AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, November 30, 2015

DARUBINI YA MTATIRO :Nchi hii haikuwa na kiongozi miaka 10 iliyopita?



Julius Mtatiro, Mwananchi.
Tangu
 Rais Pombe Magufuli alihutubie na kulizindua Bunge la Kumi na Moja Ijumaa Novemba 20, mambo kadhaa yamewashangaza wafuatiliaji wa masuala hapa nchini.
Mshangao mkubwa ulikuwa ni kwa namna Rais huyu mpya alivyokuwa anafafanua na kueleza uozo ulioko serikalini kama vile nchi haikuwahi kuwa na kiongozi kwa miaka mingi iliyopita.
Ni kama vile Tanzania ilikuwa ni kisiwa cha kuponda raha kuanzia Ikulu hadi kitongojini kwa mjumbe wa Serikali ya kitongoji, kijiji na mtaa. Yaani unaweza kustaajabu iweje nchi iendeshwe kwa udhaifu mkubwa namna hiyo na vyombo vyote muhimu vya dola vipo.
Sote tunafahamu kuwa hii ni nchi ambayo hata twiga na wanyama hai wengine husafirishwa kwa ndege kwenda nje ya nchi kinyume na sheria ya nchi yetu. Hii ni nchi ambayo wauzaji wakubwa wa dawa za kulevya wanaharibu maisha ya vijana wetu huku wanachekewa na kukaribishwa kwenye hafla kubwa za kuchangia hiki au kile.
Hii ni nchi ambayo kijana anaingia kufanya kazi serikalini akiwa hohehahe na baada ya mwaka mmoja anakuwa tajiri akimiliki ghorofa ya mamia ya mamilioni, magari matatu ya kifahari na mpiga matembezi kwenye hoteli kubwa za kitajiri hapa nchini.
Hii ni nchi ambayo mtoto wa kigogo ndiye anafanya kazi katika sekta nyeti za Serikali lakini kubwa kuliko yote hii ni nchi ambayo mkurugenzi wa shirika au kampuni fulani ya umma au binafsi akiwa anatoka kabila fulani basi asilimia 70 ya wafanyakazi wa shirika, kampuni au ofisi hiyo watakuwa wanatoka kwenye kabila hilo, tunayo mifano mingi ya aibu.
Haya yote yameendelea na nchi ikiwa na uongozi na wizara lukuki, ina polisi, ina Takukuru, mashirika makubwa ya kitaalamu ya kudhibiti ubora wa viwango vya bidhaa lakini asilimia 50 ya bidhaa tunazotumia ni feki na zinadhuru afya za Watanzania.
Serikali imekuwapo hata mwaka jana wakati fedha zinaibiwa Akaunti ya Escrow.
Safishasafisha ambayo imeanzishwa na Magufuli ni vita kubwa kushinda tunavyodhani, si vita rahisi kwani wanaosafishwa wanaweza kubadilisha mbinu za wizi wao ili wajinufaishe zaidi bila kubainika na ikifika hapo mtu mmoja hataweza vita hii.
Hii ni vita ya Taifa ambayo kila mtu anapaswa kuiunga mkono bila kujali anatoka chama gani, dini gani na ana masilahi gani katika nchi, ikiwa wezi na mafisadi wanakamatwa na kushtakiwa ni jambo la heri kwa Taifa letu na ni ajenda muhimu iliyo kipaumbele cha Watanzania.
Kwa sasa, lazima hatua zichukuliwe ili tofauti ya maisha ya matajiri na maskini ipungue.
Mbunge wa lililokuwa jimbo la Ubungo (aliyemaliza muda wake na sasa Mbunge wa Kibamba), John Mnyika, aliwahi kusisitiza kuwa Taifa letu linaangamia na moja ya sababu ni kuwa na rais dhaifu.
Lakini Mnyika alisisitiza uwepo wa uzembe mkubwa kwa Bunge na akatupa lawama za kutosha kwa chama kinachoongoza dola.
Nadhani baada ya hatua mbili tatu alizozichukua Magufuli mtu yeyote anaweza kujiuliza, hivi kabla ya Magufuli, Tanzania ilikuwa na Rais aliyekuwa muwajibikaji?
Iweje nchi ilikuwa na Rais na mawaziri na idara zote na watendaji halafu wezi na matajiri wabaya wanakwepa kulipa kodi ya makontena 300? Kwamba taifa linaibiwa Sh80 bilioni huku Serikali yote ipo, “Eni wei” ni kama pia walivyoiba yale mabilioni ya EPA na mengine mengi tu, nadhani serikali ilikuwapo na haikuchukua hatua zozote na ni Serikali ya chama kilekile ambayo ipo hadi leo.
Hakika, Serikali ilikuwa dhaifu ikiacha mambo mengi yakivurugika na pengine kwa kuzilinganisha na nyingine zilizopita, pengine hii imeongoza.
Ni aibu ya karne kuona kuwa ujinga wa kupindukia unatokea katika nchi, fedha za walipakodi zinaliwa na huku maisha ya wananchi wengine yakiharibika kwa kukosa huduma muhimu za kijamii na kiuchumi kwa sababu tu ya genge la wezi katika nchi.
Ni nani alikuwa anawalinda wezi hawa hata Ikulu yenye tochi ya moto isiwaone? Ni nani alikuwa analinda wezi hawa hata dola yenye mkono mrefu isiwakamate? Ni nani alikuwa analinda wezi hawa hadi wanaharibu uchumi kiasi hiki? Je, huyu tunamhukumu vipi?
Madudu haya yote yalipokuwa yanafanyika chama kinachoongoza dola kilikuwa usingizi upi? Kwa sababu baadhi ya waharibifu wakubwa wa uchumi wa nchi hii ni marafiki wakubwa wa chama dola, ni wafadhili wakubwa wa chama hicho na huenda viongozi wa chama hicho hula na kunywa nao meza moja. Hawa wanafanywaje? Wako wapi?
Madudu yote ambayo yametokea hapa nchini yalitokea huku kukiwa hakuna viongozi? Kama walikuwapo waliokuwa wanaongoza wanachukuliwa hatua gani? Kama tuko kwenye nchi ambayo jinai haifi na Rais ameahidi sheria ni msumeno na inakata kotekote, hebu na iwakate viongozi wote waliokuwa wanasimamia wizi huu. Hili panga liwe refu “bring them all to justice” ili mbele ya safari madudu ya namna hii yasitokee tena kuharibu maisha ya wananchi wetu.
Tukutane Jumapili ijayo kwa darubini nyingine.
(Julius Mtatiro ni mchambuzi wa masuala ya Kijamii na Kisiasa (Adv Cert in Ling, B.A, M.A, L LB) +255787536759, juliusmtatiro@yahoo.com).

No comments :

Post a Comment