Mkurugenzi wa Elimu kwa Walipakodi wa TRA, Richard Kayombo
Dar es Salaam. Wakati Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikivunja rekodi kwa kukusanya kiasi kikubwa cha mapato mwezi huu ikilinganishwa na mingine iliyopita, wachumi nchini wametaja mambo manne yanayotakiwa kufanywa na Serikali ili kukusanya mapato mengi zaidi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wachumi hao waliyataja mambo hayo kuwa ni kufikiwa kwa vyanzo vyote vya mapato, kuziba mianya ya ukwepaji kodi, kuboreshwa huduma za jamii na kuwa na vyanzo vingi vya mapato.
Kauli ya wasomi hao imekuja siku moja tangu Rais John Magufuli kumpongeza Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Philip Mpango kwa kukusanya Sh1.3 trilioni, kiwango ambacho kimeelezwa kuwa ni rekodi kwa mamlaka hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu za TRA, Agosti mwaka huu ilikusanya Sh890.5 bilioni, Septemba Sh1 trilioni na Oktoba Sh970 bilioni.
Juni mwaka huu wakati akiwasilisha makadirio ya mapato ya Serikali kwa mwaka 2015/16, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alisema hadi Aprili, mapato ya kodi yalifikia Sh8.1 trilioni sawa na asilimia 72 ya makadirio ya mwaka ya Sh11.3 trilioni.
Ukusanyaji huo wa mapato umeongezeka kwa kasi baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani, jambo ambalo wachumi walisema kuwa linatokana na umakini wa ukusanyaji ulioanza kuonyeshwa na maofisa wa mamlaka hiyo. Jana, Mkurugenzi wa Elimu kwa Walipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema mamlaka hiyo iko bega kwa bega na Rais Magufuli kuhakikisha inakusanya mapato ipasavyo ili kufikia lengo la kukusanya Sh12.3 trilioni ifikapo Juni mwakani.
Wadau wazungumza
Mhadhiri Mwandamizi Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Jehovaness Aikaeli alisema: “Ni lazima TRA ifikie vyanzo vyote vya mapato vilivyoainishwa... Ukishaweza kufika katika vyanzo vyote vya mapato ni lazima uanze kubana mianya ya ukwepaji kodi. Unaweza kuwa na utaratibu mzuri wa ukusanyaji kodi, ila kama huwezi kuziba ukwepaji wa ulipaji kodi ni kazi bure, hutapata kitu, ” alisema na kuongeza kuwa:
“Ili kuwafanya wananchi walipe kodi ipasavyo ni lazima Serikali ihakikishe kodi wanayolipa inatumika kuboresha huduma za jamii.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (Repoa), Profesa Samuel Wangwe alisema: “Ukitaka kukusanya kodi ipasavyo ni lazima uhakikishe hakuna anayekwepa kulipa kodi. Jambo jingine muhimu ni kupanua wigo wa ukusanyaji wa kodi kwa maana na kuwa na vyanzo vingi vya kodi. Hili ni jambo muhimu, ” alisema Wangwe.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Omary Mbura alisema: “Upotevu wa mapato hutokana na uzembe na tabia za makusudi. Binafsi naamini katika kuziba mianya ya ukwepaji kodi. Sehemu hii ikifanyiwa kazi tutapata mapato mengi.” Dk Mbura alisema vyanzo vya kodi vinapaswa kuwa vingi na kutoa mfano wa kodi katika nyumba za kupanga. “Eneo hili linaweza kuipatia Serikali mapato mengi, ” alisema.
No comments :
Post a Comment