Wagombea wa nafasi ya urais Zanzibar wameondolewa ulinzi siku moja baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa visiwa hivyo.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa, wagombea 12 waliokuwa wakiwania nafasi hiyo wameondolewa ulinzi wa askari kanzu (polisi) waliokuwa wakiwalinda tangu walipoteuliwa na Zec kuwa wagombea.
Wagombea walionyang’anywa ulinzi ni Khamis Iddi Lila (ACT-Wazalendo), Juma Ali Khatib (Tadea), Hamad Rashid Mohammed (ADC), Soud Said Soud (AFP), Ali Khatib Ali (CCK), Mohammed Masoud Rashid (Chaumma) na Tabu Mussa Juma (Demokrasia Makini).
Wengine ni Abdallah Kombo Khamis (Demokratic Party), Kassim Bakari Ali (Jahazi Asilia), Seif Ali Iddi (NRA), Issa Mohammed Zonga (Sau) na Hafidh Hassan Suleiman (TLP).
Wagombea waliobakia na ulinzi kutokana na nyadhifa zao ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad.
Mgombea wa urais wa Jahazi Asilia, Kassim Bakar Ali alisema haikuwa muafaka kwa wagombea wa urais kuondolewa ulinzi wakati uchaguzi bado haujakamilika na mshindi kupatikana.“Sisi bado ni wagombea na hatujapokea barua yoyote ya kufutwa kugombea kwetu, tunachosubiri uchaguzi ukamilike inakuaje tuondolewe ulinzi?” Alihoji mgombea huyo.
Alisema tangu matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar yafutwe, wagombea wote wamebakia njiapanda hawafahamu kinachoendelea kutokana na Tume ya Uchaguzi kukaa kimya.
“Huwezi kuwaondolea wagombea ulinzi kabla ya fainali ya mchezo haijamalizika, sisi ni wagombea na kama itatokea mmoja wetu kuhujumiwa na kupoteza maisha uchaguzi utalazimika kuahirishwa,” alisema mgombea Juma Ali Khatib wa Tadea.
Alisema mlinzi aliyepewa alimuaga ghafla kuwa hawatakuwa pamoja anarudi kuendelea na shughuli nyingine kazini baada ya matokeo ya uchaguzi kufutwa.
Alisema Zec inapaswa kukaa pamoja na wagombea wote kuwaeleza nini kinachoendelea badala ya kukaa kimya kwa zaidi ya wiki moja sasa bila ya kutoa taarifa yoyote tangu kufutwa kwa matokeo hayo.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame, alithibitisha wagombea hao kuondolewa ulinzi baada ya tume kufuta matokeo ya uchaguzi Zanzibar Oktoba 28, mwaka huu.
Alisema ulinzi huo utarejeshwa baada ya Tume ya Uchaguzi kutoa utaratibu na ratiba ya uchaguzi wa marudio.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment