Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea na Mkuu wa Wialya ya Kinondoni, Paul Makonda, jana nusura wazichape kavu kavu mbele ya wafanyakazi wa Kiwanda cha Kutengeneza Nguo cha Tooku Tanzania Garment walipokutana kwa lengo la kutatua mgomo wa wafanyakazi hao ulioanza jana asubuhi.
Hali hiyo ilitokea baada ya Makonda kuzungumza na wafanyakazi hao na kufunga mkutano bila kumruhusu Kubenea kuzungumza na wafanyakazi hao.
Baada ya Makonda kumaliza kuzungumza na wafanyakazi hao, aliwaamuru watawanyike, lakini kabla hawajaondoka, Kubenea aliomba azungumze nao.
Hata hivyo, Makonda alimkataza Kubenea kuzungumza na wafanyakazi hao kwa maelezo kwamba tayari amekwisha kufunga mkutano hivyo hamruhusu kuzungumza kwani yeye ndiye aliyekuwa mzungumzaji wa mwisho.
Kauli ya Makonda ilizua mabishano makali na Kubenea huku akiwataka wafanyakazi hao watulie na kwa upande wmingine Maonda naye akisisitiza asizungumze chochote.
Hali hiyo iliwafanya Polisi waliokuwapo eneo hilo na baadhi ya viongozi wa kiwanda hicho, kuingilia kati kusuluhisha mzozo huo kwa kumshika mikono Kubenea ambaye alionekana dhahiri kuwa na hasira kali."Huwezi kufunga mkutano nisiongee na wafanyakazi na wapiga kura wangu. Nimekuja hapa tangu asubuhi nimepambana mpaka tukafikia hapa na niliwaahidi nikitoka kwenye kikao cha menejimenti nitawapa `briefing.' Inakuwaje wewe umekuja sasa hivi unazungumza na kufunga mkutano kwa ubabe?," Alihoji Kubenea.
Hata hivyo, Makonda aliendelea na msimamo wake kwamba tayari amefunga mkutano na haruhusu mtu mwingine kuzungumza.
" Nafahamu kwamba hawa ni wapigakura wangu na ndiyo maana nikaja tangu asubuhi kupambana ili wapate haki yao, nimekuja hapa nikawa nazuiliwa kuongea na uongozi, sasa hapa nimefanikiwa kuongea na uongozi kufahamu nini kinaendelea hata hujafahamu kilichojiri kwenye kikao unafanya ubabe. Niache niwaambie kilichotokea kwenye kikao," alisisitiza Kubenea.
Aliongeza: "Mimi hawa wamenipigia kura, wewe umepata kura ngapi?. Huwezi kunifanya lolote wewe," alisisitiza Kubenea.
Baadaye, Makonda aliwaamuru polisi wamkamate Kubenea pamoja na kuagiza kunyang'anywa kamera ya mpigapicha wa kituo cha Star Tv iliyotumika kuchukua tukio hilo.
Polisi walimtaka Kubenea apande gari lao, lakini kulitokea mabishano makali kutokana na Kubenea kukataa kupanda gari la polisi.
Baada ya mabishanao hayo, polisi walikubali Kubenea atumie gari lake na kuongozana na askari hao hadi Kituo cha Polisi Magomeni.
Kubebea alifika katika eneo hilo la kiwanda saa 6:30 mchana kusikiliza kero za wafanyakazi hao baada ya kupata taarifa za kuwapo kwa mgomo.
Alipofika, alipokelewa na kundi la wafanyakazi hao zaidi ya 1,000 na mojawapo ya malalamiko yao yalikuwa nyongeza ya mshahara ambayo walisema walikuwa wakidai kwa kipindi kirefu.
Baada ya kusikiliza, alitaka kuonana na uongozi wa kiwanda, lakini alipotaka kuingia, alizuiwa mlangoni.
Kubenea alilazimika kwenda hadi kwa uongozi wa Epza waliompangisha mmiliki wa kiwanda hicho na kumsaidia kukutana uongozi wa kiwanda na kuzunguza nao.
Kabla kukutana na menejimenti ya kiwanda hicho, Kubenea alikuwa amewaahidi wafanyakazi kuwa atawapa taarifa ya kilichojiri katika kikao hicho.
Hata hivyo, kabla ya kumalizika kwa kikao hicho saa 8:30 mchana, Makonda alifika eneo hilo la kiwanda.
Hadi inafika saa 12:00 jioni, Kubenea alikuwa katika Kituo cha Polisi Magomeni na Mwanasheria wake, Frederick Kihwelo, alifika hapo kushughulikia dhamana yake.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment