Juzi polisi ilitegua bomu la kienyeji lililotegwa eneo la Mkunazini, jana bomu lingine liliteguliwa eneo la Maskani ya Cuf Michenzani
Juzi polisi ilitegua bomu la kienyeji lililotegwa eneo la Mkunazini na jana bomu lingine liliteguliwa eneo la Maskani ya Cuf Michenzani.
Watu watatu wanashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mabomu hayo yaliteguliwa na askari wa JWTZ na hakuna mtu aliyejeruhiwa.
Kamanda Mkadam alisema walipokea taarifa za kuonekana kitu kisicho cha kawaida katika eneo hilo jana, maarufu kama Commonwealth Masikani na kuanza kufanya uchunguzi wake.
Alisema bomu hilo lilikuwa limetengenezwa kwa kutumia kopo lililokuwa limefungwa simu ya nokia ya tochi na juu likiwa limeshikiliwa na kamba ya mpira na nyanya.
“Katika eneo la tukio pamekutwa mabaki ya vipande vya nondo, misumari ya nchi nne, mabaki ya kopo lenye kuonekana kama la oil ya engine lililohifadhi mlipuko na mabaki ya vipande vya simu ya nokia bado eneo hilo linalindwa kwa uchunguzi zaidi,” alisema.
Hata hivyo, aliwataka wananchi kuwa watulivu na kuendelea na shughuli zao kwani polisi inaendelea kuwasaka watu wanaofanya vitendo hivyo.
Alisema tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu, watu 38 wanashikiliwa na polisi kutokana na tuhuma za kuhusika na vitendo vya uvunjifu wa amani visiwani hapa.
Alisema kati ya waliokamatwa wengine walikuwa katika harakati za kulinda kura kutoka mita 200.
Wakati huo huo, Kamanda Mukadam alisema polisi imepiga marufuku mikusanyiko au maandamano katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar.
Uamuzi huo alitangaza jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuenea tetesi za kufanyika maandamano ya kupinga kufutwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Alisema Jeshi la Polisi halitambui uwepo wa maandamano yoyote na limejipanga kuwachukulia hatua za kisheria watu ambao wataonekana kuhatarisha amani na umoja wa kitaifa visiwani humo.
“Tumesikia tu tetesi mitaani kuwa vijana wanajiandaa kufanya maandamano siku ya Jumatatu (kesho), lakini tutahakikisha kuwa hakutakuwa na maandamano,” alisema.
Alisema Jeshi la Polisi litaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ili kuhakikisha amani ya nchi inaendelea kudumu visiwani humo.
Hali hiyo imeanza kujitokeza baada ya mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad, kutangaza kuwa ameamua kurejesha ajenda ya kupinga kufutwa matokeo ya uchaguzi mkuu kwa wananchi wadai haki yao ya kidemokrasia kwa njia ya amani baada ya juhudi zake za kutafuta ufumbuzi kukwama.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment