MWANASHERIA Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu anatarajiwa kuongoza jopo la mawakili watano watakaomtetea Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) katika kesi ya kupinga ubunge wake.
Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Didas Massaburi.
Kubenea aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na MTANZANIA baada ya Massaburi kufungua shauri la madai namba 8 la mwaka huu Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Kubenea, Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la Ubungo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mbunge huyo wa Ubungo alisema kwa kuwatumia wanasheria wake wamejibu hoja 11 ambazo zitawasilishwa mahakamani wiki hii.
“Jopo la mawakili wangu wamefanyakazi ya kujibu na naamini kesi hiyo itaisha katika hatua za mwanzo maana nina imani kubwa na kazi ya wanasheria wangu ambao ni Tundu Lissu, Mabere Marando, Peter Kibatala, Method Kimomogolo na Fredrick Kihwelo,” alisema.
Kubenea alisema katika madai waliyomtumia ameona hakuna madai ya msingi miongoni mwa madai hayo 11 yaliyotolewa na mlalamikaji.
Alisema miongoni mwa madai hayo, Massaburi ambayo anapinga ubunge wake ni kwamba waliruhusiwa wapiga kura ambao walikuwa hawakidhi umri halali wa kupiga kura ambao mwenyewe mlalamikaji aliwashuhudia.
Dk. Massaburi anadai kwamba msimamizi hakumuarifu kuhusu muda, mahali au tarehe ya sehemu yalikokuwa yakifanyika majumuisho ya mwisho ya kura za uchaguzi huo mkuu.
Vilevile Dk. Massaburi anadai kuwa yeye na mawakala wake hawakuruhusiwa kuona vifaa vya kupigia kura kama ilivyofanyika kwa Kubenea na mawakala wake.
Pia anamlalamikia Kubenea kwa kutoa rushwa ya jenereta katika hospitali ya Mavurunza eneo la Kimara, zawadi ya meza ya mchezo wa pool kwa vijana wa Makuburi na kujenga barabara ya Matete eneo la Kimara akiwashawishi kumchagua.
Katika madai hayo amemlalamikia msimamizi kukataa kuhakiki kwa mara ya pili matokeo yake ikiwamo na watu kadhaa wa maeneo ya Mizizini, Mianzini, Kilimahewa, Mizambarauni, Shule ya Mugabe na Kanuni, kutopiga kura.
No comments :
Post a Comment