NA EDITOR
30th November 2015.
Kutokana na hukumu hiyo iliyotolewa wiki iliyopita, endapo mwekezaji huyo atakamilisha taratibu za kulitwaa eneo hilo, wananchi na watoto wao waliokuwa wakitumia ufukwe huo kwa ajili ya kujiburudisha hawatakuwa na fursa hiyo tena, vinginevyo watalazimika kulipa kiingilio kitakachowekwa na mwekezaji huyo. Tunaomba na kuisihi serikali iingilie kati suala hilo na kuhakikisha kuwa eneo la Coco Beach linabakia kuwa eneo la wazi kwa ajili ya umma wa Watanzania.
Kampuni ya Q Consult ilifungua kesi hiyo kupinga kitendo cha Manispaa ya Kinondoni kusitisha mkataba wa kumiliki na kuendesha ufukwe huo. Hata hivyo, manispaa iliamua kuvunja mkataba ule kutokana na mwekezaji kushindwa kukamilisha masharti yaliyowekwa.
Tunapenda kueleza masikitiko yetu kwa kitendo cha ufukwe wa Cocoa kumilikishwa na mtu mmoja wakati inajulikana kwa miaka mingi ni eneo la wazi kwa ajili ya wananchi wote kujiburudisha. Kitendo cha kumilikishwa kwa ufukwe wa Cocoa kwa mtu binafsi ni mfululizo wa vitendo vilivyokithiri kwa maeneo ya wazi na hasa katika jiji la Dar es Salaam kunyakuliwa na watu binafsi. Kinachoshangaza wengi ni kuwa jiji la Dar es Salaam kwa sasa halina sehemu ya wazi kwa ajili ya watu kupumzika baada ya shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa.
Suala hili la eneo la Cocoa Beach sio la kufumbiwa macho kwani linapaswa kupingwa kwa namna yoyote ile, kwani sehemu hiyo ndiyo kati ya maeneo machache yaliyobakia kwa ajili ya watu kupumzika.
Pia watu wenye kipato cha chini na kile kikubwa pia walikuwa wanatumia eneo hilo kujiburudisha hasa wakati wa sikukuu mbalimbali. Sasa baada ya kuchukuliwa na mwekezaji ina maana sasa watu watapaswa kuanza kulipia kiingilio kwa ajili ya kupumzika kwenye eneo la ufukwe wa bahari.
Hata hivyo, bahati nzuri suala hilo limekuja kipindi ambacho serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, ambayo imejipambanua katika kuinua maisha ya Watanzania bila ya kuwabagua bila shaka itafuatilia suala hili kutokana na ukweli kuwa sio jambo la busara kwa mfanyabiashara mmoja kumilikishwa eneo la wazi ambalo limekuwa likinufaisha maelfu ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Sehemu nyingi za fukwe zimepewa watu binafsi kwa mfano eneo la Mbezi Beach ambako walalahoi hawawezi kugusa kutokana na kuwapo kiingilio cha gharama kubwa.
Miji mbalimbali maarufu duniani ina sehemu za kupumzikia watu wake bila kujali matabaka baada ya kazi ngumu za binafsi au zile za ujenzi wa taifa.
Mathalani, katika Jiji la Nairobi, nchini Kenya kuna bustani maarufu ya Uhuru Park, ambako watu huweza kukutana hapo na kupumzika na kupanga mikakati mbalimbali.
Pia katika Jiji la London, Uingereza kuna Hyde Park, Paris, Ufaransa (Jardin de Tuileries), Johannesburg, Afrika Kusini (Nelson Mandela Square) na New York, Marekani (Flushing Meadow Park). Ni jambo la kushangaza kuona kuwa kuna watendaji katika Jiji la Dar es Salaam hawafikirii kuhusu kuwapo kwa maeneo ya watu kupumzikia na badala yake kuwazia kipato kutoka kwa wafanyabiashara wenye tamaa ya kumiliki maeneo ya umma na kuwaacha wananchi wa kawaida wakiwa hawana hata sehemu ya kupumzika.
Tunaomba serikali iiingilie kati suala hili ili kuhakikisha kuwa eneo la Cocoa Beach linabakia mikononi mwa umma na sio mtu mmoja.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment