Wakati tarehe ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa marudio ikiendelea kubakia kitendawili Zanzibar, Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, kimesema kipo katika maandalizi mazito ya kushiriki na kushinda uchaguzi huo.
Msimamo huo umeleezwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai, alipokuwa akizungumza na Nipashe Makao Makuu ya chama hicho, Kisiwandui Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja jana.
“CCM tayari tumeanza kukaza buti katika kukamilisha maandalizi ya kushiriki uchaguzi wa marudio, imani yetu kubwa uchaguzi uwe huru na wa haki,” alisema Vuai.
Alisema maandalizi hayo yameanza kufanyika baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) kutangaza rasmi kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa awali na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali la Novemba 6, mwaka huu. Aidha, Vuai aliwataka wanachama wa CCM kupuuza taarifa zinazosambazwa na wapinzani wakidai hakuna uchaguzi wa marudio Zanzibar wakati wao tayari wameanza kujiandaa na uchaguzi wa marejeo.
“Nani kasema kuwa tumesema uchaguzi haupo, huyo anayesema hivyo aje na vielelezo vya ushahidi, sisi tunachojuwa uchaguzi upo na tutashiriki, tunaisubiri Tume ya Uchaguzi itangaze tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo,” alisema Vuai.
Alisema kuwa CCM inaendelea na matayarishio mazito ya kushiriki uchaguzi huo kwa Unguja na Pemba ili kuhakikisha malengo yake ya kuendelea kushika dola yanafanikiwa katika uchaguzi huo.
Hata hivyo, alisema wapo tayari kuingia katika uchaguzi kwa ukisimamiwa na tume yoyote, muhimu tu ni haki itendeke na uchaguzi uwe wa huru na wa haki.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment