Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimeanza kuwaandaa wanachama wake na uchaguzi wa marudio baada ya Tume ya Uchaguzi visiwani humo (Zec) kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Akizungumza na wanachama wa CCM mkoa wa Magharibi, Mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo, Yussuf Mohammed, aliwataka wanachama hao kushiriki uchaguzi wa marejeo.
“Msione ajabu kushiri uchaguzi wa marejeo CCM itashinda kwa kishindo kikubwa ni kujipanga na kujiandaa vizuri kushiriki uchaguzi huo, tume ikisema kesho uchaguzi unarejewa sisi ni kwenda kupiga kura tu,” alisema.
Akizungumza na wanachama wa CCM tawi la Kiembesamaki, alisema CCM mkoa wa Magharibi inaunga mkono tamko la serikali lililotolewa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi kuwa wananchi watulie na wasubiri uchaguzi wa marejeo ili kwenda kupiga kura.
Aliwataka wana-CCM kuwa makini na kupuuza propaganda kuwa CCM inafanya njama ili kushinda uchaguzi huo.
Alidai kuna maandalizi yanayofanywa na vyama vya upinzani kusambaza vipeperushi ambavyo vinasomeka kuwa Dk. Ali Mohammed Shein ameridhia Maalim Seif Sharif Hamad (Cuf) atangazwe kuwa mshindi wa urais wa Zanzibar wakati uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 ulikuwa na udanganyifu mkubwa.
“Niwaombe wana-CCM vipeperushi hivyo karibu vitasambazwa mitaani lakini ukishakipata kisome halafu kichome moto wala usihadaike,” alisema.
Mohammed alitoa wito kwa wananchi wakiwamo wana-CCM kuwa watulivu na kudumisha amani na kutokubali kushawishiwa kuivuruga amani iliyopo.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment