NA MHARIRI
8th November 2015.
Kilichowashangaza wengi ni kuwa Rais Magufuli alifika kwenye wizara hiyo kwa kutembea kwa miguu kutoka katika ofisi yake iliyoko Magogoni, Ikulu hadi wizarani hapo.
Rais alipoingia ndani ya moja ya ofisi za wizara hiyo, alikuta watumishi zaidi ya sita hawapo, jambo ambalo ilibidi amhoji mmoja wa watumishi waliokuwepo kwamba "Hawa ambao hawapo wamekwenda kunywa chai?".
Rais Magufuli aliendelea hadi Hazina ambako alitoa maagizo ya namna ya kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima, akasisitiza pia waongeze ukusanyaji wa mapato ya serikali ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku kuwalipa posho wabunge nje ya malipo wanayolipwa na Bunge.
Ziara hiyo ya ghafla ilimwezesha Rais kutoa maagizo kwa watendaji wa Wizara ya Fedha kuhakikisha kuwa wanavunja haraka mtandao wa wakwepa kodi, na kwamba wizara itoe maelekezo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili ikusanye kodi halali za serikali kwa mujibu wa sheria.
Kwa nia ya kudhibiti mianya ya wakwepa kodi, Rais Magufuli alisisitiza kuwa katika serikali anayoiongoza, hakuna mkubwa yeyote atakayeruhusiwa kutoa 'ki-memo' kwa TRA kwa lengo la kusamehe ulipaji kodi halali za serikali.
Ni dhahiri kuwa Rais Magufuli anakerwa na uzembe unaoweza kujitokeza katika ukusanyaji kodi halali za serikali, anaweka mikakati ya makusudi ili mapato ya serikali yaweze kudhibitiwa kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Tunaamini kuwa ziara ya ghafla aliyoifanya Rais Magufuli, inatoa funzo kubwa la kuwa na nidhamu na kufuata sheria mahali pa kazi kwa watumishi.
Ni dhahiri kuwa baadhi ya watumishi, hutumia muda mwingi wa saa za kazi kwa shughuli zao binafsi, na ndio maana Rais alipouliza wafanyakazi wengine waliko, hakupata jibu kutokana na kila mmoja kuamua kufanya lolote atakalo kinyume cha taratibu.
Tunaamini kuwa dhamira ya Rais Magufuli ni njema, anataka kuonyesha kuwa kaulimbiu ya 'Hapa Ni Kazi' haikuwa kwa ajili ya kampeni za kutafuta kura, alikuwa anakusudi la dhati la kufanya kazi kwa malengo ya kupata mabadiliko ya maendeleo.
Ziara hiyo ya ghafla ni fundisho kwa maeneo mengine ya wizara, taasisi pamoja na maeneo yote ya kazi nchini ili yaweze kuthamini muda wa kazi pamoja na utekelezaji wake.
Rais alijua kuwa atabaini watumishi wengine kutokuwepo maeneo ya kazi, alijua hilo kutokana na uzoefu wake katika utumishi alioshuhudia mwenyewe akiwa katika wizara mbalimbali, ingawa sasa anataka yawepo mabadiliko ya kuwajibika ipasavyo.
Tunaamini Rais Magufuli anaguswa na ahadi alizozitoa wakati wa kampeni, ahadi ambazo nyingi zinahitaji gharama kubwa kuzitekeleza, na ndio maana ameisisitiza Wizara ya Fedha ikishirikiana na TRA kuhakikisha kuwa mapato ya serikali yanakusanywa na kodi zote halali zinalipwa bila kigugumizi.
Ni ukweli usiopingika kuwa nidhamu kazini ni mhimili wa mafanikio yenye tija, uzembe hupunguza kasi ya uzalishaji, nidhamu ya kazi ni pamoja na kuwepo maeneo ya kazi na kutekeleza majukumu muhimu.
Tunatakiwa kubadilika katika utendaji, na kinachotakiwa zaidi ni kujenga nidhamu ya kazi ili matokeo ya kazi tuifanyayo yatafsiriwe kwa hatua ya maendeleo yatakayotokea, na hayo ndiyo mabadiliko ya kweli.
Ni imani yetu kuwa kila mwananchi atatimiza wajibu wake ipasavyo katika kipindi hiki ambacho tunataka kufanya mabadiliko katika nyanja mbalimbali za maisha yetu, kazi iwe kama dira yetu itakayotuongoza kufikia mabadiliko ya kweli.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment