Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, December 14, 2015

SMZ: Hakuna wa kuingilia uchaguzi wa marudio Zanzibar.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheir
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema uchaguzi mkuu wa marudio visiwani humo utafanyika  bila ya kuingiliwa na taasisi yoyote iwe ya kitaifa au kimataifa kwa sababu ni kinyume cha  Katiba na Sheria ya Uchaguzi Zanzibar.
 
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheir, alipokuwa akizungumza na wananchi walioathirika na vurugu za uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, huko Gomani, katika kisiwa cha Tumbatu, Zanzibar, mwishoni mwa wiki.
 
Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) ni chombo huru na ndicho pekee kinatakiwa kuratibu na kusimamia uchaguzi bila ya kuingiliwa na taasisi yoyote ya ndani wala nje ya nchi.
 
Alisema Zec imetangaza rasmi kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu na tamko hilo kuchapishwa katika Gazeti la Serikali la Novemba 6, mwaka huu kwa mujibu wa sheria.“Tume ya Uchaguzi itaratibu na kusimamia uchaguzi wa marudio bila ya kuingiliwa na taasisi yoyote iwe ya kitaifa au kimataifa kwa sababu ni kinyume cha  Katiba na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar,” alisema. 
 
Kheir aliwataka wananchi wa Kisiwa cha Tumbatu kujiandaa na uchaguzi wa marudio ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua Rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani kwa misingi ya demokrasia.
 
Aliwataka wananchi kudumisha amani na umoja wa kitaifa wakati huu wa kuelekea kufanyika kwa uchaguzi wa marudio visiwani humo.
 
“Zanzibar haiwezi kupiga hatua kubwa ya maendeleo bila ya kuwapo kwa mazingira ya amani na umoja wa kitaifa kwa wananchi wake. Nawapa  pole waathirika wa vurugu za uchaguzi waliochomewa nyumba zao moto kwa sababu za kisiasa. Haya ni mambo ya kulaaniwa na yasiyopaswa kufanywa na waliostaarabika,” alisema
 
Waziri huyo aliwakabidhi waathirika hao misaada mbalimbali ikiwamo, magodoro, vitanda, nguo, vyombo vya nyumbani, pamoja na fedha za kusadia gharama za ujenzi wa nyumba kwa familia saba zilizobomolewa katika vurugu zilizotokea katika mji mdogo wa Gomani, Kisiwani Tumbatu.
 
Aidha, alisema wananchi wanaosubiri mgombea urais wa Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad, aapishwe kuwa Rais wa Zanzibar kwa matokeo ya uchaguzi uliyofutwa wanapoteza muda na kujidaganya wenyewe.
 
“Watu wanaofanya kisomo na kuchoma ubani wakitia nia kuomba Mungu Maalim Seif awe Rais wa Zanzibar katika mitaa mbalimbali wanapoteza muda wao na kujidaganya kutokana na matokeo ya uchaguzi huo kuwa si halali na yamefutwa,” alisema.
 
Kheri alisema Mwenyekiti wa Zec alifuta matokeo hayo kwa kutumia  kifungu cha 119 (10) cha Katiba ya Zanzibar pamoja na Sheria ya Uchaguzi Zanzibar kifungu cha 3(1) na 5(a) vya Sheria namba 11 ya Uchaguzi ya Mwaka 1984 baada ya kubaini kufanyika udaganyifu mkubwa katika uchaguzi huo na kinachosubiriwa kwa sasa ni tume hiyo kutangaza tarehe ya kufanyika uchaguzi wa marudio.

CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment