Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, November 10, 2015

Lowassa ni fumbo la siasa Tanzania


ZAIDI ya Watanzania milioni sita takriban asilimia 40 ya waliopiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, walimchagua Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, awe rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Idadi ya waliompigia kura huenda ikawa ni zaidi kama madai ya kuibiwa kura wakati wa hesabu yaliyotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya Ukawa ni sahihi.

Kwa mujibu wa Chadema na washirika wao wa Ukawa, hesabu zao zinaonesha kuwa mgombea wao, Lowassa, alishinda kwa kura asilimia 60 au zaidi.

Watanzania wengi tulitaka mageuzi makubwa baada ya kuona kuna mambo mengi hayaendi sawa hapa nchini. Katika hamu yetu ya kupata mabadiliko viongozi wetu wa mabadiliko wakatuletea Lowassa kutoka CCM aongoze vuguvugu hilo lililoratibiwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Edward Lowassa alipokuwa CCM, siku chache zilizopita kabla ya kuhamia upinzani, aliimba sifa za chama hicho tawala na viongozi wake, akasifu hadi ukomo wa kusifu! Kisha katika mchakato wa kinyang’anyiro cha tiketi ya kugombea urais ndani ya CCM, Kamati Kuu ya chama chake, iliyokua ikichuja wagombea ikakata jina lake.
Ni wazi Lowassa hakupendezewa. Hapo ndipo Ukawa kwa busara zao wakaona hiyo ni fursa, wakamfuata na kumshawishi kuhama CCM na akafanya hivyo.

Kuanzia hapo Lowassa akaanza kuzungumza lugha tofauti kabisa. Lowassa mpya akaanza kuinanga CCM, chama ambacho siku chache zilizopita alikuwamo huko kama mmoja wa wanachama waandamizi akikitetea kwa nguvu zake zote. CCM ikawa mbaya na haifai.

Inawezekana chama kikabadilika na kuwa kibaya muda wowote. Kwa mantiki hiyo, ingewezekana kuwa CCM ilianza kuwa mbaya mwaka huu na hususan siku ile mara baada ya Lowassa kukatwa. Yeye na wastaafu wenzake, Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye na kada mkongwe wa zamani wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru ni kwamba CCM ilikuwa mbaya miaka na miaka!

Wazee hao walisema katika majukwaa ya kampeni kuwa, ukichukua rekodi yake tangu uhuru, CCM imeshindwa na haijafanya maendeleo na kwa sasa imekata pumzi.

Kwa maoni yangu walichosema wazee wetu hawa ni sahihi kabisa. Ni kweli CCM ni mbaya sana na viongozi wa chama hicho wameipurura nchi yetu kwa uongozi wao mbaya. Hali zetu zingeweza kuwa bora zaidi kama uongozi uliotokana na chama tawala CCM ungekuwa bora.

Hata hivyo, sio kauli tuliyoitegemea kutoka kwa Lowassa, Sumaye na Kingunge kwa sababu mbili kuu. Kwanza, maneno hayo ya kuikashifu CCM yanawaweka pamoja katika kundi la wanasiasa ndumilakuwili, vigeugeu, waliokosa kauli thabiti na msimamo, waongo na wanafiki. Sababu ya pili inayowanyima Lowassa na wenzake haki ya kusema CCM imekuwa mbaya miaka yote na haijafanya kitu tangu uhuru ni ukweli kuwa wao wenyewe wamekuwa sehemu ya ubaya na uovu huo wa CCM.

Halafu, kwa mfano, Lowassa asingekatwa CCM wangehama? Na uovu huo ungekuwa umesameheka kwa kuwa nao wamo?

Ningeelewa sana mwanasiasa akitoka CUF kwenda Chadema au kinyume chake. Lakini mwanasiasa mwandamizi kama Lowassa anapotoka CCM kwenda upinzani kugombea urais, na mara tunamuona ghafla kaanza kuwa muumini wa serikali tatu, katiba ya wananchi na hata kuanza kujua kuwa CCM wanaiba kura!? - haiingii akilini hata kidogo.

Tafsiri yangu ya kitendo cha Lowassa kuhamia upinzani na kuanza kuisema vibaya CCM na kubeba ajenda za Ukawa ni kwamba alikuwa anafanya maigizo. Maneno ya Lowassa hayakuwa yakitoka moyoni, na bahati mbaya aliyasema akijisahaulisha kuwa wao wenyewe ni sehemu ya historia ya uozo huo wa CCM wa miaka nenda rudi! Pia, tafsiri yangu nyingine ni kuwa Lowassa ni mwanasiasa mwepesi ambaye hana misingi anayoiamini na anayumba kama bendera inayofuata upepo au yupo tayari kubadili misimamo yake kirahisi ili tu aingie ikulu.

Nakumbuka katika moja ya hotuba za Rais wa kwanza nchini, Julius Nyerere wakati akitaja sifa za kiongozi bora alisema tutakayemchagua kuongoza nchi yetu awe mtu ambaye tukiulizwa, je huyu anaweza kufanya yake ambayo tunamtarajia kuyafanya, majibu yetu yasitoke mdomoni tu, bali moyoni kuwa huyo anaweza.

Je, ninyi ndugu zangu milioni sita, asilimia 40 ya wapiga kura, nini kiliwashawishi kuamini kuwa Lowassa anayebadilika kama kinyonga, angeweza kuwa rais bora?

Kwa hiyo, kwangu mimi, achilia mbali Lowassa kuhusishwa na ufisadi, na vile vile licha kudaiwa kuwa ana maradhi na ameshindwa kuwasilisha na kufafanua vema sera na mipango yake, hili la ugeugeu lilitosha kuwasaidia Watanzania kufanya uamuzi wa kumkataa Lowassa. Lakini kwa Watanzania wengi, hiyo haikuwa sababu iliyotosha kumkataa.

Watanzania tunafuata mfumo wa siasa za demokrasia, ambapo tunakuwa na uchaguzi unaoshindanisha vyama na kutupatia fursa sisi wananchi kuamua nani atuongoze. Hivyo basi, waliompa kura Lowassa, kama wale waliompa John Magufuli wa CCM, walikuwa na haki ya kufanya hivyo.

Lakini katika demokrasia tunatakiwa tufanye uamuzi wa busara unaotokana na ufahamu na taarifa tulizonazo. Na vile vile, licha ya kuwa demokrasia inatoa fursa kuchagua, kuna mijadala ambayo kama raia tunaiendesha ili kupanuana mawazo.

Najua, tulifanya mijadala ya aina hii wakati wa kampeni, lakini kwa mambo ambayo baadhi yetu hatukuyaelewa kipindi kile, si vibaya kuyarejea na kuyatathmini. Moja ya mambo hayo ni fumbo la Lowassa, mgombea ambaye si tu alivutia nyomi lakini alivuna kura ambazo zilitishia CCM saa za mwanzo matokeo ya kura yalipoanza kumiminika.

Binafsi, nilikuwa na sababu kumi na zaidi za kumkataa Lowassa. Lakini la ugeugeu na kukosa misimamo ni la msingi sana. Bora mtu awe na msimamo usio sahihi kuliko kuyumba hovyo katika misimamo na kujaribu kubadilika kwa tamaa ya maslahi binafsi kabisa.

Kura alizopata Lowassa, iwe asilimia 40 au zaidi kama aliibiwa kura, ni nyingi. Ni kura nyingi kuliko kura zilizompatia ushindi Kikwete mwaka 2010.

Haijapata kutokea mgombea wa upinzani kuzoa kura kiasi hiki. Lakini, kwamba aliyepata kura hizi ni Lowassa, aliyetajwa kuwa na udhaifu mwingi, ni jambo ambalo Mungu ninamuomba na nitaendelea kumuomba anipe ufunuo kulielewa.

Je ni ile hali ya wengi wetu kukata tamaa kwa hiyo tunakamata chochote kinachotupa matumaini kujiokoa? Au tulitaka kuikomoa CCM tu?

- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/lowassa-ni-fumbo-la-siasa-tanzania#sthash.G59VsphQ.dpuf

No comments :

Post a Comment