MAJINA ya Wazanzibari wawili yamechomoza kama mojawapo ya watu wanaoweza kupewa nafasi ya kuongoza mojawapo ya wizara ambazo Rais John Magufuli ametangaza kwamba bado anatafuta mawaziri wa kuziongoza.
Wazanzibari hao; Khamis Mussa Omar na Profesa Idris Ahmada Rai, si wanasiasa lakini wamechomoza kama mojawapo ya wataalamu kutoka Visiwani humo wenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi.
Omar kwa sasa ndiye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi Zanzibar na Profesa Rai ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) ambacho kimeanza kujizolea umaarufu kama mojawapo ya vyuo vikuu vinavyokuja juu katika eneo la Afrika Mashariki.
Omar anayetajwa kama mmoja wa wachumi bora waliopo nchini kwa sasa jina lake linatajwa kama Waziri wa Fedha mtarajiwa huku Rai akitajwa kwenye Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
“Magufuli ameamua kufikiri nje ya boksi. Anatafuta taarifa mbalimbali kutoka kwa watu lakini hayo majina mawili yanaibuka mara kwa mara. Wote wawili ni Wazanzibari lakini wameonyesha uwezo mkubwa kwenye nyadhifa zao walizonazo sasa,” gazeti hili limeambiwa na moja ya vyanzo vyake vya kuaminika serikalini.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa SUZA, Profesa Rai alikuwa Mkuu wa Kitivo cha Teknolojia ya Mawasiliano katika Chuo Kikuu maarufu cha Makerere nchini Uganda.
Taarifa kutoka katika mitandao mbalimbali inaonyesha kwamba Rai alikiinua kitengo hicho kutoka kuwa kisichofahamika na kukifanya kuwa miongoni mwa vilivyo bora katika eneo la Afrika Mashariki.
Kwenye Chuo Kikuu cha Zanzibar, Rai amefanya maboresho mbalimbali ya kimuundo, kitaasisi na kitaaluma yaliyokifanya kiongeze idadi ya vitivo na wataalamu ndani ya muda mfupi.
Raia Mwema linafahamu kwamba wakati linakwenda mitamboni, zaidi ya wafanyakazi 50 wa SUZA walikuwa wanafadhiliwa na chuo hicho kwenye masomo ya juu ya ngazi ya shahada ya uzamili na uzamivu.
Kwenye wasifu wake ambao unapatikana mtandaoni, Profesa Rai anaeleza kuwa lengo lake ni kukifanya chuo hicho kiwe chaguo la kwanza miongoni mwa wanafunzi kutoka Afrika Mashariki katika kipindi cha miaka kumi ijayo.
Gazeti hili limeambiwa kwamba Rai anaweza kupewa Wizara ya Elimu kwa sababu ya uelewa wake wa sekta hiyo na ubunifu alionao pamoja na ukweli kwamba yeye pia ni mwanasayansi.
“Ukweli mwingine ambao Magufuli atakuwa ameambiwa ni kwamba SUZA sasa kina miradi inayotokana na fedha za wafadhili mbalimbali. Wafadhili hao wamekuja kutokana na mipango iliyoandaliwa na Rai na maana yake ni kwamba akipewa wizara ataleta ubunifu huo.
“Mojawapo ya matatizo ya elimu yetu katika miaka ya karibuni ni ukweli kwamba tumekosa kabisa ubunifu. Watu wanakuja kuwa mawaziri wakiwa hawana mawazo yoyote zaidi ya kuwa bora liende.
Mtu kama Rai anakuja na mtazamo mpya,” kilisema chanzo hicho. Omar, kwa upande wake, anatajwa kubebwa na uelewa wake wa uchumi mpana na masuala ya maendeleo na ingawa anafanya kazi zake Zanzibar, sifa zake zimefika mezani kwa Magufuli.
“Ukitaka kujua uhodari wa Omar kiuchumi hudhuria vikao vya bodi za kitaifa alizopo au kwenye mikutano. Anaujua uchumi ndani na nje na pia ni mzungumzaji mzuri. Wabunge na Watanzania watafaidi kumsikiliza na pia ni mtu thabiti na msafi,” kilisema chanzo hicho cha Raia Mwema.
Gazeti hili limeambiwa kwamba Wazanzibari hawa wawili ndiyo watakaoongeza idadi ya Wazanzibari ndani ya Baraza la Mawaziri ambalo nalo limekuwa sehemu ya mjadala tangu kutangazwa kwa baraza hilo.
Kwa sasa, Wazanzibari wawili tu; Dk. Hussein Mwinyi na Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, ndiyo ambao wametangazwa kuwemo kwenye baraza hilo, idadi ambayo baadhi ya wachambuzi wamedai ni ndogo kutokana na mazoea ya huko nyuma.
“Wanaosema kwamba idadi ya Wazanzibari ni ndogo wasubiri kwanza Magufuli atangaze baraza lote la mawaziri. Baada ya hapo waangalie ni asilimia ngapi kulinganisha na ilivyokuwa huko nyuma. Hata hivyo, tofauti na watangulizi wake, Magufuli yeye ataweka mtu mahali anapofaa bila ya kutazama sana masuala ya muungano.
Ndiyo maana umeona Profesa Mbarawa amepewa Wizara ya Maji ambayo si sehemu ya mambo ya Muungano. Anachoangalia yeye ni kazi tu, limeambiwa Raia Mwema.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/wazanzibar-watajwa-wizara-ya-fedha-elimu#sthash.NR0FZxgP.dpuf
Prof Rai receives an education leadership award
Prof Rai, the vice chancellor of state university of Zanzibar, is recognized for his leadership in education - receives education leadership award at World Sustainability Congress that took place in Mauritius on 9th, December.
No comments :
Post a Comment