BAADHI ya wachambuzi na wanasiasa wamempongeza Rais, Dk. John Magufuli kwa kuteua baraza la mawaziri kwa kuwa na idadi ndogo, huku wakitoa kasoro mbalimbali.
Akizungumza na MTANZANIA baada ya kutangazwa kwa baraza hilo jana, Mtaalamu wa Uchumi ambaye pia alipata kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alikosoa uteuzi wa baraza hilo, ingawa alipongeza kuwapo kwa idadi ndogo ya mawaziri.
Profesa Lipumba alishangaa kitendo cha Rais Magufuli kumrudisha Profesa Sospeter Muhongo katika Wizara ya Nishati na Madini, wakati aliwahi kujiuzulu kwa kashfa ya Escrow.
“Watanzania hawajasahau kashfa ya Tegeta Escrow ambayo mawaziri na vigogo mbalimbali wa serikali walijiuzulu. Sasa nimeshangazwa kuona tena Profesa Muhongo akirudishwa alijiuzulu kwa tuhuma hizo za Escrow,”alisema Profesa Lipumba.
Mtaalamu huyo wa uchumi alisema ni wazi kwamba ile dhamira ya Rais Magufuli ya kupambana na rushwa na ufisadi itakuwa imepata doa kubwa kwa kumrudisha mtu ambaye alijiuzulu kwa kashfa ya ufisadi.
“Hili linafedhehesha sana kwa sababu suala la Profesa Muhongo kutuhumiwa kwa Escrow halina ubishi maana katika maazimio ya Bunge mawaziri waliotuhumiwa walitakiwa kujiuzulu na wakafanya hivyo sasa iweje leo Rais Magufuli aturudishie…inaleta picha gani?,” alihoji.
Alisema kwa upande wa uwakilishi wa Zanzibar, kwa kawaida Wizara ya Mambo ya Nje, waziri wake anatokea bara na naibu Zanzibar lakini safari hii wote wametokea Tanzania Bara.
LISSU
Kwa upande wake Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alieleza kushangazwa kwa kitendo cha Rais Magufuli kurudisha majina ya mawaziri mzigo waliokuwa katika baraza lililopita la Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete.
“Nafikiri ameteua mawaziri kwa njia ya kushangaza sana, ni mwendelezo ule ule wa Kikwete. Mawaziri 13 kati ya 15 aliowateua ni wale wa JK, sasa yule rais wa hapa kazi tututamzamaje. Katika hili baraza lake sura mpya ni wawili tu sasa mtu kama Nape Nnauye huyu ana dili gani?
“Jingine lililonishangaza ni uteuzi wa Profesa Muhongo tulimfukuza bungeni kwa sababu ya kashfa ya Escrow, hii maana yake ni kwamba hajali Bunge lilisema nini na anawatukana wabunge na Watanzania…unamletaje mtu ambaye alihusika na kashfa hii?,” alihoji Lissu.
“Jingine lililonishangaza ni uteuzi wa Profesa Muhongo tulimfukuza bungeni kwa sababu ya kashfa ya Escrow, hii maana yake ni kwamba hajali Bunge lilisema nini na anawatukana wabunge na Watanzania…unamletaje mtu ambaye alihusika na kashfa hii?,” alihoji Lissu.
Lissu alisema kutokana na hilo, Bunge lijalo wataendeleza mjadala huo wa Escrow kwa kuwa hata mwaka haujaisha tangu Profesa Muhongo alipojiuzulu kwa kashfa hiyo kubwa.
Alisema tangu utawala wa Mwalimu Julius Nyerere hadi uongozi wa awamu ya nne, haijapata kutokea rais akakosa mtu wa kumteua kwenye baraza.
“Anatuambia ameshindwa kumpata mtu wa wizara fulani…Magufuli anatuambia kwamba wabunge wote wa CCM hajaona mtu anayefaa kuwa katika wizara ya ujenzi na maliasili,”alisema.
PROFESA MPANGALA
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala alisema Rais Magufuli ametimiza ahadi yake ya kuwa na baraza dogo kwa kuchanganya baadhi ya wizara pamoja ili kupunguza gharama za uendeshaji wa Serikali.
“Ametimiza ahadi yake kwa kuwa na wizara 18 ambazo ni chache ukilinganisha na serikali iliyopita, lakini ameonesha umakini katika uteuzi wa mawaziri wake kwani ametumia muda kuwatathimini na hadi sasa wizara nyeti kama vile Uchukuzi, Ujenzi na Miundombinu, Fedha na Mipango, Elimu, Sayansi na Ufundi na Wizara ya Utalii hajapata mawaziri, bado anaendelea kuwatafuta watakaomfaa,” alisema Mpangala.
PROFESA KITILA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitila Mkumbo, alisema yalikuwa matarajio ya wengi kwamba ataunda baraza dogo, lakini ameunda baraza la kawaida.
“Katika historia ya Taifa hili ni Rais Jakaya Kikwete tu ndiye alikuwa na baraza kubwa la mawaziri, lakini kabla yake yalikuwa mabaraza madogo na ndicho alichofanya Rais Magufuli,” alisema Mkumbo nakuongeza.
“Kwa kadiri nilivyosikia majina ya mawaziri ni baraza la kawaida kwa sababu lina mawaziri wa zamani…kikubwa tumpe rais na mawaziri wake muda tuwaombee heri wafanye kazi nzuri tusonge mbele,” alisema.
- BANA
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana alisema baraza dogo aliloliteua Rais Magufuli imeondoa utitiri wa wizara.
“Pia ameteua wazoefu, wasomi na kuna mchanganyiko wa vijana na wazee. Pia alivyomrudisha Profesa Muhongo wakati tunafikiria kuisuka upya Tanesco ni jambo jema,”alisema Dk. Bana.
KIBANDA
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), ambaye pia ni Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006), Absalom Kibanda alimpongeza Rais Magufuli kwa kumteua Nape Nnauye kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo.
“Nimepokea kwa furaha na matumaini makubwa ya kikazi, uteuzi wa Nape kuwa waziri mwenye dhamana ya habari. Namuhakikishia ushirikiano wa dhati wakati akitekeleza majukumu yake mapya,” alisema Kibanda.
WANANCHI
Baadhi ya wananchi waliozungumza na MTANZANIA baada ya Rais Dk. John Magufuli, kutangaza baraza hilo walisema wana imani kubwa na mawaziri na manaibu walioteuliwa.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) Mkoa wa Mwanza, Richard Rukambura, alisema ana imani kubwa na baraza hilo kwa kuwa limezingatia mahitaji ya Watanzania.
Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza, Mohamed Balla, alisema Rais Magufuli, amezingatia uwiano wa mikoa na ameteua mawaziri na manaibu wachapakazi na kuwataka wasimuangushe.
No comments :
Post a Comment