Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), kupitia Kampuni ya mawakala wa nyumba wametoa siku 14 kwa uongozi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), kulipa malimbikizo ya kodi ya Sh. bilioni 3.6.
Imedaiwa kuwa malimbikizo hayo ni kutokana na kodi wanazotakiwa kulipa kuanzia Agosti 2012 hadi Septemba 2015 kwa kodi ya Sh. 73,000,000 kwa mwezi tangu ulipomalizika mkataba wa awali Agosti 2011.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, ilieleza kuwa deni hilo limefika kiasi hicho kutokana na kiasi cha Sh. bilioni moja ambacho kilikuwa hakijalipwa katika deni la awali kipindi cha Septemba 2011 hadi Agosti 2012.
Ilieleza kuwa iwapo uongozi wa IMTU utashindwa kufanya malipo ndani ya siku hizo, hatua kali zitachukuliwa, ikiwamo kutolewa kwa nguvu na mali zao kuchukuliwa ili kufidia gharama hizo.Taarifa hiyo ilieleza kuwa mkataba wa awali kati ya IMTU na NDC ulimalizika Agosti 2011 na baada ya hapo, uongozi huo haujawahi kulipa, hivyo kusababisha deni hilo.
Imeelezwa kuwa IMTU iliingia mkataba wa kwanza na NDC mwaka 1996 kwa makubaliano ya kulipa Sh.100 kwa mwezi, hivyo mkataba huo ulioendelea kwa muda wa miaka 15.
“NDC ni taasisi ya serikali hivyo inapaswa kulipwa madeni yake ili kiasi hicho kitumike kwa ajili ya huduma zingine,” ilisema taarifa hiyo.
Meneja Utawala wa IMTU, Mateus Diniz, alipoulizwa alisema hana taarifa na kuhitaji kupewa muda kwa ajili ya kufanya malipo na kwamba atalifuatilia ili kujua madai yanahusu nini.
”Nimeshtushwa na taarifa hizo kuwa tunadaiwa, lakini subiri nifuatilie na kesho saa nne asubuhi nitakuwa na majibu ya madai yaliyolalamikiwa kwani kwa sasa sina majibu mazuri,” alisema.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Donan Mmbando, alisema hawezi kuzungumza chochote kuhusu suala hilo.
“Nipo kwenye kikao ila nakushauri tembelea eneo husika ili kupata majibu,” alisema.
Meneja Habari na Uhusiano wa NDC, Abel Ngapemba, alisema kiasi hicho kilichotajwa hapo juu ni kidogo, hasa kutokana na malimbikizo ambayo wamegoma kulipa kwa muda mrefu.
Alisema haiwezekani majengo ya serikali yatumiwe na mtu binafsi bila kulipa kodi.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment