Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, December 14, 2015

Magufuli apasua majipu Kikwete akipasua anga REKODI: Wakati Kikwete akisafiri kwenda mataifa mbalimbali tangu astaafu ikiwamo Uingereza, Magufuli hajakwea pipa hata mara moja kwenda ughaibuni tangu aapishwe.

Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, akizungumza na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, walipokutana kwenye Mkutano wa Tano wa China na Nchi za Afrika jijini Johannesburg, Afrika Kusini wiki iliyopita.

Wakati Rais John Magufuli, akitumia siku zote 38 za kuwa kwake madarakani hadi kufikia jana kwa kusimamia kampeni yake ya kuongeza mapato ya serikali na kukomesha vitendo vya ufisadi kupitia kile anachokiita ‘kupasua majipu’, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, anaendelea kupasua anga baada ya kuzifikia nchi nne tangu kuachia madaraka. 
Hata hivyo, wakati Kikwete akiendelea kusafiri kutokana na majukumu mbalimbali yanayomkabili akiwa Rais mstaafu, Rais Magufuli ameendeleza rekodi yake ya kutosafiri kwenda nje ya nchi tangu aingie Ikulu. 
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa tayari alishakwea ‘pipa’ na kuzifikia nchi za Ethiopia, Uingereza, Visiwa vya Comoro na pia Afrika Kusini, huku baadhi ya safari hizo zikitokana na mialiko maalum anayopewa.
Mara baada ya kuingia madarakani Novemba 5, mwaka huu kufuatia ushindi wake wa asilimia 58.46 katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, Rais Magufuli alitangaza hatua kadhaa za kubana matumizi yasiyo ya lazima kwa serikali na pia kuwabana wakwepa kodi ili hatimaye kuinua mapato na mwishowe kunufaisha Watanzania kwa kuwaondolea kero mbalimbali zitokanazo na huduma za jamii.
Hadi sasa, tayari Rais Magufuli ameshachukua maamuzi kadhaa makubwa yaliyookoa mabilioni ya fedha na pia kuongeza nidhamu ya kazi katika ofisi za umma. 
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Rais Magufuli ni pamoja na tangazo lake la kudhibiti safari holela za nje ya nchi kwa viongozi wa Serikali ambazo sasa ni lazima zipate kibali chake au cha Katibu Mkuu Kiongozi wa Ikulu. 

Pia ameshafuta matumizi ya fedha za serikali kwa ajili ya maadhimisho ya siku mbalimbali za kitaifa ikiwamo ya Ukimwi ambazo huigharimu serikali mabilioni ya fedha. 

Kadhalika, mwendelezo wa utumbuaji majipu wa serikali ya Rais Magufuli umewezesha kufichua ukwepaji kodi kupitia uondoaji mizigo bandarini uliokuwa ukilikosesha taifa takriban bilioni 600, zaidi ikiwa ni kutokana na kontena 2,431 yaliyopitishwa kinyemela bila kulipiwa kodi. 

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kodi Tanzania (Rished Bade) amesimamishwa kazi kutokana na kashfa ya kontena, kama ilivyo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Awadh Massawe, ambaye pia uteuzi wake umetenguliwa, kuvunjwa kwa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA na pia maafisa takriban 50 wa mamlaka hizo wakifikishwa mahakamani kutokana na tuhuma zinazohusiana na ukwepaji kodi huo.
SAFARI ZA MAGUFULI
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa tangu alipoingia Ikulu Novemba 5, Rais Magufuli hajawahi kupanda ndege ili kwenda safari yoyote na ameonekana akitumia muda mwingi kuandaa mazingira ya utekelezaji wa ahadi zake mbalimbali alizozitoa kwa Watanzania wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.
Rekodi zinaonyesha kuwa katika kile kinachoonekana kuwa ni kuonyesha njia juu ya namna ya kutekeleza dhamira yake ya kudhibiti safari holela za nje, Rais Magufuli hajasafiri kwenda ughaibuni walau kwa gia ya kujitambulisha kwenye jumuiya ya kimataifa kama ilivyozoeleka kwa marais wengi mara tu waingiapo madarakani .
Magufuli alisafiri kwa gari kutokea Ikulu jijini Dar es Salaam hadi katika Ikulu Ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma, Novemba 17, 2015.  Alikaa Dodoma kwa zaidi ya wiki moja na kutimiza jukumu lake la kutangaza jina la Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), kumuapisha (Waziri Mkuu) na kisha kuzindua Bunge.
Mara baada ya kulihutubia Bunge Ijumaa, Novemba 20, Rais Magufuli alirudi Ikulu jijini Dar es Salaam Novemba 26, ambako alijichimbia na kuendeleza kasi yake ya ‘kutumbua majipu’. Alhamisi ya wiki iliyopita, akiwa Ikulu jijini Dar, Magufuli alitangaza baraza lake la mawaziri lililojumuisha mawaziri na naibu mawaziri 30, huku nafasi za mawaziri wanne akiziacha wazi kutokana na kile alichodai mwenyewe kuwa ni kuendelea kutafuta watu wenye sifa ya kuziongoza. Wizara hizo ni Fedha na Mipango; Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano; Maliasili na Utalii na pia Wizara ya Elimu, Teknolojia na Ufundi
Aidha, inakumbukwa kuwa wakati akilihutubia Bunge, Magufuli alisema safari holela za nje huligharimu taifa mabilioni ya fedha ambazo zingeweza kutumiwa kwa shughuli nyingine za maendeleo. Alitoa mfano wa safari za nje zilizogharimiwa na serikali katika mwaka wa fedha 2013/2014 na 2014/2015 ambazo ni Sh. bilioni 356, huku Sh. bilioni 104 kati ya hizo zikiteketea kwa posho za safari hizo kwa viongozi na maafisa wengine wa juu wa serikali.
SAFARI ALIZOJINYIMA MAGUFULI 
Pengine katika kutekeleza agizo alilolitoa la kudhibiti safari za nje, Rais Magufuli hakujihusisha na safari ya kwenda kwenye mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Madola (CHOGM), uliofanyika visiwa vya Malta  Novemba 27, 2015.
Badala yake, Magufuli alimtuma Balozi wa Tanzania nchini Uingereza kwenda kumuwakilisha katika mkutano huo, akiwa pamoja na maofisa wengine watatu na hivyo jumla yao kuwa watu wanne. 

Inaelezwa kuwa wakati wa utawala wa awamu ya nne, msafara kwenye mkutano kama huo uliofanyika Malta ulikuwa ukimhusisha Rais, baadhi ya mawaziri na maafisa wengine wa juu serikalini ambao kwa ujumla walikuwa takriban 50. 
Novemba 29, Magufuli alitakiwa kuwapo jijini Paris, Ufaransa katika mkutano wa kimataifa wa 21 kujadili mabadiliko ya tabia nchi duniani (COP21) ambapo wakuu wa nchi takriban 150 kutoka katika nchi 195 walishiriki, wakiwamo marais Barack Obama wa Marekani na Xi Jinping wa China. Hata hivyo, Magufuli hakukwea ndege kwenda kuhudhuria mkutano huo na badala yake akabaki nyumbani akiendelea kushughulikia ‘upasuaji majipu’ , hasa TPA na TRA.

Desemba 5, 2015, Rais Magufuli hakupanda ndege pia kwenda Johannesburg, Afrika Kusini kulikokuwa na mkutano wa tano wa wakuu wa nchi za Afika na Rais wa China, Xi Jinping, kupitia Jukwaa la Nchi za Afrika na China (FOCAC). Katika mkutano huo, Rais Magufuli aliwakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan. 
SAFARI ZA KIKWETE
Siku moja baada ya kushuhudia mrithi wake akiapishwa, (Novemba 6, 2015), Rais mstaafu Kikwete alisafiri kwa ‘chopa’ kutoka Dar es Salaam kwenda kijijini kwake Msoga, jimbo la Chalinze Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Siku chache baadaye, Kikwete alikuwa jijini Addis Ababa, Ethiopia ambako aliwahi kuripotiwa Novemba 26, 2015 akiipongeza timu ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) iliyokuwa imetinga robo fainali ya Kombe la Chalenji.
Novemba 30, Kikwete alikwenda Moroni, Comoro baada ya kuteuliwa kuwa mmoja wa wajumbe wa Umoja wa Afrika (AU) kwenda kuhudhuria mkutano ulioangalia namna ya kukabili dalili za mgogoro wa kisiasa visiwani humo kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Aprili, 2016.
Baadaye Kikwete alikwenda jijini London, Uingereza ambako alihudhuria mkutano Mkuu wa 20 wa Taasisi ya Ushirikiano wa Usimamizi wa Sayansi na Teknolojia kwa nchi za Jumuiya ya Madola (CPTM) na kutunukiwa tuzo maalum kwa kutambua mchango wake katika ukuaji wa matumizi ya Sayansi na Teknolojia, ikiwamo matumzi ya simu katika utoaji wa huduma za fedha. Alitunukiwa tuzo hiyo Desemba 1, 2015.
Kadhalika, Kikwete alikwenda jijini Johannesburg, Afrika Kusini, kama mualikwa, kuhudhuria Mkutano wa Tano FOCAC uliofanyika Desemba 4, 2015. Mkutano huo ulikuwa na lengo la kudumisha maendeleo ya pamoja kati ya nchi za Afrika na China, kuibua maeneo ya maendeleo yakiwamo ya miundombinu na kuimarisha fursa za kibiashara.
Siku ya Uhuru, (Desemba 9, 2015), Kikwete alionekana akiwa na wananchi wenzake wa Chalinze, wakishiriki kufanya usafi ili kuunga mkono maelekezo ya Rais Magufuli ambaye aliwataka Watanzania kusherehekea siku hiyo kwa kufanya usafi kwenye maeneo yao ili kukabiliana na magonjwa kama kipindupindu.
WASOMI WANENA 
Akizungumzia hatua ya Rais Magufuli kutowahi kwenda nje ya nchi hadi sasa, Profesa Chriss Maina wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema Rais (Magufuli) anatatua kero alizizoziona kwa wananchi wakati akiwa katika kampeni za uchaguzi mkuu na hivyo, anaamini hiyo ndiyo sababu ya kutumia muda wake wote hadi sasa akiwa nchini na kwamba, hilo ni jambo jema.
Alisema kadri aonavyo, Rais Magufuli amejipanga vizuri katika kutatua mambo ambayo yalikuwa ni kero kubwa kwa wananchi likiwamo suala la ufisadi katika mashirika ya umma.
Aliongeza kuwa anachokifanya sasa Rais Magufuli ni sawa na mtu aliyehamia nyumba yake mpya, hivyo hawezi kuanza kusafiri pasipo kusafisha nyumba hiyo na kujiridhisha kuwa iko katika hali nzuri.
Mkuregenzi Mtendaji wa Asasi ya Concern For Development Initiatives in Afrika ( forDIA), Bubelwa Kaiza, alisema Rais Magufuli amechaguliwa na wananchi na hivyo anataka kuwatumikia na siyo kusafiri kila uchao.

Alisema kadri aonavyo, Rais Magufuli ameamua kutosafiri kwa sababu anaamini bado wananchi wake wana matatizo mengi na hivyo anahitaji kuyatatua kwanza ndipo aangalie uwezekano wa kusafiri ili kushughulikia masuala ya kimataifa.
Alisema nchi kwa sasa ina matatizo mengi, ikiwamo matumizi makubwa ya fedha katika wizara, ufisadi bandarini na Mamlaka ya Kodi (TRA) pamoja na baadhi ya viongozi kutokwenda sambamba na mfumo anaouhitaji yeye.
“ Rais Magufuli ameangalia hapa nchini na kuona kuna matatizo mengi … hivyo akaamua asisafiri hadi pale angalau atakapoyapunguza matatizo hayo. Hili ni jambo zuri na anastahili pongezi,” alisema Kaiza.
Aliongeza kuwa Rais mstaafu Kikwete ni mtu ambaye anasafiri sana kutokana na ukweli kuwa alitokea katika nafasi ya kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambayo ilimlazimu kusafiri mara kwa mara.

Aliyekuwa Katibu Mtendaji Baraza la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki, Profesa Mayunga Nkunya, alisema mambo anayoyafanya Rais Magufuli kwa sasa ni mfano wa kuigwa kwa kiongozi yoyote.
Alisema kwa mtazamo wake, anaamini Rais Magufuli anatakiwa kuhakikisha kuwa mabadiliko ameshayafanya ndani ya nchi kwa namna inayotakiwa na ndipo aanze kusafiri kwenda nje ya nchi.
Kuhusu safari za Rais mstaafu Kikwete, alisema ni vyema Watanzania wakasahau yaliyopita na kuangalia yajayo kwa manufaa ya taifa.
Septemba 15, 2015, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF) na NLD, alimlalamikia Rais Kikwete kwa kutumia muda mwingi wa kuwa madarakani akiwa safarini, huku akidai kuwa ametumia takriban Sh. trilioni 4.5 kugharimia safari katika miaka yake 10 ya kuwa madarakani. 
MBATIA, MEMBE
Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilimjibu Mbatia kwa kueleza kwa kifupi kuwa safari hizo za Kikwete (wakati huo akiwa Rais) zilikuwa na manufaa makubwa kwa taifa. 

Kadhalika, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliwahi kukaririwa akimpongeza Rais Magufuli kwa kuamua kudhibiti safari holela za nje ya nchi kwa kukiri kuwa wakati wao walikuwa wakipishana na ndege hewani utafikiri Tanzania ilikuwa ikiwaka moto.

CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment