Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Thursday, November 5, 2015

Mizigo ya JK kwa Magufuli hii hapa.

Dk. John Pombe Magufuli.
Imebainika kuwa Rais wa awamu ya tano anayetarajiwa kuapishwa leo, Dk. John Pombe Magufuli, atakuwa na mzigo mzito wa kushughulikia ahadi na mambo kadhaa mazito yanayoachwa na mtangulizi wake, Rais Jakaya Kikwete.
 
Magufuli alishinda kwa zaidi ya asilimia 58 katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 na leo ataapishwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, katika siku maalum iliyotangazwa kuwa ya mapumziko kitaifa ili kutoa fursa kwa kila Mtanzania kushuhudia.
 
Hata hivyo, wakati mamilioni ya Watanzania wakitarajiwa kufuatilia tukio hilo la kuingia madarakani kwa rais mpya kwa nia ya kuanza kushuhudia ‘mabadiliko ya kweli’ aliyoahidi Magufuli wakati wa kampeni, bado kuna mambo mazito anayoachiwa na Rais Kikwete, na ambayo baadhi ya wafuatiliaji wa siasa za Tanzania wanayaelezea kuwa ni ‘mizigo’ mizito kwake.
 
Baadhi ya mambo hayo yanatajwa kuwa ni mgogoro ulioibuliwa upya wa hali ya kisiasa visiwani Zanzibar; katiba mpya na pia utekelezaji wa baadhi ya maazimio ya bunge kuhusiana na kashfa ya ulaji wa mabilioni ya fedha za akaunti ya Tegeta Escrow. 
 
Kadhalika,  wafuatiliaji wa siasa za Tanzania wanataja mzigo mwingine mzito unaoachwa na Rais Kikwete kwa Rais mpya, Dk. Magufuli, ni utekelezaji wa ahadi kadhaa kubwa zilizowahi kutolewa tangu wakati wa kampeni na Rais Kikwete anayemaliza muda wake leo.
 
MGOGORO ZANZIBAR

Huu ni unatajwa kuwa ni ‘mzigo’ mzito zaidi unaoachwa na Rais Kikwete bila kupatiwa ufumbuzi wa kina. Hapo kabla, Rais Kikwete alimwagiwa sifa nyingi kwa kuwezesha maridhiano yaliyifanikisha uanzishwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani Zanzibar, ambayo inahusisha mseto wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).Hata hivyo, amani na utulivu uliodumu kwa takriban miaka mitano sasa iliingia doa wiki iliyopita baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kutangaza ghafla kuwa amefuta uchaguzi mkuu visiwani humo ambao mgombea wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, alisema anaelekea kushinda kwa asilimia 52.87 kutokana na karatasi za matokeo walizokusanya kutoka kwenye vituo vya uchaguzi. 
 
Wakati akitangaza kuufuta uchaguzi huo ambao matokeo yake ya urais wa Jamhuri ya Muungano yalijumuishwa katika hesabu zilizomuingiza Magufuli madarakani, Jecha alidai uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki. Hata hivyo, waangalizi wote wa kitaifa na kimataifa wameelezea mshituko wao kuhusiana na uamuzi huo na kutaka kura ziendelee kujumuishwa na mshindi halali atangazwe. 
 
Hadi sasa, mgogoro huo bado haujapata suluhu na hivyo katika hali isiyotarajiwa, Dk. Magufuli anaapishwa leo huku hatma ya uchaguzi wa Zanzibar ikiwa bado gizani.
 
KATIBA MPYA

Huu ni mzigo mwingine mzito anaoachiwa Dk. Magufuli. Jitihada za Rais Kikwete kufanikisha jambo hili ziligonga mwamba baada ya mchakato wake kukwama kabla hata wananchi kupigia kura katiba inayopendekezwa. Inakumbukwa kuwa miongoni mwa sababu zilizotibua mchakato wa katiba mpya ni mgawanyiko uliojitokeza katika Bunge Maalum la Katiba kati ya wafuasi wa chama tawala (CCM) na wale wa upinzani. Serikali ya Magufuli ina kazi kubwa kufufua mchakato huo kwa maslahi ya taifa.
 
MAAZIMIO YA BUNGE AKAUNTI YA ESCROW

Licha ya Rais Kikwete kutekeleza maazimio kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwatimua baadhi ya mawaziri wake waliotajwa kuhusika katika kashfa ya Escrow, bado kuna maazimio mengine hayajatekjelezwa hadi sasa na hivyo Dk. Magufuli atakuwa na kazi ya ziada kumalizia ‘kiporo’ hiki. Baadhi ya maazimio ya Bunge ambayo yaonekana kuwa bado hayajatekelezwa kwa dhati ni Serikali kuandaa na kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria iliyounda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi, na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa Taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo.
 
Pia Serikali ilitakiwa kupitia mikataba mibovu ya kuzalisha umeme kati ya Tanesco na kampuni binafsi ya kufua umeme, hivyo basi Serikali imetakiwa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti.
 
Hata hivyo, inaelezwa kuwa hadi sasa kuna mmoja wa watuhumiwa bado angali akilipwa mabilioni ya fedha kila mwezi licha ya Bunge kuazimia vinginevyo. Ni wazi kuwa Dk. Magufuli atakuwa na kibarua kizito cha kushughulia suala hili kwa mujibu wa maazimio ya Bunge.
  
AHADI MELI, RELI MPYA, FLYOVERS 

Mzigo mwingine mzito anaouacha Rais Kikwete kwa Dk. Magufuli ni utekelezaji wa ahadi kadhaa nzito, zikiwamo za ununuzi wa meli tatu mpya kwa ajili ya maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.
 
Kadhalika, serikali ya Dk. Magufuli itakuwa na kazi kubwa ya kutekeleza ahadi ya kukamilisha miradi ya ujenzi wa flyovers katika makutano ya barabara kubwa mijini kama Mandela/Nyerere katika eneo la Tazara na Morogoro na Ubungo jijini Dar es Salaam. Ipo pia kazi kubwa ya kutekeleza ahadi ya ujenzi wa reli mpya kwa kiwango cha ‘standard gauge’,  ununuzi wa bajaji maalum za kubebea wagonjwa katika hospitali na pia kumalizwa tatizo la maji katika maeneo kadhaa nchini. 
 
Kadhalika, ipo pia ahadi ya Rais Kikwete ya kuiendeleza Kigoma kiasi cha kuwa na hadhi ya kuitwa ‘Dubai ya Afrika’. 
 
Ahadi hii ni kwa maana  ya kuwa mkoa wa kibiashara kama ilivyo Dubai kwa kujenga uwanja wa ndege, kupanua bandari na kuimarisha reli ili kuhudumia nchi za maziwa makuu na za kusini mwa Afrika.
 
MAFANIKIO SERIKALI YA JK 

Mzigo mwingine wa serikali ya Rais Dk. Magufuli ni kufikia au kuyapiku mafanikio kadhaa yaliyoletwa na Rais Kikwete. 
 
Licha ya changamoto zilizopo, serikali ya awamu ya nne imefanikiwa katika maeneo kadhaa yaliyotokana na ahadi zilizotolewa wakati wa chaguzi zilizopita, hivyo kumpa kibarua cha ziada Rais Magufuli katika kuhakikisha kuwa serikali yake inaongeza juhudi ili idumishe mafanikio hayo.
 
Baadhi ya maeneo ya mafanikio ni ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, ujenzi wa mtandao mkubwa wa barabara za lami na pia ujenzi wa madaraja makubwa kama la Mto Malagarasi. 
 
Mafanikio mengine ni kuwapo kwa shule nyingi zaidi za sekondari nchini, kushamiri kwa vyuo vikuu na kuongezeka kwa ufanisi katika sekta ya Bandari ni miongoni mwa maeneo ya mafanikio. 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment