Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, December 15, 2015

Dk Kigwangalla-Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto


Historia
Dk Hamis Andrea Kigwangalla ndiye Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika Serikali ya Awamu ya Tano, ameteuliwa katika baraza la mwanzo la mawaziri la Rais John Pombe Magufuli.
Hivi sasa Dk Kigwangalla ana umri wa miaka 40 na ifikapo mwezi Agosti mwaka 2016 atatimiza miaka 41, huyu ni kijana mbichi kabisa kwenye siasa za Tanzania. Baba mzazi wa Dk Kigwangalla anaitwa Mahampa Kigwangalla na amewahi kufanya kazi za kibenki na uandishi wa habari, lakini mama ya Kigwangalla yeye amekuwa mwalimu kabla hajajiunga na siasa za ndani ya vyama akipitia Chama cha Mapinduzi (CCM), huyu ni Bagaile Lumola.
Wazazi wa Kigwangalla wote wana asili ya mkoa wa Tabora na hata Kigwangalla mwenyewe katika sehemu ya maisha yake amekulia mkoani humo, lakini kwa uhakika wakati anazaliwa wazazi wake walikuwa mkoani Kigoma kwa ajili ya utumishi wa umma.

Elimu
Pamoja na kuzaliwa mkoani Kigoma (ambako wazazi walikuwa kikazi), Kigwangalla alifanikiwa kurejea mkoani Tabora na kutumia sehemu ya maisha yake ya utotoni katika wilaya za Uyui na Nzega na aliweza kuanza masomo na kuhitimu katika shule ya msingi Kitongo na Mwanzoli zote za wilayani Nzega kabla hajarejea tena mkoani Kigoma kuendelea na masomo ya sekondari katika shule ya Sekondari Kigoma kwa kidato cha kwanza hadi cha nne.
Baadaye alijiunga kidato cha tano na sita katika shule ya Sekondari Shinyanga (Shy Bush) katika mchepuo wa PCB (Fizikia, Kemia na Baiolojia), alifaulu kwa kupata daraja la kwanza na kuchaguliwa kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kubobea katika masomo ya udaktari wa binadamu katika Chuo cha Sayansi ya Tiba cha Muhimbili. “Kigwa” alihitimu shahada yake ya udaktari “Doctor of Medicine” (MD) mwaka 2004 na kama ilivyo ada akafanya mafunzo ya awali ya kazi (Internship) katika hospitali za Mwananyamala na Muhimbili.
Kigwangalla aliendelea na kiu yake ya “ubobezi” nchini Sweden katika Taasisi ya Teknolojia ya Blekinge na kuhitimu shahada ya umahiri ya biashara (MBA) akibobea kwenye “Oganaizesheni na Uongozi” na tena akiwa huko huko Sweden akajiunga katika Taasisi ya Karolinska ambako alihitimu shahada ya umahiri ya afya ya jamii (MPH) “Public Health”.
Dk Kigwangalla anatarajia kutunukiwa shahada ya uzamivu (PhD) katika Afya ya Jamii akiweka ubobezi kwenye Uchumi wa Afya, ameandika tasnifu yake kuhusiana na haki, usawa na uhalali wa mchakato wa bajeti kwenye sekta ya afya nchini Tanzania.

Uzoefu
Daktari Kigwangalla ana uzoefu wa utumishi na uongozi katika Afya, Biashara na Siasa. Kutokana na taaluma yake amewahi kufanya kazi kama Daktari daraja la II, Mtafiti na mtaalamu mshauri wa kujitegemea, amekuwa mkurugenzi wa makampuni binafsi yanayofanya kazi chini ya MSK Group na amewahi pia kuongoza makampuni haya (japokuwa si makampuni yenye mafanikio yanayofahamika).
Ndani ya CCM, “Kigwa” alijiunga mwaka 1994 kupitia mfumo wa Chipukizi na tokea hapo alijifunza uongozi wa chini wa chama, aliwahi kuwa kiongozi wa chipukizi Wilaya ya Nzega na kushiriki makambi mbalimbali ya vijana na halaiki, amewahi kuwa mwanachama wa kikundi cha “Green Guard” (kikundi cha ulinzi) cha CCM, amewahi kuwa Mwenyekiti wa Vijana wa CCM tawi la Kigoma Sekondari na Mjumbe, Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Sikonge akiwawakilisha vijana.
Pia Kigwangalla amekuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM, Mkoa wa Tabora, Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Nzega na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa.
Kigwangalla alianza harakati za ubunge jimboni Nzega mwaka 2010, ndani ya kura za maoni za CCM akashikilia nafasi ya tatu kwani wakati huo wana Nzega walimpigia kura nyingi kijana mwingine wa chama hicho, Hussein Bashe (Rafiki na mtu wa karibu sana na Edward Lowassa) na nafasi ya pili ikachukuliwa na mbunge aliyekuwa akimaliza muda wake, Lucas Selelii.
Kwa sababu ya mivutano ya kimakundi ndani ya CCM, Hussein Bashe aliundiwa “zengwe” juu ya shaka kwenye uraia wake, vikao vya juu vya CCM vikamtosa, vikamkwepa mshindi wa pili kwenye kura za maoni, vikaenda kwa mshindi wa tatu ambaye naye kama walivyo wenzake alikuwa na sifa za kutosha, “Kigwa”, huu ndiyo ukawa mwanzo wa nyota yake, akagombea ubunge wa Nzega na kushinda kwa tabu, akawaongoza wananchi wa Nzega kwa miaka mitano 2010 – 2015.
Akiwa ndani ya Bunge, Kigwangalla amekuwa mmoja kati ya wabunge vijana walioibeba CCM sana, lakini mara kadhaa alichukua misimamo ambayo ilimtofautisha sana na wana CCM wenzake. Amekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, lakini pia amekuwa mjumbe wa kamati zingine kadhaa.
Kigwangalla alitangaza nia yake ya kugombea urais kupitia CCM akiwa jijini Dar es Salaam katika hoteli ya Kilimanjaro “Hyatt Regency” Septemba 7, 2014 mbele ya vyombo vya habari na wageni maalumu walioalikwa na alieleza vipaumbele vyake chini ya kaulimbiu “Fikiri Tofauti, Amua Mabadiliko Sasa!”
Aliweka vipaumbele vyake kuwa ni utoaji wa huduma bora za kijamii (elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara na umeme), haja ya kuwa na bima za afya kwa Watanzania wote bila kujali vipato vyao na uwezo wao na udumishaji wa utawala bora. Hata hivyo chama hicho hakikumpendekeza katika michujo ya awali.
Baada ya kuenguliwa kwenye urais Kigwangalla alirejesha majeshi yake jimboni Nzega kugombea ubunge katika jimbo la Nzega Vijijini na kushinda huku lile la Mjini akimuachia Hussein Bashe baada ya kugawanywa. Ushindi huu umempa tiketi na sifa za kuteuliwa kuwa Naibu Waziri na Rais JPM.

Nguvu
Huyu ni mmoja wa naibu mawaziri vijana ambao wafahamu mahitaji ya jamii ya kisasa, elimu yake ya shahada tatu za chuo kikuu iliyojikita katika sayansi ya tiba, biashara na uongozi kwa upande mwingine ni silaha ambazo huenda mawaziri wengi hawana. Kigwangalla anazidi kujijengea ushawishi mkubwa katika siasa za Tanzania na huwezi kumlinganisha “Kigwa” wa sasa na yule aliyeshika nafasi ya tatu kwenye kura za maoni ya ubunge ndani ya CCM mwaka 2010. Akitumia vizuri vipaji vyake vya elimu atakuwa mmoja wa naibu mawaziri bora kabisa kwenye baraza la JPM.
Wakati nafanya uchambuzi juu ya wagombea urais wa CCM miezi kadhaa iliyopita (kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu) nilimuelezea Kigwangalla na dhana ya u-king’ang’anizi na nilisema “…viongozi ving’ang’anizi hufika mbali mara zote na huwa hawakati tamaa katika mipango yao hata wachekwe”. Dhana hii bado inampa nguvu kubwa Kigwangalla na huenda ikawa moja ya silaha ambazo zitamfanya ang’are katika wizara hii ngumu ambayo inahitaji watu makini na wafuatiliaji.
Kitendo cha kuwa mbobezi wa masuala ya sayansi ya tiba kisha kupewa uongozi wa wizara inayohusika na masuala ya tiba kina maana ya “kumpa samaki bahari ili aogelee”, samaki huyu ataogelea ipasavyo, kitaalam na kiweledi ikiwa ataamua kufanya hivyo, kama ni jipu naweza kusema limepata mtumbuaji sahihi. Wizara hii inahitaji mtu asiyeogopa, mbishi na ikiwezekana mkaidi mwenye busara ili awadhibiti “panya” wote wanaotafuna sekta ya afya na kuifanya iwe moja kati ya sekta zilizodorora kabisa nchini.
Kigwangalla ni mtu anayependa sana mijadala ya wazi, kwenye mitandao ya kijamii na kwingineko, hata alipojaribu kuchukua fomu ya urais ndani ya CCM ni yeye na Mwigulu Nchemba ndiyo walishiriki mjadala mmojawapo wa wagombea ulioandaliwa na taasisi za ndani ya nchi, anachopaswa kufanya hivi sasa ni kutumia zaidi utayari wa mijadala na weledi katika eneo hilo ili kuihuisha sekta ya afya kwa kutambua matatizo ya watendaji wa sekta hiyo, kujadiliana nao badala ya kupigana nao na kuyatatua. Hili ni jambo rahisi sana kwake kama atataka.

Udhaifu
Nilipofanya uchambuzi juu ya Kigwangalla miezi kadhaa iliyopita wakati anasaka urais ndani ya CCM nilieleza kuwa “…moja ya taswira za Kigwangalla na ambayo si salama kwake, ni majivuno. Kwa watu wanaomfahamu Kigwangalla, ni kijana anayejisikia sana na anadhani ni mwerevu kuliko watu wengine. Tulipokuwa katika Bunge Maalum la Katiba mara kadhaa wabunge wenzake wa CCM na hata kundi la 201 walisikika wakimsema na ukiwauliza wanakwambia kuwa ni mtu wa kujisikia.”
Nilipofanya uchambuzi ule Kigwangalla hakupendezwa na alinilaumu kwenye mitandao ya kijamii, tukafanya mijadala kadhaa na kulifunga suala lile, lakini dhana hii inabaki palepale. Na tukumbuke kuwa moja kati ya mambo yanayowaangusha viongozi wengi sana duniani ni “majivuno na kujisikia”, sijui Kigwangalla atakuwa amejirekebisha kiasi gani hadi sasa, lakini hili bado ni jambo hatari kwake.
Ikiwa ataendeleza kujikweza, kujidai anajua kuliko mtu yeyote n.k. atalipa gharama zake haraka sana. Kwa hatua ya sasa anapaswa kuwekeza nguvu kubwa na kujenga utulivu wa kutosha, madaraka aliyopata ni ya kawaida sana katika umri wake, kuna wenzake wengi waliyashikilia wakiwa na miaka 20 au 30, akiamua kwenda mbali kiuongozi atapaswa kujenga usikivu wa kutosha, kujifunza kuchukua hatua bila kufuata mkumbo au ushabiki na kuwashirikisha wengine katika hatua hizo.
Watu wa aina ya Kigwangalla ni rahisi sana kujisahau na kujitengenezea “one man show”, hili nadhani analitambua na atachukua hatua stahiki ili kujenga mustakabali mwema katika wizara yake na utendaji wake ambao utapaswa kuwa shirikishi na si wa mtu mmoja.
Alipokuwa mbunge Kigwangalla alikuwa akiwashambulia mawaziri wa CCM mara kadhaa, alijitofautisha na wabunge wa CCM ambao huwa ni “ndiyo mzee” kwenye kila kitu, jambo lile halikuwapendeza baadhi yao ndani ya CCM na leo hii baadhi yao ni wabunge na Kigwangalla ni Naibu Waziri, atakuwa na jukumu la moja kwa moja kufanya nao kazi kwa umakini na kujitambua kuwa yeye alikuwa mkosoaji mkubwa, watakapokuja kuikosoa wizara yake awasikilize zaidi na asiwe mwepesi kuwajibu “hovyo, kimamlaka na kuwashambulia” kwa dhana ile ya u-king’ang’anizi, aondoe uwezekano wote wa kutengeneza udhaifu wa aina hiyo ambao unaweza kumharibia kazi nzuri ambayo anatarajiwa kuifanya.

Matarajio
Matarajio ya Watanzania wengi ni kuona utendaji unabadilika kwa asilimia mia moja kwenye sekta ya afya, hili si jambo jepesi sana lakini linawezekana. Uzoefu wa Kigwangalla, elimu yake, juhudi zake na mwenendo wake kwa kiasi kikubwa vinaelemea kwenye upande wa mafanikio zaidi kuliko mapungufu kwenye sekta ya afya kwa ujumla wake.
Hapa namaanisha kuwa, kwa namna Kigwangalla alivyo na kwa wanaomfahamu, utundu wake, weledi wake, ubishi wake na sifa nyingine nyingi zinamfanya awe na uwezo mkubwa wa kusimamia mabadiliko ambayo yanahitajika kwa hali ya sasa, yaani “he is an opportunity” (yeye ni fursa tosha), na mtu unapokuwa fursa hupaswi kushangaa, unapaswa kuchapa kazi na kutumia weledi wako kwa misingi ya kuleta mabadiliko, baada ya muda mfupi watu wote watasema wizara fulani imepata mwarobaini.

Changamoto
Changamoto kubwa ambayo itamkabili Kigwangalla na ambayo lazima aitilie mkazo ni namna gani atafanya kazi na waziri ambaye siyo mweledi kwenye eneo wanaloliongoza, japokuwa ni ukweli kuwa kazi ya uwaziri ni uongozi tu na haihitaji ubobezi katika eneo husika, lakini ukweli wa kibinadamu unabakia kwamba unapokuwa na wizara ya afya ambayo waziri wake ni mwanasheria na naibu wake ni mtaalamu wa afya huenda huyu wa chini ambaye ndiye mbobezi wa fani hiyo anaweza kujisikia kama anajua sana kuliko yule wa juu yake, Kigwangalla akwepe kabisa mtego huu.
Sekta ya afya ya Tanzania ina matatizo makubwa sana, kuanzia wizi wa fedha za miradi ya afya, kutowajibika kwa madaktari, wakunga na wauguzi, malipo duni kwa watendaji wa sekta hii, changamoto za kiafya za watoto kama vile vifo vya watoto wachanga, huduma mbovu kwa kina mama wanaojifungua, utapiamlo, ukosekanaji wa dawa muhimu kwa wagonjwa kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali na nyingine lukuki, Kigwangalla anapaswa kuweka nguvu kubwa katika kumsaidia waziri wake kupambana na changamoto hizi, kuliko kujisahau na kujazwa maneno kuwa yeye “ana elimu kubwa, weledi ubobezi n.k.” kwenye afya kuliko waziri wake, mtego huu nasisitiza kwamba aukwepe ili usije kumwangusha. “If you are good, you are good!” (Kama wewe u mzuri katika jambo fulani, u mzuri tu), watu watakupima kwa uwezo wako na watasema wenyewe, “…ile wizara mtendaji ni fulani”.
Presha ya namna hii kwenda kwa Kigwangalla itafikishwa kwake na wenzake wengi ambao anajuana nao kwenye sekta ya afya kuliko ilivyo kwa waziri wake, hao nao asiwasikilize kwani wanaweza kumharibia mapema akajikuta hamsikilizi waziri wake kwa sababu yeye si mbobezi sana, napenda Kigwangalla awe kwenye baraza hili muda wote wa uongozi wa JPM kwa sababu uwezo wa “Kigwa” ni mkubwa, sitaki aanguke na ndiyo maana hana budi kuwa mtulivu sana, vita za kuusaka uwaziri kabla hujaonesha uwezo mkubwa na utulivu wa hali ya juu kwenye unaibu waziri si vita salama sana.

Hitimisho
Hakika, Hamis Kigwangalla “Kigwa au HK” ni moja kati ya Watanzania wenye bahati zao, alipoanza siasa za kitaifa alionekana kama mtu anayejaribu kazi ngumu sana, lakini miaka mitano ya umahiri mkubwa ndani ya bunge imemuivisha, sasa analijua bunge vizuri, anaijua vizuri Serikali na anazijua vizuri changamoto za Watanzania kwenye sekta ya Afya, kama sekta ya Afya ikikwama huku yeye ni Naibu Waziri basi huwenda tutakuwa tunahitaji watumishi kutoka mwezini. Namtakia kila la heri kijana huyu na atambue kuwa Watanzania wana matumaini makubwa sana na utendaji wake.

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ni mmoja kati ya vijana wenye uzoefu mkubwa na siasa za Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi (“Cert of Ling”), Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Umahiri (M.A) ya Usimamizi wa Umma na Shahada ya sheria (L LB); +255787536759, juliusmtatiro@yahoo.com, https://www.facebook.com/JuliusSundayMtatiro/, - Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi).

No comments :

Post a Comment