WAKATI fulani mnamo mwaka 1958 Julius Nyerere, wakati huo tayari akiwa ni kiongozi wa chama cha TANU, alikutana na Tom Mboya mjini Nairobi. Katika mazungumzo yao, anaandika Tom Mboya, wazo la kuunda Vuguvugu la Ukombozi wa Kimajumui wa Afrika kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati, yaani PAFMECA lilizaliwa. PAFMECA ikaasisiwa mwezi Septemba mwaka 1958 miezi michache kabla ya Mkutano wa Watu wote wa Afrika (All African Peoples’ Congress) uliokuwa umeitishwa na Nkrumah, kiongozi wa Ghana. Lengo la PAFMECA lilikuwa kuvikutanisha vyama vyote vya ukombozi katika eneo la Afrika Mashraiki na Kati na kuratibu na kuimarisha nguvu katika mapambano yao. Mkutano uliozaa PAFMECA ulikuwa pia ni maandalizi ya wajumbe toka eneo husika la bara kwa ajili ya Mkutano wa Accra.
Mpaka wakati huo ambapo PAFMECA inaundwa huko Ghana, chini ya uongozi wa Nkrumah, ndio ilokuwa Mecca ya harakati za ukombozi wa bara la Afrika. Hii ikitokana na mtazamo wa kimajumui wa Kiafrika wa Nkrumah, ambae akiamini kwamba Uhuru wa Ghana ulikuwa ni hatua tu ya kufikia ukombozi wa bara zima la Afrika, na kwamba Ghana haiwezi kuwa huru kama sehemu nyingine Barani hazikuwa huru.
Ni wazi kwamba katika kipindi hiki jina lililosikika na kuhusishwa sana na Umajumui wa Kiafrika ni la Kwame Nkrumah. Nyerere kama Mmajumui hakujulikana sana wakati huu. Kwa Nyerere, hata walipokuwa wanaunda PAFMECA msukumo ulikuwa namna ya kuunganisha na kuratibu mapambano ya ukombozi na kusaidiana katika harakati hizo na sio ujenzi wa Afrika yenye serikali moja.Mpaka wakati huo ambapo PAFMECA inaundwa huko Ghana, chini ya uongozi wa Nkrumah, ndio ilokuwa Mecca ya harakati za ukombozi wa bara la Afrika. Hii ikitokana na mtazamo wa kimajumui wa Kiafrika wa Nkrumah, ambae akiamini kwamba Uhuru wa Ghana ulikuwa ni hatua tu ya kufikia ukombozi wa bara zima la Afrika, na kwamba Ghana haiwezi kuwa huru kama sehemu nyingine Barani hazikuwa huru.
Nyerere alikuwa kiongozi wa Chama cha Ukombozi (TANU) ambacho katika kipindi kifupi toka kiasisiwe kilikuwa tayari kimejipatia umaarufu mkubwa. Asili ya TANU ilikuwa African Association, chama cha Waafrika kilichoasisiwa mwaka 1929, kilokuwa na mtazamo wa kuwafikiria Waafrika kama wamoja. African Association, kilikuwa na wanachama na matawi katika sehemu mbalimbali za koloni la Tanganyika na Zanzibar. Wenyewe katika African Association wakijitambulisha kama Waafrika weusi wasiojali asili, nchi, dini, wala kabila la mtu.Kuwa Mwafrika mweusi ilitosha.
Katika mfano mmoja wa mawasiliano baina ya T. Edward John Mwangosi [Honorary Secretary wa African Association Dodoma] na Katibu Mkuu wa African Association Dar es Salaam, anaandika hivi juu ya African Association:
… nia yetu i pamoja na wale wote wanaopenda kutumia jina la “African Association”. Chama hiki kina maana sana pana Afrika kwa kuwa Wa-Afrika wengi ni mataifa mbali-mbali – wa kenya, Uganda, Nyasaland, Belgium Congo na Tanganyika tena kati yao kila watu wanajaribu kuweka chama chao kwa taifa lao au kwa dini yao bali African Association ni Chama cha Wa-Afrika wote wa pande zozote na wadini yeyote na kabila lolote na wasio dini wastaarabu na wasio wastaarabu mradi wakiwa weusi wa Afrika.
Pamoja na kwamba African Association hakikuwa chama cha kupigania uhuru lakini kilikuwa na mtazamo mpana wa Uafrika. Na tayari katika mwaka 1946 kilikuwa kimeanzisha mawasiliano na Shirikisho la Wamajumui wa Kiafrika (The Pan-African Federation) lililokuwa London, Uingereza, na mmoja wa viongozi wao akiwa George Padmore. Tofauti ya dhana ya Mwafrika ya African Association na ya Nyerere ni kuwa wakati kwa African Association Mwafrika ni mtu mweusi kwa Nyerere Mwafrika ni mtu yeyote aliyechagua kuishi na kupafanya Afrika nyumbani kwao. African Association ilijikita zaidi kwenye umoja wa watu weusi bila kujali dini, kabila na tofauti nyingine, lakini sio moja kwa moja kwenye umajumui. Hata hivyo, tokea mapema, Nyerere, akiwa bado mwanafunzi pale Makerere, alikuwa na mahusiano na mawasiliano na baadhi ya watu wa African Association. Na mmoja kati ya watu hao ni Mwangosi ambaye anamtaja kama mtu aliyemshauri aanzishe tawi la African Association pale Makerere badala ya kuanzisha chama kipya. Hapana shaka kuwa fikra za umajumui wa Kiafrika za Nyerere zilitokana pia na kusoma na kufuatilia kwake vuguvugu la umajumui wa Kiafrika kwa wakati huo.
Nyerere hakuhudhuria Mkutano wa All African Peoples Conference ulioandaliwa na Nkrumah. Hili ni suala linalohitaji uchunguzi zaidi, ingawa wakati mkutano huo ukiandaliwa Tanganyika ilikuwa ikijiandaa kwa uchaguzi wa kwanza ambao ungeipa Tanganyika Serikali ya Madaraka (Responsible Government). Hii ilifanya Nyerere, mpaka wakati huo, asijulikane sana katika nyanja za mijadala ya kimajumui wa Kiafrika. Lakini tokea mwaka 1961, mara tu baada ya Tanganyika kupata uhuru wake, Nyerere alianza kuchomoza kama kiongozi mmajumui wa Kiafrika na Tanganyika ikaanza kuipiku Ghana kama Mecca ya wapigania uhuru barani. Ni wakati huo ambapo Nyerere alianza kuzungumzia masuala yasiyoihusu nchi yake tu bali nchi nyingine za Kiafrika. Hii iliinua nafasi yake kama msemaji na mtetezi wa nchi za Kiafrika. Msimamo wake juu ya Tanganyika kuwa au kutokuwa mwanachama wa Jumuiya ya Madola kama Afrika Kusini, chini ya ubaguzi wa rangi, ingeruhusiwa kuwa mwanachama ulivutia hisia za wafuatiliaji wengi wa mambo barani.
Vuguvugu la ukombozi lilikuwa limepamba moto na mikutano na majadiliano ya kuunda umoja wa Afrika yalikuwa yameshika kasi. Makundi tofauti yenye kujumuisha nchi mbalimbali za Kiafrika yalizuka na yakachukua misimamo iliyokinzana juu ya aina ya umoja wa Kiafrika unaotakiwa na namna utakavyofikiwa. Nkrumah aliongoza kundi la nchi lililoamini kuwa wakati wa Afrika kuungana ulikuwa umefika huku kundi jingine, ambalo baadae Nyerere ndio aliibuka kama kinara wake katika kulielezea, likichagiza kuwa wakati ulikuwa bado na sharti waende pole pole. Ni katika mijadala juu ya vuguvugu hili ambapo fikra za Nyerere juu ya umajumui wa Kiafrika zilipoanza kuchomoza wazi wazi.
Mtazamo wa Nyerere juu ya umajumui wa Kiafrika umejikita kwenye maeneo makuu sita. Kwanza, kwamba umoja ndio njia pekee ya kuharakisha na kuleta uhuru wa nchi za Kiafrika; pili, kwamba umoja huo huo ndio njia pekee itakayoisaidia Afrika kujiletea maendeleo yake, na hivyo kupambana na maadui ambao akiwaongelea sana - ujinga, maradhi na umaskini; tatu, kwamba umoja ndio njia pekee itakayoihakikishia Afrika usalama na uhuru wake kamili; nne, wakati gani umoja wa Afrika uundwe, na kwa njia au namna gani umoja huo utafikiwa; tano, ni nani hasa ataongoza jitihada za kuihimiza na kuisukuma Afrika iungane; na sita, pindi Afrika itakapoungana umoja huo utachukua sura gani hasa. Katika azma hizi Nyerere hakutofautiana sana na wenzake; tofauti kubwa ilikuwa kwenye wapi pa kuanzia – kutoka umajumui kwenda utaifa, au kutoka utaifa kwenda umajumui.
Kuhusu umoja na suala la ukombozi Nyerere aliamini kuwa ili kuharakisha ukombozi wa Afrika umoja ulikuwa ni lazima. Kwake yeye umoja ulikuwa ni silaha muhimu dhidi ya ukoloni na ubeberu. Lilikuwa ni suala la kimantiki tu kutambua kuwa pale watu wanapogundua kuwa na tatizo linalowakabili kwa pamoja, punde hugundua kuwa suluhu yake itapatikana kwa wao kushirikiana. Chimbuko la mtazamo huu linatokana kwa kiasi kikubwa na uzoefu wake wa kuendesha harakati za ukombozi katika Tanganyika, koloni ambalo chama kimoja tu kilichipuka na kupevuka huku kikiungwa mkono na sehemu kubwa ya umma wa Watanganyika. Nyerere alitaka kuuelekeza uzoefu huu katika ngazi ya bara na kwenye mradi wa kuunda umoja wa Afrika bila mafanikio makubwa. Kwa upande mmoja alichukulia mambo kwa wepesi bila kuzibaini tofauti za kijamii na kisiasa katika kila nchi, na kwa upande mwingine, hakuzibaini nguvu za ubeberu na jitihada zake za kukwamisha ajenda yoyote yenye lengo la kuleta ukombozi wa kweli kwa Waafrika.
Wakati nchi za Afrika zilipokuwa zikipata uhuru dunia ilikuwa kwenye vita baridi, na wakoloni wakiandaa watawala ndani ya Afrika watakaowaendesha nyuma ya pazia kwa mtindo wa ukoloni mamboleo. Kwa hivyo kulikuwa na hali ya kutiliana mashaka ya nani ni nani na yuko upande gani katika siasa hizi za dunia. Mathalani pale Tanzania ilipochaguliwa na kuafiki kuwa mwenyeji wa Kamati ya Ukombozi wa Bara la Afrika, Nkrumah alipinga kwa sababu akimtilia mashaka Nyerere kuwa ni kibaraka wa nchi za kibeberu. Hoja ya Nkrumah ilichochewa na kuitwa kwa majeshi ya Uingereza nchini Tanganyika kuja kusaidia kuzima maasi ya wanajeshi mwaka 1964.
Nyerere aliamini kwamba mapambano dhidi ya ukoloni yalikuwa ni kwa ajili ya kuwawezesha Waafrika kujiamulia mambo yao wenyewe na kwa hivyo kujiletea maendeleo yao wenyewe. Uhuru ulitakiwa kuwasaidia Waafrika kupambana na wale maadui wakuu wa maendeleo. Lakini alibaini kuwa hakuna nchi ya Kiafrika peke yake ambayo ingeweza kufanikiwa katika vita hii bila kushirikiana na nchi zingine za Kiafrika. Kwenye barua aliyomwandikia Mzee Kenyatta, Rais wa Kenya, mwaka 1963, Nyerere anabainisha kwamba Tanganyika ilitaka Shirikisho la Afrika Mashariki baada ya kugundua kuwa dola ya Tanganyika ilikuwa dhaifu mno kama nyenzo ya kukamilisha mapinduzi yaliyoanzishwa na mapambano ya uhuru. Na kwa maoni yake ukweli huu ulikuwa ni dhahiri kwa nchi zote barani Afrika. Hii ilitokana na ukweli kwamba hata baada ya nchi za Afrika kupata uhuru rasilimali zake nyingi ziliendelea kushikiliwa na kuthibitiwa na nchi za kibeberu na makampuni yao.
Nyerere pia alibaini kuwa hali ya udunishwaji wa maendeleo ya nchi za Afrika (underdevelopment) ilidhoofisha jitihada zozote za nchi za Kiafrika za kujiletea maendeleo yao wenyewe. Na hii ilikuwa hivyo kwa sababu ya mfumo wa biashara ya kimataifa kutokuwa sawa na hivyo kuinyonya tu Afrika. Kutokana na uduni wa maendeleo yake, nchi nyingi za Afrika ni tegemezi na hushindana katika kutafuta misaada na upendeleo toka nchi tajiri na zenye nguvu. Njia pekee ya kupambana na hali hii, Nyerere alipendekeza, ni umoja ambao utaiwezesha Afrika kuzitumia rasilimali zake kwa manufaa yake. Katika fikra hizi Nyerere hakutofautiana sana na Nkrumah japo Nkrumah alilitazama suala hili kwa upana na kina na katika muktadha wa siasa-uchumi wa kibeberu.
Uduni wa maendeleo ya nchi za Kiafrika na utegemezi wao kwa nchi za kibeberu unazipunguzia, kama sio kuziondolea kabisa, uhuru (sovereignty) nchi za Kiafrika. Mbali ya hoja ya kiuchumi, Nyerere anakwenda mbali zaidi na kuangalia uwezo mdogo wa nchi moja moja ya Kiafrika katika kupambana na hila za mataifa makubwa za kuzigawa na kuzigombanisha kwa maslahi ya ubeberu. Na kwa sababu hiyo aliona umoja wa nchi za Kiafrika kama ndio njia pekee ya kuimarisha uhuru na usalama wao. Katika maisha yake yote, aliamini kuwa ‘vinchi’ vidogo vidogo vya Afrika visingekuwa huru bila kuunganisha nguvu zao kwa kuunda Serikali moja ya Afrika.
Baada ya kudurusu fikra na mtazamo wa Nyerere kuhusu umajumui wa Kiafrika, jambo moja linajitokeza - nalo ni kwamba fikra zake zinatokana na utambuzi na hisia za utaifa ndani ya mipaka ya ukoloni. Hisia hizi zinaweza kuwa na sura mbili. Moja ni ile ya kutambua kwamba Waafrika wa Tanganyika walikuwa wananyonywa, kudhalilishwa, na kupuuzwa ndani ya ukoloni; lakini hali hiyo hiyo iliwakabili Waafrika katika makoloni mengine pia, na hivyo ili kuondosha upuuzwaji na udhalilishwaji wa Mwafrika wa Tanganyika sharti kukomesha udhalilishaji wa Waafrika katika bara lote. Kwa hivyo umoja ulikuwa ni njia muhimu sana katika kuharakisha uhuru wa kila nchi na kukomesha madhila haya. Na sura ya pili ni utambuzi kuwa ‘vinchi’ vidogo vidogo vya Afrika na dola zake havikuwa kitu chochote mbele ya mataifa tajiri na ya kibeberu. Na hivyo njia pekee ya kukabiliana na hali hiyo ilikuwa ni umoja. Hii ni tofauti na Nkrumah ambaye toka awali aliitazama Afrika kama ilitarajiwa kupambana na kupata uhuru ikiwa kama moja. Ndio maana hata pale Ghana ilipopata uhuru wake mwaka 1957 Nkrumah alisema uhuru wa Ghana haukuwa na maana yoyote kama Afrika yote haikuwa huru. Ni tofauti pia na chimbuko la umajumui wa Kiafrika, ambalo lilikuwa na itikadi ya umajumui wa watu, siyo madola. Dhana ya awali ya umajumui wa Kiafrika ilikuwa mshikamano zaidi kuliko umoja – mshikamano katika kuongoza madai ya watu weusi ya utu, usawa na kutokubaguliwa.
Aidha Nyerere alionesha hofu yake kuhusu mipaka iliyoachwa na wakoloni kuwa itakuwa chanzo cha migogoro baina ya nchi za Kiafrika na kuzidhoofisha zaidi. Ili kuepuka hilo aliona umoja kama njia pekee itakayosaidia kuepusha migogoro hiyo kwa sababu hakutakuwa tena na mipaka baina ya nchi za Kiafrika.
Pamoja na imani yake kubwa katika umajumui wa Kiafrika Nyerere hakuamini kabisa kwamba umoja wa Afrika unaweza kutokea haraka na mara moja kama alivyoamini Nkrumah. Msimamo huu wa Nyerere ulianza kujidhihirisha zaidi mara baada matumaini ya kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki kupotea kabisa. Ukichunguza kwa makini hoja alizotumia Nyerere kushawishi viongozi wenzake katika Afrika Mashariki ili wakubali kuundwa kwa shirikisho, utabaini kuwa zinafanana sana na hoja za Nkrumah za kudai na kuhimiza kuundwa kwa umoja wa Afrika kwa haraka na mara moja
Katika kuhimiza kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki pendekezo la Nyerere lilikuwa ni kwamba shirikisho liundwe kabla ya nchi za Afrika Mashariki hazijapata uhuru wake. Kwa mara ya kwanza wazo hili lilitolewa na Nyerere katika mkutano wa PAFMECA mwaka 1960. Wakati huo ni Tanganyika pekee ndio ambayo ilikuwa na serikali ya madaraka na ndiyo pekee iliyokuwa ikijua tarehe ya uhuru wake toka kwa Waingereza. Lakini, kama inavyojulikana na wengi, Nyerere alikuwa tayari kuahirisha tarehe ya uhuru wa Tanganyika ili kusubiri nchi zote za Afrika mashariki ziweze kupata uhuru wao kwa pamoja zikiwa tayari zimeungana.
Moja ya sababu za hoja yake ya kuundwa kwa shirikisho kabla ya uhuru ni kwamba hisia za umoja zilikuwa kubwa na dhahiri zaidi miongoni mwa wapigania uhuru wakati wa harakati za kupigania uhuru kuliko wakati mwingine wowote. Vyama na viongozi wengi waliounda na kuongoza vuguvugu la kupigania uhuru wa nchi zao walikuwa tayari wamejenga ushirikiano mkubwa baina yao. Kwa hivyo ilikuwa rahisi kutumia vuguvugu hilo kuyaunganisha makoloni yote ya Afrika Mashariki chini ya Mwingereza. Aidha Nyerere alihofia kwamba mara baada ya uhuru viongozi wangejishughulisha zaidi na matatizo ya serikali zao na hatimaye kusahau faida kubwa itokanayo na umoja wa Afrika (au shirikisho); na kuwepo kwa maafisa wengi wanaotumikia nchi zao na kufaidika na maslahi na marupurupu yanayoambatana na vyeo vyao kungejenga kada kubwa zaidi ya wapinzani wa wazo la kuunda Serikali moja ya shirikisho kwa sababu tu ya kulinda nafasi na maslahi yao. Na jambo jingine ambalo aliliona lingeweza kuwa kikwazo, ni ugumu wa nchi kusalimisha mamlaka yake kamili (sovereignty) mara tu baada ya kuyapata.
Katika kubadilika kwake kifikra, na hasa alipoanza kuzungumza habari ya kufikia umoja hatua kwa hatua, Nyerere alisahau mambo haya muhimu na akapingana na Nkrumah kwa misingi hii. Hata hivyo karibu na mwisho wa miaka ya 1990 Nyerere alirejea hoja hii na kukaribia kukiri kuwa Nkrumah alikuwa sahihi. Miaka ya 1960 Nkrumah alisisistiza kwamba Afrika sharti iungane wakati ule, au sivyo haitaungana asilani kwa sababu utashi wa umajumui ungehama kutoka kwa watu na kujikita kwenye dola na viongozi wake. Yaani medani ya mapambano ya kimajumui ingebadilika.
Nyerere aliwashambulia waliodai kuwa muda wa kuunda Shirikisho ulikuwa bado; hawa aliwaita kina “bado kidogo”, ambao wakidai kuwa uundwaji wa shirikisho kabla ya uhuru ungechelewesha uhuru wa kila nchi. Alishangaa vipi hoja iliyotumiwa na mabeberu kupinga kupatikana kwa uhuru wa nchi za Kiafrika kwa madai kuwa zilikuwa “bado kidogo” kupata uhuru kwa sababu ya ukabila, udini, na ukanda itumiwe na Waafrika wenyewe. Ndani ya Afrika mashariki hoja ya bado kidogo ilitokea Uganda, hasa miongoni mwa Wabaganda ambao wakihofia kumezwa kwa hadhi yao maalumu ndani ya Uganda na jumuiya kubwa itakayojumuisha muungano wa nchi nyingi.
Tofauti na alivyotarajia Nyerere, upinzani dhidi ya shirikisho la Afrika mashariki ulizuka kutoka ndani ya Afrika mashariki na kutoka sehemu zingine za Bara la Afrika. Msukumo wa wazi dhidi ya shirikiso kutoka nje ya Afrika mashariki ulitoka Ghana. Mwanahistoria Basil Davidson, katika kitabu chake cha Black Star: A View of The Life and Times of Kwame Nkrumah anabainisha kuwa Nkrumah, sio tu hakukubaliana na uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki lakini pia alifanya jitihada za wazi wazi za kuingilia na kujaribu kuuzuia mchakato wa uanzishwaji wake, jambo lililomkera sana Nyerere. Hoja ya Nkrumah dhidi ya Shirikisho la Afrika Mashariki ni kwamba ushirikiano wa kikanda ilikuwa ni namna nyingine ya kuigawa Afrika vipande vipande na kuchelewesha umoja kamili wa Afrika yote. Nkrumah pia alitilia mashaka chanzo cha msukumo wa Shirikisho, na akimshuku Nyerere kuwa alikuwa akitekeleza matakwa ya nchi za kibeberu. Aidha, kwa mujibu wa chapisho maarufu la Chama cha Nkrumah, Spark, Shirikisho la Afrika Mashariki lilionekana kwenda kinyume na Makubaliano ya Addis Ababa yaliyoanzisha OAU.
Kuingilia kwa Nkrumah katika mchakato wa uundwaji wa Shirikisho kulizua malumbano makali baina yake na Nyerere. Mwezi Juni 1963 Nyerere alikuwa amewaandikia marais mbalimbali wa Kiafrika kuwajulisha juu ya azimio la viongozi watatu wa Afrika mashariki la kuunda shirikisho. Mmoja wa watu aliowatumia barua hiyo ni Nkrumah. Majibu ya Nkrumah kwa Nyerere yalimkasirisha sana Nyerere na kumfanya amjibu kwa hisia kali na za bezo. Katika baadhi ya majibu ya madai ya Nkrumah Nyerere alimshangaa Nkrumah katika kuamini kwake kuwa eti nchi tulizorithi kutoka ukoloni ndio ziwe nguzo muhimu ya umoja wa Afrika na nchi zinazoundwa kwa kuunganisha nchi kadhaa za Kiafrika ziwe kikwazo cha uundwaji wa umoja wa Afrika. Katika kuendelea kuteteta uundwaji wa Shirikisho, Nyerere alidai kuwa Shirikisho au umoja na Serikali za kikanda zinapunguza idadi ya nchi zitakazokuwa zikikutana kwenye mikutano ya OAU na kujadili suala la umoja, akiamini kuwa ni rahisi kufikia makubaliano mkiwa wachache kuliko mkiwa wengi. Kisiasa hili halikuwa tokeo la lazima kwani kama tulivyokwisha dokeza, pamoja na harakati za Nkrumah kukwamisha Shirikisho, siasa za ndani ya Uganda ziliifanya Uganda ianze kuvuta miguu kuelekea Shirikisho hata baada ya Waziri wao Mkuu, Milton Obote, kuwa ameshiriki katika mkutano uliopitisha azimio la kuundwa shirikisho.
Shirikisho la Afrika Mashariki halikupatikana kama ilivyoazimiwa. Hii illimfanya Nyerere kuanza kutilia mashaka nia na azma ya viongozi wote wa Kiafrika ya kuunda umoja kamili wa nchi za Afrika. Fikra hizi za Nyerere zilitokana na mosi, kitendo cha Nkrumah kuingilia mchakato wa kuunda shirikishso, na pili, Nkrumah kuendelea kumshambulia Nyerere na kumsema kuwa alikuwa kibaraka wa ubeberu. Malumbano ya Nyerere na Nkrumah, hasa kwa njia za barua, yaliyoanza tokea mwaka 1960, yalifikia upeo wa juu pale Nkrumah alipoishambulia Tanganyika na Kamati ya Ukombozi ya OAU. Nkrumah hakuwa amekubaliana, hata huko nyuma, na Tanganyika kupewa heshima ya kuwa makao Makuu ya Kamati ya Ukombozi. Ni katika Mkutano wa OAU wa Cairo wa mwaka 1964, ambapo Nyerere aliachana na hotuba yake iliyoandikwa na kujibu mashambulizi ya Nkrumah. Katika mashambulizi yake, Nyerere alihoji kama kweli Nkrumah alikuwa na nia ya dhati ya kuona bara la Afrika likiungana. Nyerere alisema kwamba wakati fulani alikuwa akifikiri kuwa viongozi wote barani Afrika walikuwa wana nia ya dhati juu ya suala la umoja. Lakini hapo alitamka wazi hofu yake kuwa si viongozi wote walikuwa na imani na nia hiyo kwa dhati. Alibainisha makundi mawili ya viongozi, wale waliotaka umoja wa Afrika kwa dhati kwa upande mmoja, na wale waliokuwa wakitumia hoja ya umoja kama propaganda. Hapana shaka Nyerere alimweka Nkrumah katika hilo kundi la pili, kwa sababu katika hoja hiyo pia alirejea jitihada za baadhi ya nchi zilizofanya hila ili kuzuia kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki.
Mtazamo wa Nyerere juu ya aina na muundo wa serikali ya Umoja wa Afrika au ile ya Shirikisho la Afrika Mashariki ni Serikali ya Shirikisho yenye nguvu na mamlaka kamili na makubwa. Alizitarajia nchi zote zilizokuwa tayari kuwa sehemu ya umoja wa Afrika kusalimisha kwa hiyari mamlaka yao kamili (sovereignty) kwa Serikali ya Shirikisho. Serikali hii ndio ingekuwa mwakilishi na msemaji mkuu wa masuala yote yanayoihusu Afrika kimataifa. Na serikali hiyo ingewajibika kutekeleza na kusimamia mambo yafuatayo - Mambo ya nje, Ulinzi, Uraia, Sarafu, Ushuru wa forodha, Biashara ya nje na Madini. Orodha ingeweza kuongezeka lakini haingekuwa pungufu ya mambo haya. Aidha Nyerere alibainisha masuala mengine ambayo yangekuwa chini ya usimamizi wa pamoja wa mamlaka ya serikali ya shirikisho la Afrika na za kila nchi (concurrent list). Hata hivyo pale ambapo mgogoro ungetokea serikali ya shirikisho ndio ingekuwa na mamlaka ya mwisho. Msimamo wake huu kwa kiasi kikubwa ulifanana na ule wa Nkrumah.
Kwa muda mrefu suala la umoja wa Afrika lilihusisha zaidi viongozi wa kisiasa na maafisa waandamizi wa Serikali. Suala moja ambalo Nyerere hakulizungumzia sana, japo linajitokeza kwenye baadhi ya hotuba na maandishi yake, ni la nani hasa atasukuma mbele jitihada za ujenzi wa umajumui wa Afrika. Fikra zinazochomoza katika maandishi hayo ni kuwa dola au serikali ndizo zenye jukumu la kuendeleza jitihada za kuunganisha bara la Afrika. Mfano, alipokuwa anapingana na hoja ya waliotaka nchi zote za Afrika Mashariki zipate kwanza uhuru wao ili baada ya hapo kila nchi itafute ridhaa ya watu wake juu ya namna ya kujiunga na Shirikisho, Nyerere hakuona haja ya kufanya hivyo. Yeye alidhani ikiwa nchi zote zingekuwa zimefikia hatua ya Serikali ya Madaraka na zinazo wawakilishi katika Baraza la Kutunga Sheria (LEGCO) kama ilivyokuwa Tanganyika mwaka 1959, ingetosha kuwauliza wawakilishi hao na jibu lao lingetosha kuhalalisha kuundwa kwa shirikisho. Na ndivyo ilivyokuwa wakati Tanganyika na Zanzibar zilipoungana mwaka 1964. Hata hivyo tofauti iliyopo kati ya LEGCO na Bunge la Tanganyika ni kuwa wapiga kura wachache zaidi walishiriki kuwachagua wajumbe wa LEGCO. Na haki ya kupiga kura nyakati zile ilibagua kwa vigezo vya elimu na mapato. Hivyo Watanganyika wengi hawakushiriki uchaguzi wa 1959. Lakini swali muhimu la kujiuliza ni kuwa katika jambo kubwa na muhimu kama hili iweje watu wasiulizwe?
Mwaka 1966 Nyerere alihutubia mkusanyiko wa wafanyakazi, wanataaluma na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zambia. Na jambo moja alilolieleza ni mtanzuko (dilemma) anaokutana nao kiongozi wa Kiafrika aliyeko madarakani ambaye pia ni muumini wa umajumui wa Kiafrika. Kiongozi wa namna hiyo anaweza akajikuta akivutwa na masuala na matatizo ya nchi yake na hivyo kusahau au kutokuwa na muda wa kufikiria masuala ya umoja wa Afrika. Nyerere alidhani kuwa katika hali kama hiyo wenye jukumu la kuwafanya viongozi wa Kiafrika waendelee kufikiri na kuendeleza jitihada za ujenzi wa umoja wa Kiafrika ni wanataaluma na wanafunzi wa vyuo vikuu vya Kiafrika. Kwa hivyo hata katika hotuba hiyo Nyerere alikuwa anasema kuwa jukumu la msingi la kuleta umoja ni la viongozi wa serikali. Na kazi ya wasomi ni kuwakumbusha wakati wote juu ya jukumu lao hilo. Mantiki ya mtazamo huu, hasa kwa wasomi, imo kwenye nafasi ya vyuo vikuu na wanavyuo kwa maana ya wanataaluma na wanafunzi.
Lakini katika Tanzania jambo moja hatuwezi kulibeza. Japo Nyerere akiuona umajumui wa Kiafrika kama mradi wa dola, dola ya wakati wake angalau ilijitahidi kuwafunda vijana wa Kitanzania tokea mashuleni wakue wakiwa na fikra na mitizamo ya umajumui wa Kiafrika. Na kwa sababu ulikuwa ni mradi wa dola pindi dola ilipoachana na mradi huo mitazamo ya kimajumui wa Kiafrika imedhoofu sana katika nchi zetu. Watu wengi na vijana katika bara la Afrika wamejaa fikra za utaifa, na kadri siku ziendavyo fikra hizo zinazidi kuelemea kwenye ukabila na udini. Suala la kuendelea kujadili kwa kina ni hili: Nani na vipi atahuisha na kusukuma mbele mapambano ya kuiendeleza ajenda ya umajumui wa Kiafrika?
Mwandishi wa Makala haya DK. NG’WANZA KAMATA ni Mhadhiri Mwandamizi, Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Imechapishwa pia katika Kitabu cha Uanazuoni wa Mwalimu Nyerere, kilichozinduliwa mwezi jana na Kavazi la Mwalimu Nyerere.
NYERERE mtazamo wake ulikuwa na faida na hasara vilevle.... NKRUMAH endapo mtazamo wake ungezingatiwa yawezekana tatizo lingekuwa kubwa zaidi.... NAJARIBU KUANGALIA JINSI AMBAVYO RAIS ANGEKUWA ANAPATIKANA KWA MTAZAMO WA KWAME NKRUMAH...
ReplyDelete