WAZIRI wa Ardhi Mhe William Lukuvi anaefananishwa na muandishi Ahmed Rajab kama ni Donald Trump wa Tanzania akitoa kauli ya kichochezi katika Kanisa la Methodist wakati wa kumsimika uaskofu, Askofu Mteule, Joseph Bundara, May, 2014.
RAIS John Magufuli ameitimiza ahadi yake kwa kuchagua baraza dogo la mawaziri likilinganishwa na lile lililofura la awamu ya nne. Anachotuonyesha ni kwamba mawaziri wachache wanaweza wakafanya kazi sawa au pengine zaidi ya ile iliyokuwa ikifanywa na mawaziri wasio na hesabu.
Kwa kupunguza idadi ya mawaziri Magufuli anakuwa anapunguza matumizi halali ya fedha za umma pamoja na ubadhirifu wa fedha hizo. Hawa mawaziri wanazitafuna fedha za umma bila ya huruma; wanalipwa mishahara minono, wanalipiwa nyumba, gharama za matibabu nchi za nje wanapokuwa wao au walio wao wagonjwa, wanalipiwa magari, mafuta ya magari, mishahara ya madereva, wanalipiwa ulinzi pamoja na marupurupu kemkem yanayoingia akilini na yasiyoingia akilini. Ilimradi wanaula.
La kusikitisha ni kwamba kuna baadhi yao ambao hawatosheki, hawakinai. Hawaridhiki mpaka waitumbukize mikono yao katika tope za ufisadi. Ndiyo maana kuna wenye kuziona siasa kuwa ni uwanja wa kula na huzivaasiasa wakiwa na tamaa hiyo ya kuweza kuchota fedha za umma na kujitajirisha.
Kwa sababu hiyo wanasiasa wa aina hiyo, hasa waliokwishauonja uwaziri, huwa hawayajali maslahi ya wananchi.Wanakuwa tayari kuzikiuka haki za binadamu, kuzipinda sheria na kufanya kila wawezalo kuyang’ang’ania madaraka.
Kwa hivyo, Magufuli alipotangaza baraza lake lenye mawaziri wasio wengi kama wale wa Jakaya Kikwete Watanzania, kwa jumla,walimshangilia na kumpongeza kwa kutimiza ahadi.
Hata hivyo, japokuwa nia yake ya kupunguza gharama za serikali ni ya kupigiwa mfano na ilimpatia sifa ndani na nje ya nchi, kuna wachunguzi waliokosoa uteuzi wa baadhi ya mawaziri wake.
Kwa ufupi, wachunguzi hao wanakubaliana kwamba sura ya baraza hilo haipendezi wala haisisimui. Ni wazi kwamba Magufuli aliwateua baadhi yao kulipa hisani. Hili, bila ya shaka, si geni katika siasa na ni jambo la kawaida.
Kwa hivyo, hatutokosea tukisema kwamba uteuzi wa akina Dk. Khamis Kingwalla (Naibu Waziri, Afya), January Makamba (Muungano na Mazingira chini ya Makamu wa Rais) na Nape Nnauye (Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo) ni kama malipo yao kwa kazi waliyoifanya wakati wa kampeni za uchaguzi wa urais.
Kazi yenyewe ilikuwa kumyanyasa Edward Lowassa, aliyekuwa mpinzani mkuu wa Magufuli katika uchaguzi huo akiwa mgombea wa Ukawa, muungano wa vyama vinne vya upinzani.
Mawaziri hao wametunukiwa nyadhifa hizo kuwa ni jaza yao kwa kazi waliyomfanyia Magufuli.
Uteuzi wa Nnauye, Katibu wa Uenezi na Itikadi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), haukuwa wa busara kwa wizara nyeti aliyopewa.Uteuzi huo umezusha hofu na wasiwasi miongoni mwa wadau wa tasnia ya habari. Hofu yenyewe ni kwamba kwa machachari yake Nnauye anaweza kuigeuza wizara ya habari iwe chombo cha kuendeshea propaganda za CCM, asiweze kutofautisha baina ya wizara ya serikali inayotakiwa iwatumikie wananchi wote bila ya upendeleo na kitengo cha propaganda cha CCM.
Hilo haliwezi kuwa jambo zito kwa kiongozi kama yeye aliyethubutu wakati wa kukaribia uchaguzi mkuu kusema kwamba chama chake lazima kishinde hata kama kwa “goli la mkono”.
Tanzania imepata sifa mbaya karibuni kwa namna waandishi wa habari na vyombo vya habari vinavyohujumiwa Bara na Zanzibar. Mfano wa karibuni ni mashambulizi yaliyofanywa usiku wa kuamkia Desemba 3 kwenye steshini ya Redio ya Hits FM kilicho Migombani, Unguja.
Inasemekana kwamba watu wapatao 15 waliojifunika nyuso zao waliingia kwa nguvu katika studio za steshini hiyo wakavunjavunja zana za utangazaji na kisha wakaichoma moto steshini hiyo. Hadi sasa Polisi hawajamkamata mtu na wanaendelea kusema kuwa hawajui ni nani wahalifu waliofanya mashambulizi hayo.
Wananchi mitaani, ingawaje, wanasema kwamba lau mashambulizi hayo yangekuwa yamefanywa na mahasimu wa CCM isingelipita saa kabla ya wahalifu hao kutiwa mbaroni.
Jambo lililojitokeza wazi pale mawaziri wa mwanzo wa baraza la mawaziri wa Magufuli walipotangazwa ni jinsi Zanzibar isivyowakilishwa kwa usawa katika baraza hilo la serikali ya Muungano. Miongoni mwa mawaziri wa mwanzo waliotangazwa ni wawili tu wenye asili ya Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Profesa Makame Mbarawa (Maji na Umwagiliaji).
Uteuzi wa Mbarawa unashangaza kwa vile wizara aliyopewa si ya Muungano na nusu ya wizara ya Mwinyi, yaani Jeshi la Kujenga Taifa, haihusiki na Muungano.
Zaidi ya hayo, Magufuli amewachafua Wazanzibarina hata baadhi ya Waislamu, Visiwani na Bara, kwa kumrejesha William Lukuvi kwenye baraza la mawaziri. Itakumbukwa kwamba mwaka jana Lukuvi alitamka maneno yaliyoonekana na wengi kuwa ni ya uchochezi wakati alipokuwa kanisaniwakati wa maadhimisho ya kutawazwa Askofu Joseph Bundala wa Kanisa la Methodist.
Alipokuwa akihutubu katika sherehe hizo Lukuvi alionya kwamba endapo wananchi wataukubali muundo wa Muungano wa serikali tatu basi jeshi litatawala nchi na Zanzibar itaukaribisha utawala wa Kiislamu na Waarabu.
Alipoyatapika matamashi hayo Lukuvi hakukaripiwa na wakubwa zake serikalini au katika chama chake. Wakati huo Lukuvi alikuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu na alimwakilisha katika sherehe hiyo Waziri Mkuu wa wakati huo Mizengo Pinda.
Hakuna mkubwa wake yeyote aliyemtaka aombe radhi wala yeye mwenyewe hakutanabahi kwamba alikuwa amesema maneno ya kijinga, yasiyo na msingi na ya uchochezi. Badala yake aliyakariri hayo matamshi yake, tena kwa kibri, katika Bunge la Katiba, licha ya kutakiwa atubu na Askofu Bundala.
Tunaweza kuumithilisha ujinga wa Lukuvi na ule wa Donald Trump, mwanasiasa wa Marekani anayetaka chama chake cha Republic kimchague awe mgombea wake wa urais katika uchaguzi wa urais wa Marekani 2016. Sawa na Trump aliyependekeza hivi karibuni kwamba Waislamu wote wasiruhusiwe kuingia Marekani, Lukuvi amethibitisha kwamba ana ulimi usio na nidhamu na kwamba ni mtu mwenye chuki za kikabila na kidini.
Tafsiri ya wachunguzi ni kwamba kwa kumteua mtu kama huyo awe waziri wake,alichofanya Magufulini kama kuwazaba kibao Wazanzibari na hata Waislamu walioshtushwa na kukerwa na matamshi ya Lukuvi.
Uteuzi mwingine uliowavunja moyo Wazanzibari ni ule wa January Makamba kupewa wadhifa wa kushughulikia mambo ya Muungano. Wanamuona kuwa ni kiongozi mwenye kibri, asiyeielewa historia ya Muungano nakwamba kuwekwa chini ya Makamu wa Rais aliye mmoja wa wahafidhina wa Zanzibar huenda kukazidi kuchafua mahusiano baina ya Serikali ya Muungano na Zanzibar.
Magufuli alikuwa hana hila ila amkubali Samia Suluhu awe mgombea mwenza wake kwa vile ndiye aliyebebeshwa na vigogo vya chama chao. Inajulikana kwa nini wenye kuamua mambo walimtaka Samia awe mgombea mwenza wa Magufuli.
Umakamu wa Rais ni tuzo aliyotunukiwa Samia kwa msimamo aliouchukua katika Bunge la Katiba kuhusu suala la Zanzibar na la rasimu ya pili ya Katiba iliyopendekezwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba. Jinsia yake, bila ya shaka, ilimsaidia akubalike kwa wengine miongoni mwa viongozi wa CCM, hususan kwa huko Zanzibar.
Inavyoonyesha hadi sasa ni kwamba wasaidizi wakuu wa Magufuli wa kuweza kumsaidia kuutanzua mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar si watu ambao watakuwa na moyo wa kwenda kinyume na shinikizo za wahafidhina wa CCM, wa Visiwani na Bara.
Ikiwa hali ya mambo itathibitika kuwa hivyo basi mustakbali wa Zanzibar hauelekei kuwa mwema. Na usipokuwa mwema na mgogoro uliopo wa kisiasa ukiendelea hivi ulivyo bila ya kupatikana ufumbuzi wa haraka basi Magufuli atajikuta katika hali ngumu katika mahusiano yake na wafadhili wa Tanzania.Hali hiyo itazidi kutatanika iwapo viongozi sampuli ya Lukuvi wasipodhibitiwa wasitoe matamshi yanayoweza kuwa ya uchochezi.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/%E2%80%9Cdonald-trump%E2%80%9D-wa-tanzania-haukuwa-uteuzi-wa-busara#sthash.Pe60SHZF.dpuf
No comments :
Post a Comment