kwa ufisadi kwenye baadhi ya shughuli za chama.
Mambo yalibadilika ghafla pale Lowassa alipojiunga na Chadema. Matokeo ya uchaguzi tunayoshuhudia yamechangiwa, pamoja na mambo mengine, na athari ya Lowassa kujiunga Chadema.
Msimamo wa Lowassa utata
Ndani ya mwezi mmoja, Lowassa alichukua fomu za kugombea urais kupitia vyama viwili tofauti na katika muda huohuo akawa anatoa kauli zinazokinzana kuhusu vyama hivyo viwili huku kauli hizo zikiibua shaka kuhusu kinachomsukuma kuomba urais.
Akitangaza nia kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais jijini Arusha, Mei 30, Lowassa alisema: “ Kiuchumi, tumeshuhudia ukuaji mzuri na kuongezeka kwa mapato ya ndani ya Serikali na uimarishaji wa mfumo wa uwajibikaji na ulipaji kodi. Kwa upande mwingine, Serikali ya Rais Benjamini Mkapa na Rais Jakaya Kikwete zimefanya kazi kubwa katika uendelezaji wa sekta ya mafuta na gesi asilia ambapo kiwango kikubwa cha gesi asilia kimegunduliwa.”
Hapo alikuwa akielezea mafanikio ya Serikali ya CCM, na jinsi atakavyoendeleza pale walipofikia waliomtangulia pindi atakapochaguliwa kuwa rais kupitia CCM.
Lakini siku chache baada ya CCM kukata jina lake asigombee urais kupitia chama hicho, mgombea huyo wa Ukawa alitoa kauli tofauti kabisa kuhusu CCM.
“Nitakuwa mnafiki kama nikiendelea kuamini kwamba CCM ni chama kitakachowaletea Watanzania ukombozi wa kweli wa kisiasa na kijamii. CCM niliyoiona Dodoma si tena kile chama nilichokulia na kilichonipa malezi ya maadili. Ni dhahiri kwamba CCM imepotoka na imepoteza dira na kupoteza mwelekeo na sifa za kuingoza nchi yetu.”
Kauli hizo mbili tofauti kuhusu chama kile kile zilitolewa na mtu mmoja ndani ya kipindi cha mwezi mmoja. Hilo lilitosha kuwapa shaka baadhi ya watu juu ya nini hasa mgombea huyo anasimamia.
Hata alipofanya mahojiano na Shirika la Utangazaji BBC, kuhusu suala la kuwa na imani na CCM na kutokuwa na imani na chama hicho ndani ya muda mfupi na kwamba kama angeteuliwa na CCM kugombea urais asingekisema chama hicho, alishindwa kutoa maelezo yenye ushawishi.
“Hiyo maana ilikuwa kwamba alikuja kwetu kutaka tu urais, hakujali na kuhangaika tunasimamia nini, alichokuwa anataka ni urais kwa njia yoyote ile, ingekuwa vigumu sana kumpambanua kama mwana mabadiliko halisi na anasimamia kile ambacho Chadema tulikuwa tunaamini,” anasema mjumbe mmoja wa viongozi wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam.
Tangu kutajwa kwa Orodha ya Fedheha (List of Shame), vita dhidi ya ufisadi umekuwa ndiyo utambulisho (si itikadi) wa Chadema, miongoni mwa waliokuwa kwenye orodha hiyo, ni Edward Lowassa, na Chadema wakitumia nguvu kubwa kumshambulia kuliko wengine 10 waliobaki kwenye orodha hiyo.
Kumpokea Lowassa kwenye chama na mara moja kumpa nafasi ya kubeba bendera ya chama hicho katika mbio za kuwania urais, ulikuwa ni uamuzi mgumu, ambao uliwafanya wengi washangilie lakini pia ukiwashitua wengi sawia.
Kwa uamuzi huo Chadema kilijiweka katika mazingira ya kutoeleweka na baadhi ya wafuasi wake makini, kwa kuwa chama hicho kilitumia zaidi ya miaka mitano kuwaaminisha wananchi kuwa Lowassa ni fisadi lakini kikatumia chini ya wiki moja kumpokea Lowassa kwenye chama na kumpa heshima ya kugomba urais na kumsafisha, huku Mwenyekiti Mbowe akieleza kwamba hawakuwa tayari kuendelea kuwa na jeuri wakati hakuna ushahidi wa wazi dhidi ya Lowassa.
Alisema Mbowe katika hotuba ya kumkaribisha Lowassa kujiunga na Chadema, na kwa maana hiyo, kujiunga na Ukawa: “Chama hiki si Mahakama. Hatuwezi kuwa chama cha kuhukumu bila ushahidi…Siwezi kula matapishi, nazungumza with confidence (kwa kujiamini). Hatuwezi kufikiri mambo mema mapya kama tutadumu kwenye kufikiri mambo mabaya ya zamani. Sisemi Lowassa ni mtakatifu.
Wala wana CCM au wana Chadema ninaowaongoza ni watakatifu. Nani mmoja wetu ambaye ni mtakatifu? Aliye mtakatifu nchi hii zaidi ya Mungu achukue mawe amrushie mwenye dhambi.
“Hatuwezi kuendelea kuwa na pride (fahari) eti kwa sababu zamani tulimtaja Lowassa kuwa fisadi. Hatuwezi kubadili misingi kama pamekosekana ushahidi wa wazi.”
Hotuba hiyo ya Mbowe ilikuwa na tafsiri kadhaa. Walau mbili kati ya hizo zinaweza kutajwa: kwanza ilizua shaka katika nyoyo za waliokuwa wakiamini katika Chadema.
Kwamba Mwenyekiti huyo huyo na maofisa wake waliokuwa wakisisitiza, kwa miaka mingi, kwamba wanao ushahidi wa ufisadi wa Lowassa, kubadilika ghafla kwa msimamo kulimaanisha kwamba chama hicho kimekosa sababu za kuaminiwa, na kwa maana hiyo wananchi hawakuwa na sababu kumuamini Mwenyekiti Mbowe hata kwa haya aliyokuwa anayasema wakati wa kumpokea Lowassa.
Pili, hotuba hiyo ilipeleka ujumbe kwamba Chadema hakina msimamo wala itikadi inayokiongoza.
Kilijieleza kwamba kinaweza kufanya chochote kile bila kujali mwanzoni kilisimamia nini ili mradi kukidhi mahitaji ya wakati uliopo. Ghafla kilioekana kuwa ni chama kipya, ni tofauti na kile ambacho wengi walikijua na kukikubali.
Mabadiliko Lowassa,
Lowassa mabadiliko
Suala jingine ambalo linaweza kuwa limegharimu juhudi za Chadema na Ukawa katika safari ya Ikulu ni hatua ya kumfanya mgombea huyo kuwa ndiye mabadiliko yenyewe.
Ukiondoa salamu ambazo zilizinduliwa na Mwenyekiti Mbowe, zilizokuwa zikiwataka wafuasi wake kuviringisha mikono kama ishara ya mabadiliko huku wakisalimiana kwa salam za Lowassa Mabadiliko, Mabadiliko Lowassa, dalili nyingine zote ziliashiria kwamba mgombea huyo alikuwa ndiyo mabadiliko.
Baada ya kuhamia Chadema, maelezo na hata sababu za Lowassa za kwanini anataka kuwa rais zilikuwa zile zile kama alipokuwa CCM, na kwa nguvu aliyoingia nayo, aliweza kumeza falsafa na hoja ambazo muungano wa Ukawa na chama kimoja kimoja vilikuwa vinasimamia.
Hoja kama ya kupambana na ufisadi, kuwashtaki au kuwafilisi mafisadi ambao toka mfumo wa vyama vingi urejewe wamekuwa wakipigiwa kelele, zilikoma kusikika kutoka kwa wapinzani.
“Watu makini kidogo walishituka na kuona kama hana jipya. Alichofanya ni kubadili njia tu ya kumfikisha Ikulu, lakini yeye anabaki kuwa yule yule aliyekuwa CCM. Alichofaulu ni kuwabadilisha wao badala ya wapinzani kumbadilisha yeye. Kuweka matumaini ya mabadiliko kwake ilikuwa ni ahadi yenye shaka, Ukawa walipaswa kuliona hili mapema,” anasema kiongozi mmoja wa Chama cha Wananchi (CUF), aliyetaka asitajwe gazetini.
Athari za Dk. Slaa na Profesa Lipumba
Ni kweli kwamba viongozi wa Chadema na CUF na baadhi ya wafuasi wao, walipuuza kuondoka kwa vigogo wa kweli wa Upinzani: Dk. Wilbroad Slaa na Profesa Ibrahim Lipumba. Waliwapuuza Dk. Slaa na Profesa Lipumba lakini wakashindwa kuzuia madhara ya kuondoka kwao.
Dk. Slaa, kwa miaka yote, alisimama kama alama ya harakati za Chadema kujipambanua kama chama kinachopinga ufisadi na alama alama ya mapambano dhidi ya ufisadi.
Historia yake akiwa mbunge wa Karatu kati ya mwaka 1995 mpaka 2010 na jinsi alivyoibana serikali kwenye masuala mbalimbali yaliyowagusa wananchi, ilimfanya awe kipenzi cha wananchi wanyonge hata alipoteuliwa kugombea urais mwaka 2010 haikushangaza alipoweza kupata asilimia 26.34 katika uchaguzi huo.
Alipojitoa kwenye chama hicho na baadaye kujitokeza hadharani kuweka bayana msimamo wake kwamba hawezi kugeuka nguzo ya chumvi kwa kumuunga mkono mtu kwa sababu tu ya kutaka kuindoa CCM madarakani bila misingi ya mabadiliko hayo, aliongeza majeraha kwa Chadema.
Kwa Chadema kukubali kumpoteza Katibu Mkuu wake dakika za mwisho kuelekea Uchaguzi Mkuu, na kumpokea mtu ambaye ukiondoa jina la chama na majina ya viongozi wake hakuwa anajua chochote kuhusu mipango na mikakati ya chama, lilikuwa ni kosa jingine la kiufundi.
Katibu Mkuu ni mtendaji mkuu wa chama, na kwa Dk. Slaa alishiriki kuunda mfumo wa uongozi wa chama hicho na kusimamia utendaji na utekelezaji wa majukumu ya chama kwa muda mrefu. Chama kisingeweza kumtosa kisha kisilipie gharama na hasara ya uamuzi huo.
Propaganda za kumdhalilisha kwa mambo yake binafsi na familia, zilifanikiwa kumfanya aonekane kwa baadhi ya watu kuwa ni mroho wa madaraka, lakini hizo zisingeweza kuondoa ombwe la kukosekana mtendaji mkuu katika chama katika wakati nyeti wa uchaguzi.
Aidha, propaganda hizo zisingeweza kuondoa ukweli wa hoja zake kwamba hoja na agenda ya siku zote ya chama hicho ilikuwa si kuindoa CCM madarakani kwa malengo ya kuindoa tu, isipokuwa kuleta mfumo mbadala wa utawala uliojengwa juu ya misingi na kanuni zitakazowezesha kutatua matatizo yanayowakabili wananchi.
Kwa Profesa Lipumba, pamoja na kugombea urais mara nne na mara zote kupoteza kwa CCM, bado alikuwa ni nguzo muhimu kwa CUF. Kama kilivyofanya Chadema, CUF nacho kilifanya kosa la kiufundi kukubali kiongozi ambaye tangu mfumo wa vyama vingi urejee amekuwa ndiyo kiongozi pekee mwenye wafuasi wengi wa kumuunga mkono, ukiondoa Maalim Seif Hamad, ambaye hana ushawishi Bara.
Kuingia kwa Sumaye na wengine
Katika mambo ambayo Chadema walikuwa wanajivunia, ilikuwa ni kuchukua baadhi ya vigogo wa CCM walijounga nao. Mmoja wa vigogo hao ni waziri mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, aliyeshika nafasi hiyo kwa miaka 10 mfululizo akiwashinda wenzake wa sasa na zamani.
Wachambuzi wa mambo hata hivyo wanasema, ushawishi wa Sumaye ulikuwa mdogo ndani ya chama kama ambavyo mwenyewe alivyosema kwamba ndani ya CCM alionekana kama sisimizi na hakuwa na maana yoyote na hivyo ndiyo sababu aliamua kujiunga na upinzani.
Miaka 10 ya uwaziri mkuu wake, ndicho kipindi ambacho kililalamikiwa sana kwa kuwa na ubinafsishaji wa ovyo ukiwemo wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), uliolalamikiwa na hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, achilia mbali mauzo ya nyumba za umma.
Sumaye asingekuwa kuwa mtu sahihi wa kunadi ujumbe wa mabadiliko dhidi ya CCM kwa vile madudu ya CCM ni madudu yake pia kwa nafasi aliyokuwanayo.
Lakini Sumaye naye alionyesha tabia ya kigeugeu wa hali ya juu. Muda mfupi kabla ya CCM kuamua mgombea wake, alitahadharisha kwamba akipitishwa mgombea ambaye ana kashfa za matumizi mabaya ya fedha kusaka urais asingekubali.
Kauli hiyo ilitafsiriwa kuwa alikuwa anamsema Lowassa ambaye inafahamika kwamba hakuwa anaiva vizuri naye.
Kukubali kuungana na Lowassa, ambaye alitishia kumkimbia wakiwa wote CCM, kuliwafanya baadhi ya watu kutilia shaka ushirikiano wa mawaziri wakuu hao wastaafu.
Chadema kumezwa
Ujio wa Lowassa, ulikuja na kitu kingine ambacho hata kama viongozi wa Chadema walikuwa hawakioni, kilikuwa na atahri zake. Katika baadhi ya maeneo wakati wa kampeni jukwaa la Chadema lilikuwa likionekana kama la CCM.
Unapokuwa na jukwaa la kampeni ya Upinzani ambalo mbele wapo Lowassa mwenyewe, Sumaye, mzee Kigunge Ngombale Mwiru, Khamis Mgeja na Mgana Msindai na wakawa wanahubiri mabadiliko, unahitaji kuwa na moyo mgumu sana kuwaamini.
Palihitajika ushawishi maalumu kuwafanya wazee hao wa CCM waaminike kwamba ni wanamabadiliko halisi na si watu walio na hasira za kushindwa.
Baregu: Tuna mashaka
Akizungumza na Raia Mwema, Mratibu wa Kampeni wa vyama vinavyounda Ukawa, Prof. Mwesiga Baregu, amesema kuna dalili za mchezo mbaya katika kujumlisha matokeo kwa sababu kura zinazosomwa haziwiani na hamasa na wingi wa watu waliokuwa wanahudhuria kwenye mikutano ya mgombe wao.
“Mpaka mwisho wa kampeni kulikuwa na ‘homa ya Lowassa’ (hamasa zaidi na Lowassa) lakini kwenye kura haionekani, kuna dalili za mchezo mbaya. Hata kama wote walikuwa wanapata watu wengi, kwanini wingi huu unaonekana upande mmoja?” alihoji Prof. Baregu.
Aliongeza kwamba wanasubiri kuona Tume itahitimisha vipi zoezi lake la kutangaza, wakitoa matokeo amabyo hayatawiana na waliyo nayo, watazumgumza.
“Tume ieleze kuna majimbo tumepata mbunge, diwani na kwingine tumechukua halmashauri, inakuwaje kura za rais zinakuwa chini kuliko hata za mbunge?”- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/lowassa-kaonewa#sthash.s1Z7ENnG.dpuf
No comments :
Post a Comment