Samia Suluhu Hassan, mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Historia imeandikwa. Samia Suluhu Hassan ndiye mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Samia anakuwa msaidizi mkuu wa Dk John Magufuli aliyeapishwa juzi kuwa Rais wa Tanzania baada ya kuibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini Oktoba 25 mwaka huu.
Ushindi huo umepokelewa kwa shangwe na wananchi hasa wanawake.
Mratibu wa Kituo cha Usuluhishi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Gladness Munuo amesema amefurahishwa na ushindi wa Dk Magufuli ambao unamfanya aliyekuwa mgombea mwenza wake, Samia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi huo wa tano kufanyika nchini kwa kuvishirikisha vyama vingi vya siasa moja kwa moja kuwa makamu wa Rais.
Munuo anasema anaamini kwamba uongozi wake utakuwa na mafanikio kwa sababu Samia atashirikiana na Dk Magufuli bega kwa bega kuwaleta Watanzania maendeleo.
“Yale mambo yaliyokuwa yakisuasua sasa yatakaa sawa, yakiwamo ya kijinsia hasa tukizingatia kuwa Makamu wa Rais ni mwanamke. Samia naye anasifika kwa uwezo wake wa utendaji.
“Tuwape miaka mitano ya kutathmini utendaji wao. Binafsi naamini kwamba amepata nafasi hii kwa mpango wa Mungu, atazingatia, hatatuangusha wanawake wenzake,” anasema.
Mratibu wa Taifa wa Umoja wa Wanawake Wanasiasa Tanzania (Ulingo), Dk Ave Maria Semakafu, anasema anaamini wanawake wengi wamefurahishwa na ushindi wa Dk Magufuli kwa kuwa umewawezesha pia, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi kuwa na Makamu wa Rais mwanamke.
“Tumefungua ukurasa mpya kwani baada ya miaka 20 ya tamko la Mkutano wa Wanawake Duniani wa mwaka 1995 Beijing nchini China, tumekuwa na mrejesho mzuri kuhusu mwitikio wa Serikali kuweka ushiriki sawa wa nafasi za uongozi.
“Badala ya kuwafanya wanawake wawe watu wa kupiga kura kwa kuchagua viongozi wa ngazi mbalimbali sasa nao wanachaguliwa, wanaaminika na kupewa nafasi kubwa ya uongozi kama hii,” anasema.
Dk Semakafu anasema pamoja na ushindani wa kisiasa kuwa mkali wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, wanawake wawili waligombea nafasi za juu, akiwamo Anna Mghwira aliyegombea urais kupitia ACT-Wazalendo.“Nilikuwa nafuatilia kampeni zao, kulikuwa na mwitikio mkubwa wa watu waliokuwa wakiwasikiliza,” anasema.
Majukumu
Samia, ambaye wakati wa kampeni alifika takriban katika kila jimbo nchini kuomba kura kwa ajili ya mgombea urais Dk Magufuli, alikuwa akisoma na kufafanua sera na ahadi zilizomo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mgombea mwenza huyo aliwapa matumaini makubwa wananchi waamini kuwa mabadiliko ya kweli yataletwa na wagombea hao wa CCM na siyo kutoka vyama vya upinzani.
Kampeni zimekwisha, kilichobaki ni kazi tu. Samia sasa ana jukumu la kuhakikisha anafanikisha ahadi alizotoa kwa wananchi hasa wanawake. Kote alikokuwa akipita alikuwa akisisitiza kuwa yeye akiwa mama, yapo masuala kadhaa ambayo yanamgusa moja kwa moja, hivyo ameamua kuyapa uzito wa pekee wa kuyashughulikia mara atakapokuwa Makamu wa Rais.
Nilibahatika kuwa katika msafara wa kampeni wa mwanamama huyu, ambaye aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba. Katika maeneo kadhaa alikopita alikuwa akiahidi mambo mawili makubwa;
Kwanza, kuboresha huduma ya afya hasa kwa mama na mtoto; pili, kushughulikia tatizo la maji ambalo linawatesa wanawake wengi hasa waishio vijijini.
Alipokuwa katika Kijiji cha Kibirashi, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, alishtushwa kuona foleni kubwa ya madumu na ndoo tupu zilizopangwa kwenye mabomba ya maji jirani na uwanja aliokuwa akifanyia mkutano wa kampeni.
Katika foleni hiyo, walikuwamo wanaume na wanawake baadhi yao walikuwa na baskeli, pikipiki na punda. Wanawake walikuwa wengi zaidi huku wengine wakiwa wamebeba watoto.
Mandhari yale yalielezea ukubwa wa shida ya maji. Samia aliwahutubia wananchi hao na kukiri kwamba kero ya maji ni changamoto atakayokabiliana nayo, hivyo aliwaomba wananchi wamchague Dk Magufuli awe rais ili yeye apate nafasi ya Makamu wa Rais na aweze ‘kujitwisha’ jukumu la kushughulikia kero hiyo na kuboresha afya ya mama na mtoto.
“Mimi ni mama, najua umuhimu wa maji, pia wanawake ndiyo watafutaji wakubwa wa maji na wanatembea umbali mrefu kuyatafuta, nawaombeni nijitwishe hilo jukumu la kuwatoa kwenye mateso hayo, pamoja na lile la uzazi kwani kuna wajawazito waliokufa kwa sababu ya huduma duni za afya, umbali wa vituo vya afya na wodi zisizo na vifaa muhimu vya kujifungulia, nawaahidi nitashughulikia hayo,” anasema Samia.
Baadhi ya wananchi waliozungumza kwa nyakati tofauti wanasema uhaba wa maji ni tatizo kubwa katika eneo hilo na kwamba kwa baadhi ya maeneo, limesababisha ugomvi miongoni mwa wanavijiji, lakini wana imani siku moja Serikali itawakumbuka na kuwapatia maji ya uhakika.
“Hilo bomba linafunguliwa kwa wiki mara mbili kuanzia saa nane mchana, lakini maji hayatoki ya kutosha, hivyo licha ya kuweka foleni si ajabu ukayakosa, hapo utalazimika kwenda kuchota kwenye kisima ambacho maji yake yana chumvi kali, huwezi hata kupikia ugali na ukipikia maharagwe hayaivi,” anasema Mariam Bakari.
Amina Saadundu anaeleza kuwa kukosekana kwa maji ya kutosha katika eneo hilo kumesababisha chuki na ubaguzi miongoni kwa jamii, kiasi kwamba wanashindwa kula vyakula kwenye sherehe au misiba kwa hofu kwamba maji yaliyotumika ni machafu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibirashi, Mohammed Chambo, anasema kero hiyo imekuwapo tangu mvua zilipoharibu miundombinu ya maji iliyokuwa imeunganishwa kutoka kwenye chanzo cha maji.
“Maji haya ni ya mradi maalumu tulioletewa na Serikali miaka kadhaa iliyopita. Mradi huu unahusisha vijiji vitatu ambavyo ni Kibirashi, Gombero na Kwamaligwa, tunapeana zamu ya kufungua mabomba yaliyounganishwa kwenye kila kijiji,” anasema.
Mwenyekiti huyo anasema wamewasiliana na ofisi ya mhandisi wa maji wa wilaya hiyo yenye jukumu la kusimamia mradi huo na kuwashauri kufungua akaunti maalumu ya kuweka fedha kwa ajili ya mradi.
Kilio cha wakazi wa Kilindi ni sehemu ya vilio vya wananchi wengi katika maeneo mengi nchini aliyofanya mikutano Samia, ukiwamo wa Jimbo la Gairo ambako mbunge mteule wa CCM, Ahmed Shabiby, aliwasilisha suala hilo kwa sura tofauti.
“Naomba unisaidie, sipendi haya maneno ya kuitwa mwizi eti nimekula fedha za mradi wa maji, ukiingia Ikulu uipe kipaumbele Gairo hasa huo mradi wa maji ili walioniita mwizi waumbuke maana hawajui wasemacho,” anasema Shabiby.
Anadai kuwa wabaya wake wanasema ‘ametafuna’ mamilioni ya fedha za mradi wa maji ambao ulikuwa unasimamiwa na Benki ya Dunia (WB).
Mradi huo uliokadiriwa kukamilika kwa gharama ya Sh6.6 bilioni ulianza mwaka 2007, lakini maji yaliyopatikana yana chumvi kali, hivyo wananchi wanatafuta mashine maalum ya kuondoa chumvi ili yaweze kufaa kwa matumizi ya binadamu.
No comments :
Post a Comment