Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Morogoro. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameiagiza Mamlaka ya Bodi ya Bonde la Mto Rufiji (Rubada), kuwafungia maji wakulima wenye mashamba makubwa ya umwagiliaji wilayani Mbarali, Mkoa wa Mbeya ili yaelekezwe kwenye mabwawa ya umeme.
Agizo hilo linafuatia baada ya kupewa taarifa na Meneja wa Kituo cha Uzalishaji wa Umeme cha Kidatu, Justus Mtorela juu kupungua uzalishaji kwa megawati 50 kutoka megawati 200 za kawaida.
“Nataka hili lifanyike ndani ya wiki moja. Nendeni mkawaeleze wakulima kuwa sasa hivi ni kipindi cha masika, hivyo maji hayo lazima yaende kwenye mabwawa ili uzalishaji umeme uongezeke. Sitaki kusikia habari za ukame kwenye mabwawa. Nataka suala hili lizingatiwe,” alisema.
Alisisitiza kuwa endapo maji hayo yatazuiwa kwenda katika mashamba hayo, mabwawa ya Mtera na Kidatu yatapata maji ambayo yatasaidia kuzalisha umeme na kuongeza idadi ya megawati katika gridi ya Taifa.
“Tukisema tusubiri hadi mvua inyeshe ili mabwawa yajaye, tutakaa hata miaka 100 lazima tutumie njia hii ili tuzalishe umeme kwa ufanisi,” alisema.
Pia, aliishauri Tanesco kuacha kufanya kazi kizamani kwa kusubiri mvua inyeshe ili mabwawa yajaye ndipo wazalishe umeme, badala yake watumie mbinu mpya na za kisasa, ikiwamo kuongea na wahusika ili kufunga mashamba hayo hususan katika kipindi hiki cha masika.
Meneja wa Tanesco wa Nyanda za Juu Kusini, Salome Mkondola na Kaimu Ofisa wa Rubada, David Mginya kwa pamoja waliahidi kutekeleza agizo hilo, linalotakiwa kufanyiwa kazi kuanzia Jumatatu ijayo baada ya vikao vya pande hizo mbili kufanyika.
No comments :
Post a Comment