DAR ES SALAAM, MTANZANIA.
RUNGU la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) limeonekana kushika kasi na safari hii limeangukia kwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).
Kwa mujibu wa barua ya TRA, Bakwata imetakiwa kutoa maelezo ya ongezeko la maombi ya msamaha wa kodi katika utoaji wa magari yanayopitishwa katika taasisi hiyo ya dini, kutoka nje ya nchi.
Hayo yamo katika barua ya TRA ya Novemba 19, mwaka huu kwenda kwa Katibu Mkuu wa Bakwata yenye kumbukumbu namba MK/TRA/09/VOL.5/107 ya Oktoba 9 mwaka huu iliyokuwa ikitaka punguzo la kodi ya gari aina ya Iveco yenye Chassis namba WJME2NM-4000428502.
Barua hiyo ya TRA inaeleza kwa sababu za kutokubali ombi hilo zimechangiwa na takwimu zinayoonyesha kwamba taasisi hiyo imekuwa na ongezeko kubwa la maombi ya msamaha ya kodi kwa magari kutoka nje.
Kwa mujibu wa barua hiyo, tangu mwaka 2006 hadi Septemba mwaka huu Bakwata imekwisha kuingiza magari 82 ya aina tofauti.
Barua hiyo iliyosainiwa na Meneja Misamaha ya Kosi wa TRA, Mwantum Salim, ilieleza kwamba kutokana na idadi kubwa ya magari ya msamaha pamoja na maombi yanayoongezeka uamuzi umechukuliwa wa kufuatilia kwa karibu kujua jinsi magari hayo yanavyotumika katika shughuli za taasisi kabla ya kuendelea kutoa misaada zaidi.
TRA imetoa siku saba kwa Bakwata iwe imewasilisha kadi za usajili wa magari, kitabu kinachoonyesha safari za magari, stakabadhi za kulipia mafuta, bima, huduma za matengenezo ya magari ikiwamo ushahidi wa maelezo na ushahidi kuhusu fedha zilizotumika kununua magari hayo pamoja na hesabu za mwaka za taasisi.
“TRA iliitaka Bakwata kuhakikisha inakamilisha hayo yote iweze kushughulikia maombi hayo ya kupata msamaha wa kodi wa gari aina ya Iveco kwa haraka,” ileleza barua hiyo ya TRA kwa Bakwata.
Mufti awa mbogo
Taarifa kutoka ndani ya Bakwata ziliambia MTANZANIA kwamba baada ya barua hiyo ya TRA, Sheikh Mkuu, Mufti Abubakari Zuberi, aliitisha kikao na kujadili suala hilo kati yake na Katibu Mkuu wake, Suleiman Lolila kuweza kupata maelezo ya kina.
“Katika kikao cha Mufti Zuberi, Katibu Mkuu Lolila, alitakiwa kutoa maelezo ya jambo hili lakini naye aliruka na kusema hausiki nalo ila linamhusu Naibu Katibu Majaliwa.
“Tangu baada ya kuletwa barua hii hapa, Bakwata kumekuwa hakukaliki hasa kwa watendaji wa juu akiwamo Katibu Mkuu na inaonekana Mufti Zuberi hana mchezo wa hili suala.
“Tena ni wazi haya yamekuwa yakifanyika kwa kipindi kirefu sana,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya Bakwata.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Bakwata, Suleiman Lolila, kupata ufafanuzi wa barua hiyo ya TRA, simu yake haikupokelewa licha ya kupigwa kwa zaidi ya mara saba kwa vile simu yake ilikuwa inaita bila kupokelewa.
Mwandishi wa habari hii alimtumia ujumbe mfupi kwa njia ya simu, Katibu Mkuu huyo wa Bakwata lakini nao hakuujibu hadi tulipokuwa tunakwenda mitamboni jana.
No comments :
Post a Comment