Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
HAPA Kazi Tu! Wakati kasi ya Rais Dk. John Pombe Magufuli ?JPM? (pichani) kutumbua majipu ikishika kasi, hasa kwa vigogo wanaodaiwa kuiingizia hasara ya mabilioni ya shilingi serikali, kikosi maalum cha Oparesheni Fichua Maovu cha Global Publishers (OFM) kimeibua majumba sita ya kigogo mmoja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), jina linahifadhiwa kwa sasa.

OFM imeyanasa majumba hayo ikiwa ni wiki mbili tu baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kufanya ziara ya kushtukiza Mamlaka ya Bandari (TPA) sanjari na Mamlaka ya Mapato (TRA) katika ofisi zilizopo bandarini na kuibua maovu.

ZILIKO NYUMBA HIZO
Nyumba hizo ambazo hazikaliwi na watu licha ya kumalizika, zipo Mtaa wa Makurunge, Kiluvya nje kidogo ya Jiji la Dar, kilomita 20 kutoka Barabara Kuu ya Dar es Salaam-Morogoro. 

OFM WATIA TIMU
Baada ya waziri mkuu kutoa amri ya kukamatwa kwa baadhi ya vigogo wa TRA na TPA, wakazi wa eneo lenye nyumba za kigogo huyo walipiga simu chumba cha habari Global na kuzungumza na OFM kuelezea uwepo wa nyumba hizo. Kamanda Mkuu wa OFM aliwatuma wachapakazi wake kwenda kujionea hali halisi. 

WALINZI WATIMUA MBIO
OFM ilishuhudia nyumba hizo zikiwa katika eneo moja lenye ukubwa wa ekari 5 na kuzungushiwa uzio wa kulinda mipaka. Hata hivyo, baadhi ya majirani waliwaambia OFM kwamba, palikuwa na walinzi wawili lakini walikimbia baada ya kupata taarifa kuwa bosi wao amekamatwa na polisi kwa madai ya ufisadi. 

HALI ZA NYUMBA
Nyumba hizo zote zimeezekwa kwa mabati ya kisasa maarufu kwa jina la ?Msauz?, sakafu ziking?arishwa na marumaru. 
NDIVYO BASI IKO HIVI
Kwa kukisia, mwonekano wa nyumba hizo, kila moja inaweza kuwa imegharimu shilingi milioni 90 hivyo kwa nyumba 6 ni sawa na shilingi 540,000,000.
AMALIZA SHIDA YA MAJI
Eneo hilo licha ya kuwa na shida kubwa ya maji lakini kigogo huyo amechimba visima viwili vya kisasa vinavyotumia mota na hivyo kumaliza tatizo hilo kwake na kwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo. 
MAZINGIRA
Licha ya utulivu mkubwa na upepo unaovuma kutokea kwenye miti iliyo jirani, lakini pia ndani ya uzio wenye nyumba hizo kuna miembe dodo, sindano na sikio la punda ambazo zilianguka na kuoza kwa kukosa walaji. 
OFM NA MAJIRANI
OFM ilikwenda kwa jirani mmoja wa eneo hilo na kumkuta mwanamke. Walipomuuliza habari za mmiliki wa nyumba hizo, alisema huwa anamuona mara chache lakini siku zote kunakuwa na walinzi na mwanamke mmoja. 
OFM walitafuta namba ya simu ya mwanamke huyo aliyetajwa kwa jina moja la Maria ambapo alipopigiwa alisema angefika eneo hilo baada ya dakika kumi lakini makachero wetu walikaa eneo hilo kwa zaidi ya saa moja, mwanamke huyo hakutokea na kuendelea kusisitiza kuwa angefika baada ya dakika chache.
Jirani mwingine aliyehojiwa na OFM alisema kwa wiki mbili zilizopita, ameshangazwa na mafundi na mmiliki wa eneo hilo kusitisha ghafla ujenzi wa kumalizia (finishing) uliokuwa ukiendelea na walinzi wametoweka. 
OFM OFISI ZA SERIKALI YA MTAA
Baada ya kugandishwa kwa muda mrefu na Maria, OFM walikwenda Ofisi za Serikali ya Mtaa wa Kiluvya, Makulunge na kukutana na mmoja wa viongozi wa ofisi hiyo ambaye alikiri kuzifahamu nyumba hizo na mmiliki wake, lakini aliomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa ishu yenyewe iko kwenye vyombo vya juu kuliko mamlaka yake. ?Aaah! Ukweli zile nyumba hapa ofisini tunajua ni za huyo mtu mliyemtaja. Inavyoonesha kwenye mafaili yetu, jamaa alilinunua eneo lile kwa baba yake ambaye kwa sasa anaishi Mkoa wa Pwani, ?document? zote ziko hapa ofisini,? alisema kiongozi huyo. 
Licha ya OFM kupewa namba ya kigogo huyo lakini hakupatikana hewani na mpaka Jumatatu iliyopita, taarifa zilisema yeye na vigogo wenzake saba, wapo mahabusu ya Gereza la Segerea, Dar, wakisubiri kurejeshwa Mahakama ya Kisutu kwa kesi ya madai ya kutoa makontena 329 bandarini na kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni 12.7.