Mwanasheria Mkuu mstaafu, Jaji Mark Bomani
Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu mstaafu, Jaji Mark Bomani ametaka Serikali kuendeleza mchakato wa kupata Katiba Mpya ulioanzishwa na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2012.
Akizungumza jana na waandishi wa habari, Jaji Bomani alisema dalili zinazoonyesha kwamba jitihada ya kupata Katiba Mpya zimegonga mwamba.
Wakati Jaji Bomani akisema hayo, Rais John Magufuli wakati akizindua Bunge la 11 aliahidi kuendeleza mchakato ulioanzishwa, ili Tanzania iweze kupata Katiba Mpya.
Alisema kazi iliyofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Bunge, inatoa msingi mzuri wa mwendelezo wa mchakato huo na kwamba kazi iliyobaki ni ndogo.
Jaji Bomani alisema wanachojiuliza Watanzania hivi sasa ni lini watakuwa na Katiba Mpya.
“Nashauri kwamba mara baada ya kupatikana kwa Serikali ya Zanzibar baada ya marudio ya uchaguzi,
Serikali mbili zifanye mazungumzo ili kuhitimisha mchakato huo,” alisema. Alisema mambo ya kuzingatia katika mchakato huo, ni kuendelea kutumia rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba yenye maoni ya wananchi.
“Tume ya Warioba iliteuliwa na rais ikazunguka nchi nzima ikakusanya maoni ya wananchi ni lazima tuzingatie maoni yao,” alisema.
Alisema katika mchakato huo, maoni ya tume na ya Bunge Maalumu la Katiba yakiunganishwa Tanzania itapata Katiba bora, kwa sababu kuna watu wengi wenye uwezo wa kazi hiyo.
Mchakato wa Katiba Mpya ulifikia katika hatua ya Katiba inayopendekezwa, na sasa kinachosubiriwa kupiga kura ya maoni.
No comments :
Post a Comment