Rais John Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari jana Ikulu jijini Dar es salaam. Kushoto ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue. Kulia ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Picha na Ikulu
Uteuzi wa baraza la mawaziri uliofanywa na Rais Magufuli jana umewanufaisha baadhi ya naibu mawaziri wa awamu ya nne ambao wamepanda na kuwa mawaziri kamili.
Katika orodha hiyo, naibu mawaziri hao sita wameachana na unaibu , sasa ni mawaziri kamili.
Miongoni mwao ni aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Ummy Mwalimu ambaye sasa anakuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii na Ustawi.
Ummy Mwalimu anakabidhiwa wizara hiyo huku kukiwa na changamoto ya malalamiko ya kukosekana kwa huduma bora za afya, ukiwemo ukosefu wa vitendea kazi, kutowapo kwa watumishi wa afya na ustawi wa jamii wa kutosha katika vituo vya kutolea huduma.
Changamoto nyingine ya wizara hii ni pamoja na upatikanaji wa dawa muhimu, vitendanishi, vifaa tiba na vifaa vingine vya matumizi katika hospitali za halmashauri, vituo vya afya na zahanati kwa nchi nzima.
Akizungumzia nafasi aliyopewa, Mwalimu alisema: “Nimepokea uteuzi huu kwa heshma na unyenyekevu mkubwa. Ni tayari kukabiliana na changamoto zinazoambatana na kazi hii.”
Mwingine ni Charles Kitwanga aliyekuwa naibu waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia nishati ambaye kwa sasa amepanda na kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Changamoto zinazoikabili wizara hii ambazo waziri Kitwanga anatarajia kukabiliana nazo ni pamoja na malalamiko baina ya jeshi la polisi na wananchi kwa kuwa utendaji kazi wa jeshi hilo umekuwa lawamani kwa muda mrefu kuwa hauko rafiki na raia.
Vile vile yupo, Charles Mwijage, aliyekuwa naibu waziri wa Nishati na Madini, ambaye amechaguliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara akikabiliwa na changamoto ya usimamizi na utekelezaji wa ahadi ya Rais Magufuli ya kuwa na Serikali ya viwanda ikiwa ni pamoja na kuvifufua vilivyobinafsishwa kwa wawekezaji.
Aliyekuwa naibu waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ametuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano.
Mwingine aliyepanda ni Angella Kairuki aliyekuwa naibu waziri wa Katiba na Sheria ambaye sasa amekuwa Waziri kamili wa Ofisi ya Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala bora.
Makamba anakabiliwa na changamoto ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanachangia Taifa kukumbwa na majanga mbalimbali kama ukame, mafuriko, moto, vita vya wakulima na wafugaji na milipuko ya mabomu, majanga yote haya huleta maafa na kusababisha athari kwa wananchi na mali zao.
Naye Kairuki, aliyekuwa naibu waziri wa Sheria na Katiba amepanda na kuwa Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais.
Anakabiliwa na changamoto kubwa mbele yake ya kuongoza wizara hiyo ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo za mzozo wa kisiasa Zanzibar.
Aliyekuwa naibu waziri wa Fedha, Mwigulu amepelekwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Hii ni Wizara inayowalenga zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wa Tanzania.
Nchemba anacho kibarua cha kuweka mikakati ya jinsi ya kushughulikia tatizo sugu la migogoro baina ya wakulima na wafanyakazi inayoonekana kuota mizizi sehemu kubwa ya nchi. Pia, lipo tatizo la ukosefu wa pembejeo, zana bora za kilimo, mambo ambayo Rais Magufuli aliahidi kuyafanyia kazi wakati akiomba kura.
No comments :
Post a Comment