Akisoma shtaka hilo jana, Wakili Mkuu wa Serikali, Timon Vitalis, alisema Kubenea anakabiliwa na kosa la kutumia lugha ya matusi ambalo ni kwa mujibu wa sura ya 89(1)a cha kanuni za adhabu toleo namba 6 la mwaka 2000.
Alisema akiwa katika eneo la Kiwanda cha Tooku Garmet Tanzania, Desemba 14, mwaka huu, Kubenea alitumia lugha ya matusi kwa kumwita Makonda kibaka, pumbavu, mjinga na kwamba cheo alichonacho amepewa na mtu mmoja.
Katika shtaka hilo, Kubenea ambaye anatetewa na jopo la mawakili sita kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakiongozwa na Peter Kibatala, alikana shtaka hilo.
Mawakili wengine wanaomtetea Kubenea ni Dk. Rugemeleza Nshala, Nyoronyo Kicheere, Frederick Kihwelo, Jeremia Mtobesya na Omari Msemwa.Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Thomas Simba, alisema Dhamana ya Kubenea iko wazi, hivyo kuruhusu dhanama ya watu wawili wanaotambulika na serikali na kila mdhamini alitakiwa kusaini bondi ya Sh. 500,000.
Waliojitokeza kumdhamini ni Mbunge wa Kinondoni kupitia Chama cha Wananchi(CUF), Maulid Mtulia na Anatropia Theonest ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), hivyo akaruhusiwa kuwa nje kwa dhamana.
Aidha, hakimu alisema kesi hiyo itaanza kusikilizwa kwa mara ya kwanza Desemba 29, mwaka huu, baada ya kukamilika kwa uchunguzi.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment