Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, December 13, 2015

Kiapo cha jasho, mawaziri wapania kazi



By Fidelis Butahe na Nuzulack Dausen, Mwananchi
Dar es Salaam. Hafla ya kuapishwa kwa mawaziri iliyofanyika jana Ikulu jijini Dar es Salaam ilikuwa kavu isiyo na shangwe zilizozoeleka huku mawaziri wakionekana wazi kuwa wamepania kufanyia kazi kiapo chao.
Hafla hiyo ilifanyika bila ya kuwapo na viburudisho vya kifahari na shamrashamra nyingine, lakini hilo halikuonekana kuwasumbua mawaziri hao ambao uteuzi wao ulitangazwa juzi, na badala yake wakaeleza jinsi walivyojipanga kutekeleza majukumu yao kwa kasi ya “hapa kazi tu”.
Baadhi ya mawaziri walianza kazi moja kwa moja baada ya kutoka Ikulu, akiwamo Dk Hamisi Kigwangalla ambaye alikwenda moja kwa moja Hospitali ya Amana iliyopo wilayani Ilala na kufanya kikao kifupi na madaktari na uongozi wa hospitali hiyo.
“Nitahakikisha kila Mtanzania anapata huduma nzuri ya afya. Hilo litafikiwa kama tutakuwa na zahanati kila kijiji, dawa za kutosha, vifaa tiba na watumishi sekta ya afya wapate motisha ya kufanya kazi,” alisema Dk Kigwangalla ambaye ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mara baada ya kuapishwa.
Waziri Mhagama anena
Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama alielekeza akili yake katika kutekeleza majukumu yake vizuri.
“Hakuna kingine zaidi ya kufanya kazi tu,” alisema Mhagama. “Nitafanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa, nikiongozwa na uzalendo.”
Waziri huyo, ambaye aliambatana na mwanae, alisema kazi kubwa atakayoifanya ni kulifanya Bunge kuwa la wananchi, kuwaunganisha wafanyakazi, vijana na sekta zote zinazosimamiwa na wizara hiyo.
Awali Mhagama alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Sera, Uratibu na Bunge). Wizara hiyo ilikatwa na kuunganishwa na wizara nyingine mbili.
Alipoulizwa sababu za kurejeshwa tena katika wizara hiyo alisema: “Nimerudishwa sababu nikiwa bungeni nilipunguza tofauti za vyama na kuwatumikia zaidi wananchi. Pia nilikuwa kiunganishi kizuri sana.”

Kilimo na Uvuvi ni maisha ya Watz
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Fedha (Sera) katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne, alisema Rais ametoa dira na hivyo jukumu lake ni kuifuata.
“Kilimo, mifugo na uvuvi ndiyo maisha ya Watanzania na tayari rais ametoa dira ya jinsi ya kuelekea katika mambo hayo. Jukumu nililonalo ni kufuata dira hiyo kuhakikisha wakulima, wavuvi na wafugaji wanakuwa katika mazingira rafiki na kubadili maisha yao,” alisema Nchemba ambaye pia aliomba ridhaa ya CCM kugombea urais.
Kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji, Mwigulu alisema atakalolifanya ni kushirikiana na wizara nyingine ambazo zina uhusiano wa moja kwa moja na matumizi bora ya ardhi.
Mwigulu ambaye aligusia sana suala la kilimo na uvuvi wakati akisaka tiketi ya kupitishwa na CCM kuwania urais, alisema: “Pembejeo za kilimo zinatakiwa kufika kwa wakati, wakulima wasikopwe mazao yao na wapate soko la mazao. Hayo ni mambo niliyoyagusia sana na nitayasimamia.”

Simbachawene atangaza vita
Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala, George Simbachawene alisema katika uongozi wake hataki kuona wakuu wa wilaya, mikoa na wakurugenzi wakikaa ofisini, na kuwataka kwenda kusikiliza matatizo ya wananchi na kuyatatua.
“Watakaoshindwa kwenda na kazi nitakayoanza nayo, ninawapa pole na wajiandae kutupisha. Ninakerwa kuona watoto wanakaa chini. Tuna miti na misitu ya kutosha, kwa nini watoto wakae chini? Kuanzia mwezi wa sita mwakani, sitaki kuona mtoto anakaa chini. Nawapa miezi sita tu,” alisema
“Watu hawa (wakuu wa wilaya, mikoa na wakurugenzi) wakitekeleza wajibu wao vizuri, matarajio ya Watanzania katika afya, elimu na kilimo yatatimia. Wakuu wa wilaya na mikoa kazi yao si kupokea wageni ni kwenda kuwatumikia wananchi,” alisema.

Nape na sheria za michezo, habari
Nape Nnauye, ambaye ataongoza Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo aliangalia changamoto kwenye sekta zilizo chini yake.
“Sitamuangusha aliyeniamini, walioniamini na Watanzania wote. Katika michezo changamoto ni nyingi, lakini kubwa mbili ni sheria zinazosimamia michezo na nidhamu katika michezo,” alisema.
Alisema masuala hayo yanakwamisha michezo kwa kiasi kikubwa na kutaka ushirikiano na wadau wote wa sekta hiyo.
Nape pia alizungumzia sheria kandamizi kwenye sekta ya habari akisema ataangalia jinsi ya kuzishughulikia ili waandishi waweze kufanya kazi zao kwa uhuru zaidi na kumaliza malalamiko na changamoto mbalimbali.

Dk Possy afurahia kitengo cha walemavu
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wenye Ulemavu, Dk Possy Abdallah alisema kuwa ni jambo la kheri kwa Rais Dk Magufuli kuamua kuweka kitengo kitakachosimamia masilahi ya watu wenye ulemavu na kwamba atafanya kazi kwa kasi licha ya kuwepo changamoto mbele yake.
Dk Possy, ambaye ni mlemavu wa ngozi, alisema mara nyingi masuala ya walemavu yalikuwa yakichukuliwa kiujumla kwa ama kuchanganywa katika idara za maendeleo ya jamii au ustawi wa jamii na kuonekana hayana uzito.
Alisema changamoto zinazowakabili walemavu si nyepesi, hivyo lazima wafanye kazi kwa bidii ili kuhakikisha usawa wa kweli unapatikana kwa kutekeleza Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010.
“Lakini utekelezaji wake mzuri utahitaji ufanyaji kazi wa sheria nyingine, masuala ya elimu, ajira, afya, hifadhi ya jamii na mengineyo. Tutabadilisha mtazamo juu ya walemavu na ukusanyaji wa mapato,” alisema Dk Abdallah.

Mwalimu kusaka fedha za dawa
Wakati mawaziri wengine wakizungumzia jinsi ya kutatua changamoto hizo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto, Ummy Mwalimu alisema jambo la kwanza ofisini ni kuhakikisha wanapata fedha za kutosha ili kutatua matatizo hayo, ambayo ni pamoja na upungufu wa dawa, wauguzi, madaktari na wataalamu wengine wa sekta hiyo.
Alisema pia watahakikisha wanaongeza ujuzi wa watumishi wote ili wafanye kazi kwa ufanisi huku wakiwashirikisha zaidi wananchi katika kuboresha sekta hiyo.

Profesa Mbarawa ataka ushirikiano
Akiwa anakabiliwa na kilio kikubwa cha maji, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa alisema ili kutatua matatizo hayo ushirikiano na wadau wote ni muhimu ili kufanikisha azma ya usambazaji wa huduma hiyo vijijini na kusadia kukusanya mapato ya kutosha.
Kilio cha maji kilitawala mikutano ya wagombea urais wote wakati wa kampeni na wagombea wote waliahidi kulitatua iwapo wangepewa ridhaa ya kuongoza.
“Tushirikiane kwa pamoja kuhakikisha tunatatua tatizo la maji na wale wenye tabia ya kukatakata na kuiba maji waache tabia hiyo mara moja,” alisema Profesa Mbarawa.
“Tukifanya hivyo tutapata mapato mazuri na tutaweza kujenga miundombinu ya kisasa ya kusambaza maji na kuzuia yasipotee.”

Lukuvi aonya matajiri wanaopora ardhi
Naye waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William
Lukuvi alisema atafanya kazi kwa ufanisi na kwa kasi zaidi huku akiwatumia salamu vigogo wenye tabia ya kuwanyang’anya ardhi wananchi masikini na wale wanaokwepa kodi ya ardhi kuwa atakabiliana nao.
“Hawa watu ambao wanavunja sheria mbalimbali za ardhi kwa kujenga kwenye fukwe, sehemu za wazi, mahali pa watu wote wajiandae kutoka tu, wasisubiri nguvu zangu maana yake safari hii nina nguvu zaidi,” alisema Lukuvi.
Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Ajira na Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angella Kairuki alisema atafanya kazi kwa kasi ya hali ya juu akizingatia utawala bora na maadili, kuboresha nidhamu na kuangalia mifumo ambayo bado haijaboreshwa ili ifanye kazi kwa ufanisi na kwenda na kauli mbiu ya “hapa kazi tu”.

Muhongo, Mwakyembe wazungumza
Mawaziri wawili ambao wamepingwa uteuzi wao kutokana na tuhuma zilizoikumba Serikali ya Awamu ya Nne, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye ni Waziri wa Nishati na Madini, na Dk Harrison Mwakyembe hawakutaka kujikita kujibu mashambulizi dhidi yao.
Profesa Muhongo, ambaye alilazimika kujiuzulu uwaziri wa Nishati na Madini wakati wa kashfa ya escrow takriban mwaka mmja uliopita lakini baadaye akasafishwa na Sekretarieti ya Baraza la Maadili ya Utumishi wa Umma, alirusha swali kuhusu sakata hilo kwa wale wanaomtuhumu.
“Kawaulize hao wanaopinga,” alisema alipotakiwa kueleza anazungumziaje msimamo wa wanasiasa wa upinzani wanaopinga uteuzi wake.
Na hata alipoulizwa anafikiri ni sababu zipi zilizomfanya arejeshwe, alisema: “Kawaulize wanaohoji.”
Lakini akajikita zaidi kuzungumzia majukumu yake akisema ataanza kufanya kazi pale alipoishia.
“Kama tunataka kuondoka katika umasikini ni lazima tuwe na umeme wa uhakika na usio katika katika. Tukitaka nchi yetu iwe na kipato cha kati lazima tuzalishe umeme wa Megawati 10,000 hadi 15,000. Ukiwa na umeme huu nchi itazalisha ajira, bidhaa zitashuka bei na hata bei ya umeme itapungua,” alisema.
Naye Dk Mwakyembe hakutaka kuzungumzia kabisa tuhuma za wapinzani dhidi ya sakata la ununuzi wa mabehewa na badala yake akasema apewe muda ili kupitia masuala mbalimbali kujua sehemu zenye changamoto, huku akisisitiza kuwa kwa kasi aliyoanza nayo Rais Magufuli ni lazima wizara hiyo ijipange na kuwa chachu ya maendeleo ya nchi.

No comments :

Post a Comment