Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, December 14, 2015

Fahamu mambo 10 muhimu ya Baraza la Dk Magufuli

Rais John Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na mawaziri baada ya kuwaapisha Ikulu jijini Dar es Salaam Alhamisi iliyopita. Picha ya Maktaba
By julius Mtatiro / Mwananchi.
Utangulizi
Desemba 10 mwaka huu, Rais John Magufuli alitangaza Baraza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Tano ambalo lina jumla ya mawaziri 34, ingawa bado hajatangaza majina manne. Tunatumia fursa hii kujadili mambo kumi muhimu yanayoambatana na baraza lake pamoja na utaratibu wa utangazaji kwa ujumla.
Udogo
Kwa kiasi fulani Rais amefanikisha ile dhana ya uundaji wa baraza dogo la mawaziri. Baraza lake lina mawaziri 19 wanaotokana na wizara 18 huku manaibu waziri wakiwa 15. Baraza hili ni dogo kwa dhana kwamba halilingani na baraza la Serikali ya Awamu ya Nne iliyokuwa chini ya Jakaya Kikwete.
Baraza la mwisho la Rais Kikwete lilifanyiwa mabadiliko makubwa mwaka 2014 kwa kupanga na kupangua mawaziri na aliunda wizara 30 zenye mawaziri 30 na manaibu waziri 23.
Kwa wastani, Serikali ya Kikwete kwa miaka yote 10 imekuwa na wastani wa wizara 28.3 zilizokuwa na wastani wa mawaziri 28 na manaibu waziri 25 kwa hiyo serikali hiyo ilikuwa inawahudumia wastani wa Watanzania 53 wenye hadhi ya uwaziri na unaibu waziri kwa wakati mmoja kwa miaka yote hiyo. Serikali ya JPM itakuwa na kazi ya kuwahudumia takribani Watanzania 34 wenye hadhi ya uwaziri na unaibu waziri, ikiwa ni pungufu ya mawaziri 20 ukilinganisha na ile ya Kikwete.
Serikali ya Magufuli imeanza na wizara 18 tu, pungufu ya wizara takribani 12 za utawala wa Kikwete na hii ya sasa imeanza na mawaziri 19 pungufu ya 11 kulinganisha na ile ya Kikwete, huku tena hii ya Magufuli ikiwa na manaibu waziri 15, ikiwa ni pungufu ya watu 10 ukilinganisha na ile ya Kikwete iliyokuwa na manaibu waziri 25.
Pamoja na juhudi hizi za Rais Magufuli, maarufu kwa kifupisho cha JPM za kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri kwa takribani asilimia 50 kulinganisha na Serikali iliyopita zinapaswa kupongezwa, lakini bado Rais anapaswa kushauriwa kuwa kama angeamua angeliweza bado kuunda Serikali yenye wizara 15, mawaziri 15 na manaibu waziri 10 peke yake. Hii ina maana kuwa angepunguza Serikali kwa asilimia 60 hadi 65 ukilinganisha na ile iliyopita. Hata hivyo mwanzo huu si mbaya.
Vijana
Jambo la pili muhimu katika baraza hili la mawaziri ni uwapo wa vijana kwa kiasi cha kuridhisha, japokuwa si wengi kama ambavyo ilitarajiwa. Kwa sababu JPM alianza kuwa Naibu Waziri akiwa kijana mdogo na akakua na kufanya kazi kubwa, ilitarajiwa kuwa angewaamini vijana wengi zaidi. Lakini katika hatua hii ya mwanzo, amekuwa na vijana wachache zaidi kulinganisha na Kikwete.
Hata hivyo, baraza la Kikwete lilionekana kuwa na vijana wengi kwa sababu lilikuwa kubwa, hili dogo la JPM lina wastani wa mawaziri vijana watano kati ya 15 waliotangazwa (wenye umri chini ya miaka 45) na manaibu waziri takribani sita kati ya 15 waliotangazwa.
Kwa maana ya kuwa na watu wepesi watakaomsaidia Rais kuendana na kasi yake, nadhani sasa anao. Na kwa maana ya kuwa na watu ambao watakuwa wanatoa mawazo ya “kisasa (ya zama za sasa)” katika Baraza la Mawaziri, naamini vijana hao wanatosha. Kwa uchache vijana hawa ni pamoja na January Makamba, Mwigulu Nchemba na Nape Nauye,
Jambo kubwa ambalo Rais anapaswa kulichukulia kwa uzito wake ni kuwapa vijana hawa nafasi ya kujifunza uongozi wa juu wa nchi na kuwasaidia wafanye majukumu yao kwa kujiamini, lakini kwa kupunguza makosa mengi yanayoweza kutokana na kujaribu.
Kwenye vikao vya Baraza la Mawaziri waachwe waseme na kutetea masuala ya msingi ambayo vijana wa Taifa hili wanayaota kila siku.
Uzoefu
Kwa kiasi kikubwa baraza la JPM limesheheni watu wazoefu kidogo kwa masuala ya uendeshaji wa Serikali. Takribani asilimia 25 ya baraza lake limesheheni watu waliowahi kuwa mawaziri bila kujali kuwa walikuwa wachapakazi au la. Lakini pia baraza hili lina wastani wa asilimia 40 ya watu ambao wamewahi kusimamia majukumu makubwa katika taasisi za umma, binafsi au wamewahi kushika nyadhifa za juu za uongozi mahali walipowahi kufanya kazi.
Hili linatupeleka katika ile dhana thabiti kwamba hakuna hata mmoja ambaye baadaye ataboronga na kuanza kujitetea kuwa alikuwa anajifunza. Kwa mtazamo wangu, kila aliyeteuliwa kuwa waziri na hata naibu waziri kwenye baraza hili bila kujali anafahamika kiasi gani kwa Watanzania, ni mtu ambaye tunaweza kujiridhisha bila shaka kuwa ana vitu kama uzoefu, elimu ya kutosha na weledi. Hivyo, akiamua kuvitumia ipasavyo anaweza kuweka tija katika wizara aliyokabidhiwa.
Mambo yote haya yanajenga uzoefu ambao ni muhimu kidogo inapotokea mtu anakabidhiwa majukumu makubwa ya serikali kama haya.
‘Bado nawatafuta’
Wakati alipotangaza baraza lake, Rais Magufuli alisema bado anatafuta mawaziri wanne kukamilisha timu yake. Jambo hili limeshtua wengi na maelezo aliyotoa Rais bado hayawezi kuwa yanaridhisha sana.
Magufuli amekuwa serikalini kwa zaidi ya miaka 20, amepata fursa ya kuzunguka nchi kwa siku 60 kuomba kura na baada ya kuchaguliwa na kuapishwa amekuwa na siku nyingine zaidi ya 40 ofisini. Kwa akili ya kawaida, anapokuja kutangaza baraza na kueleza kuwa “bado nawatafuta”, kwani anataka kutangaza Wakenya, Waganda au watu kutoka ‘mawinguni?’
Katiba yetu ya sasa inamtaka Rais ateue mawaziri kutoka bungeni, na kama mtu siyo mbunge Rais anawajibika kumteua kuwa mbunge kwanza, ndipo ampe uwaziri. Kama JPM hajaona watu katika bunge amekuwa na siku zaidi ya 100 tangu kuanza kampeni. Hajawaona Watanzania wenye uwezo walioko nje ya Bunge?
Wizara ambazo hazina mawaziri zote ni nyeti; Elimu, Fedha, Ujenzi na Utalii. Kwa mtazamo mpana tunaweza kukubaliana kuwa hizi ndizo wizara ambazo zilipaswa kupewa mawaziri haraka ili zianze kuchapa kazi.
Rais angeweza kuchukua mwaka mzima anamsaka waziri wa michezo, lakini siyo waziri wa fedha. Kwenye mfumo za serikali za Jumuiya ya Madola, ni nadra sana kukuta nchi inatangaza baraza la mawaziri lenye mapengo makubwa kabisa kwenye sekta nyeti.
Mathalani, shule zinafunguliwa mwezi Januari na Watanzania waliahidiwa elimu bure, bado siku 18 tu kabla ya kuanza mwaka mwingine ili watoto waende shule, Rais haoni umuhimu wa kuwa na waziri wa elimu akaanza kazi mapema kabisa? Pia kwenye suala la fedha mathalani, huku ni muhimu mno na kulitaka mtu wa kuanza kumsaidia kwa kasi haraka, Rais ameteua mawaziri 15 watumia fedha, lakini hajamteua waziri mmoja muhimu wa kutafuta fedha hizo, kupanga matumizi na kueleza matumizi.
Nafasi ya wanawake
Wanawake wamekuwa na nafasi ya kipekee kwenye wizara za JPM. Kati ya mawaziri na manaibu 30 waliotangazwa, kuna takribani wanawake wanane, sawa na asilimia 26.6 ya baraza zima. Idadi ya wanawake kwenye baraza la mawaziri la JPM imepunguzwa kwa asilimia 6 kulinganisha na baraza la Kikwete ambalo lilikuwa na wastani wa asilimia 32 ya wanawake kila mara. Hata hivyo Kikwete aliogelea kwenye baraza kubwa la mawaziri wapatao 50 na zaidi, kwa hiyo nadhani JPM amepunguza idadi ya akinamama kutokana na udogo wa baraza lake.
Hata hivyo, kwa mara ya kwanza mwaka huu wanawake wa Tanzania wamepata Makamu wa Rais mwanamke. Jambo hili lina maana ya kupunguza machungu yao ya uwakilishi pale inapotokea hawapo wanawake wengi.
Serikali ya JPM ina kazi kubwa ya kuinua uwezo wa wanawake, si tu kwa kuwapa nafasi za uteuzi bali kuwajenga kimfumo waonyeshe uwezo wao, wasimamie mambo makubwa katika nchi na wajiamini kama inavyopaswa kuwa.
Ni vyema siku moja Rais anayekuja awe na uhuru wa kuteua baraza ambalo litakuwa na wanaume asilimia 50 na wanawake asilimia 50, jambo hili litafikiwa kama wanawake wakijengewa mifumo imara tofauti na ya sasa ya kufanya waamini kuwa wao ni watu wa kusubiri uteuzi tu.
‘CCM kindakindaki’
Chama cha Mapinduzi CCM kimeendelea kuwa na nafasi ya kipekee katika baraza hili. Rais amewateua baadhi ya watu muhimu waliokuwa mihimili ya chama na kuwapa nafasi kwenye baraza jipya. Ukiliangalia baraza unaweza kuwaona watu hao.
Uteuzi huo una maana sasa ya kuwaondoa kwenye uongozi wa kila siku na wa moja kwa moja kwenye chama na kuwarudisha serikalini, na huenda morali hii ya Magufuli ikawazuia tena wasiendelee na utendaji wowote ndani ya chama ili kujenga Serikali imara, huku chama nacho kikijijenga kwa kuwatumia watu wenye uwezo wa kufanya hivyo na wenye nafasi ya kufanya kwa ufanisi.
Kama hili likifanyika, linaweza kuthibitisha ile dhana ya CCM kuanza kujipanga upya na hizo ni salamu za kufanyia kazi kwa vyama vya upinzani, hususan vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambavyo vinapaswa kuweka mikakati mizito ya kujipanga kuelekea 2020.
Majina makubwa nje
Baraza la mawaziri la JPM limewaacha nje wakongwe wengi  ambao wana majina makubwa kwenye siasa. Watu wengi waliamini kuwa majina kama ya Profesa Mark Mwandosya, Asha Rose Migiro, Benard Membe na Stephen Wasira yangeonekana katika baraza hili hata kwa kuteuliwa kwanza kuwa wabunge, kisha kupewa uwaziri.
Lakini pia, wakongwe wengine ambao walitarajiwa ni pamoja na Hawa Ghasia, Profesa Jumanne Maghembe, Dk Diodoras Kamala, Dk David Mathayo, Dk Mary Nagu na Peter Serukamba. Hawa ni wabunge wa sasa na hata wao wenyewe walikuwa kila wakilala wakiamka, wanaamini wana nafasi za kuwa mawaziri. Si wao tu na wananchi ambao wamezoea kuamini kuwa uwaziri ni jina kubwa basi na wao wangelitegemea hali hiyo kutokea. Baraza limekuja tofauti; wakongwe wengi waliokuwa wakipigiwa chapuo, hawamo.
Hii ina maana moja tu, kwamba enzi zina mwisho wake na hilo halijadiliki, unatumikia Serikali kwa miaka mitano, kumi, ishirini na hata thelathini – kwa ngazi za juu kabisa, lakini kuna wakati unafika unaondoka bila kujali kuwa watu walikuwa bado wanakuhitaji au la, na bila kujali ulikuwa mtendaji mzuri au la. Huwa ni suala la muda tu.
Majibu kwa waandishi
Pamoja na hayo yote, kuna jambo moja muhimu sana la kushughulikia. Hili ni Rais na vyombo vya habari. Ukifuatilia maswali ambayo waandishi walimuuliza baada ya kutangaza baraza na majibu yake, unagundua kuwa Rais anahitaji wataalamu washauri waliobobea na wasiomuogopa.
Rais hana budi kutambua kuwa unapokuwa Rais, una wajibu wa moja kwa moja wa kutoa majibu au ufafanuzi kwa masuala ya msingi unayoulizwa, vinginevyo watendaji wa ngazi za chini yake kwa maana ya mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, wilaya ama wakurugenzi, nao watachukulia aina ya majibu yake kama mtindo wa kuiga kila afanyacho Rais.
Mathalani, mhariri wa gazeti la Jamhuri, Manyerere Jackton alimuuliza Rais Magufuli swali kwamba “kwa kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri na kwa kulinganisha na tulipotoka, Serikali itakuwa imepunguza kiasi gani?”.
Rais alimjibu, “wewe ndiye utapiga hesabu, kwa vile ni mmiliki wa gazeti. Huwa ukipiga hesabu huwa unapata kiasi gani?”
Mwandishi mwingine aitwaye Raymond Nyamzihula wa Uhai Production, alimuuliza, “siku saba zimetimia, wafanyabiashara wamesharejesha zile hela?” Rais alijibu, “swali hilo kamuulize kamishna wa kodi wa TRA”.
Katika mkutano huo, mwandishi mwingine alimuuliza JPM akisema: “Kuna ina mawaziri wawili, huko kazi ni ngumu?”, lakini Rais alijibu “Kafanye utafiti kwenye hiyo wizara, zimeunganisha wizara ngapi utapata majibu.” wizara
Aina hii ya majibu ya Rais ni dhahiri kuwa inawafanya waandishi wa habari wakatafakari waandike wanachojua wao na siyo kile ambacho Rais alikusudia. Lakini pia majibu ya namna hiyo yanakera.
Rais ni mtu mwenye mamlaka makubwa, lazima ashauriwe na afundishwe kuwa hivi sasa yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa nchi yetu, ana wajibu wa moja kwa moja kutoa majibu ya maswali anayoulizwa, ili watendaji wake nao wajifunze kutoka kwake. Vinginevyo atatengeneza Serikali ya maswali juu ya maswali.
Semina elekezi
Ni kawaida kuwa unapounda uongozi wowote ukatenga muda na mahali ili kukutana na uliowateua na kufanya nao mazungumzo ya siku kadhaa ya namna ya kujipanga na namna unavyotaka kazi zifanyike. Muda huo hutumiwa pia kukaa na kuwasikiliza wasaidizi wako, lakini pia kuwajulisha mipaka ya kila mmoja wao na namna watakavyopaswa kufanya kazi kama ambayo wewe uliyewateua ungependa iwe.
Rais ametamka wazi kuwa kwenye utawala wake hakuna semina elekezi kwenye baraza la mawaziri. Sikuelewa hasa anamaanisha nini. Ambacho anaweza kuungwa mkono ni dhana ya kuondoa gharama kubwa katika ufanyaji wa semina elekezi hiyo, mathalani angeliweza kutamka kuwa bajeti ya semina elekezi imepunguzwa kwa asilimia 90, yaani angeweza kuamua kuwa badala ya kutumia Sh2 bilioni kwa ajili ya semina hiyo, sasa zitumiwe Sh50 milioni tu. Mawaziri na manaibu wao watokee majumbani mwao, semina ifanyikie ikulu, gharama ziwe za vyakula tu na posho angezifuta.
Lakini kusema kuwa hakuna semina elekezi kabisa na kwamba mawaziri wakajifunze huko huko. Hili si jambo sahihi hata kidogo. Ili Serikali ya JPM ifanikiwe lazima mawaziri waelewe mipaka yao, kazi zao, itifaki, nini watapaswa kufanya na nini hawapaswi kufanya, lazima wajue ni uamuzi upi utakwenda kinyume na matarajio ya Rais.
Kuwanyima kabisa mawaziri semina ya namna hii ambayo ingeweza kufanywa hata kwa kutumia maji na soda, ni kituko. Jambo hili nalo lazima litazamwe kwa macho mawili na lisipigiwe makofi ya pongezi tu bila kuangalia athari za kutowaweka mawaziri hawa chini.
Maadili
Rais aliahidi angeteua mawaziri wachapakazi, wenye maadili na wasio na kashfa. Wadau wengi wamelalamikia uteuzi wa Profesa Sospeter Muhongo ambaye alijiuzulu dakika za mwisho za uongozi wa awamu iliyopita kwa sababu ya kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, wakati akiwa Waziri wa Nishati na Madini.
Pamoja na kwamba Profesa Muhongo hakuhusika moja kwa moja na kashfa ile, lakini kitendo cha kujiuzulu kutoka kwenye wizara husika halafu baada ya miezi michache Rais mwingine anamteua kwenye wizara ileile, ni kuleta mgogoro ambao hauna tija.
Huenda Rais alipaswa kumteua Profesa Muhongo baada ya muda fulani, lakini pia kama anataka kuongoza Serikali kwa uwazi angeliweza hata kutoa maelezo ya kina kwa nini amemteua ili kuwafanya Watanzania wengi ambao walifuatilia kashfa ile wajue sababu za kumrejesha. Kumteua kimyakimya na kuliacha jambo hilo hewani, kunazua ubashiri mwingi ambao huenda si wa kweli au maswali ambayo hayana maana kwa sasa.
Rais hakupaswa kuangalia  upande mmoja tu ambao unaona Muhongo alionewa, bali angeangalia pia upande ambao unaona Profesa Muhongo hakuonewa ili kutoa maelezo ya kuwaridhisha wale wote ambao wanadhani kuwa alihusika na kashfa ile au hakuhusika.
Kumteua kwenye baraza la mawaziri kumeibua “minong’ono” ya kimaadili. Kuna watu wanasema, mbona hata Edward Lowassa anayetangazwa kuwa fisadi alijiuzulu baada ya kuona ameelekezewa tuhuma za ufisadi ambazo hazijathibitishwa hadi leo kama ilivyo kwa Profesa Muhongo?
Hitimisho
Rais Magufuli ameshamaliza sehemu kubwa ya kazi yake, bado ana kiporo cha wizara kadhaa muhimu. Kasi ya utendaji wake itaanza kupimwa mara moja kwani sasa ana Serikali. Baada ya siku 90 tokea baraza hili liteuliwe Watanzania watakuwa wanajua nini kimo ndani, vichwa vya mawaziri vina uwezo gani na kero gani zimeanza kutatuliwa. Wakati unakwenda haraka, tusubiri tuone na kupata majibu.
Tunalitakia kila la heri baraza hili jipya la mawaziri la Serikali ya Awamu ya Tano ya JPM na kauli mbiu yake ya “Hapa Kazi Tu”.
(Julius Mtatiro ni mshauri mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya kisiasa. Ana cheti cha juu cha sarufi, Shahada ya Sanaa (B.A - Hons), Shahada ya Umahiri ya Usimamizi wa Umma (M.A - Hons) na Shahada ya Sheria (L LB - Hons) +255787536759,juliusmtatiro@yahoo.com, https://www.facebook.com/julius.mtatiro, - Uchambuzi huu ni maoni binafsi ya mwandishi).

No comments :

Post a Comment