Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, December 20, 2015

Mawaziri waonyesha dalili njema za uwajibikaji

NA MHARIRI

20th December 2015.
Maoni ya Katuni
Tangu Rais Magufuli alipoteua baraza la mawaziri na kuwaapisha, baadhi yao siku hiyohiyo  walianza kuchukua hatua mbalimbali za kuwajibika katika maeneo yao, ikiwa ni pamoja na kufuatilia kwa karibu utendaji wa watumishi waandamizi walioko chini yao.

Hatua ya mawaziri kuanza kwa kasi kutekeleza majukumu yao inafanana na kasi aliyoanza nayo Rais Magufuli mara tu baada ya kuapishwa tarehe 5 Novemba mwaka huu, alipomteua mara moja Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na kumwapisha siku ya pili tarehe 6 Novemba.

Mawaziri hao wameonyesha dhamira ya kwenda kasi ili kupambana dhidi ya uzembe, ubadhirifu na kuziba mianya ya rushwa katika wizara zao, na pia wameonyesha dira ya mwelekeo wa utendaji wao ili kuboresha huduma ya kuwatumikia wananchi kwa ufanisi.

Baadhi ya mawaziri walioanza kuweka sera zao za utekelezaji wa 'Hapa Kazi Tu' ni pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi ambaye alitoa siku saba ya kupata maelezo kamili kuhusiana na mpango wa kuendeleza ufukwe wa Oysterbay na hasa Coco Beach, na pia undani kuhusu watu wanaomiliki mashamba makubwa bila ya kuyaendeleza.

Jenista Mhagama, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge amewataka wafanyakazi wa ofisi ya Waziri Mkuu kuacha mara koja kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wajitume zaidi ili kuendana na kasi ya Rais Magufuli.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga naye amewaweka 'kiti moto' viongozi waandamizi wa Jeshi la Polisi nchini akitaka kujua kwanini kero mbalimbali zinazidi kulisakama jeshi hilo ikiwa ni pamoja na kuwabambikiza watu kesi pamoja na tatizo la madawa ya kulevya, akatoa mbili kuitaka polisi wampe orodha ya wauzaji wa dawa za kulevya.

Mawaziri wengine kama Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangala, alitoa siku saba kuhakikisha takataka zote zilizolundikana maeneo mbalimbali nchini ziwe zimezolewa, upande wa Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Mifugo, Mwigulu Nchemba pia alitoa siku tano kwa mnunuzi wa korosho awe amewalipa wakulima bilioni 3.4/-.

Wengine waliotoa tahadhari kwa utendaji wao ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, pamoja na majukumu mengi alitoa siku 30 walioomba umeme wote waunganishiwe, Waziri wa Maji, Makame Mbarawa ametoa miezi sita kwa watendaji wake wahakikishe wanaotumia maji ya Dawasco wanaongezeka kuanzia idadi ya sasa ya 148,000 na kufikia milioni moja.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jaffo naye alitoa siku 26 kuhakikisha mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato uanze kutumika nchi nzima.

Mawaziri ni wasimamizi wa sera za mipango ya maendeleo ya Serikali, chini yao wana makatibu wakuu ambao pia ndio watendaji wakuu, na ndio maana mawaziri wanapotoa maazimio ya utekelezaji, ni wajibu wa viongozi wote walioko ndani ya wizara husika kutekeleza kwa mujibu wa kanuni na sheria.

Tunaamini kuwa matarajio ya utekelezaji wa muda mfupi waliojiwekea mawaziri hao, itakuwa dira ya utendaji wao kwa kasi ya kuwaondolea  umaskini wananchi wengi, ni dhahiri pia kuwa watasukuma mbele ahadi zilizowekwa na Rais Magufuli za kuwatumikia kwa mafanikio Watanzania.

Tumeshaona hata namna viongozi mbalimbali  walivyoanza kutoa msukumo wa utendaji katika maeneo yao kuanzia ngazi ya wilaya na vijijini, wanafuata maagizo kiutendaji ya kutekeleza kasi ya utendaji kama wanayoiona kutoka kwa Rais Magufuli.

Ni dhahiri kuwa utendaji wenye weledi mkubwa na unaozingatia nidhamu na maadili, utaitoa nchi kutoka katika hali ya utegemezi na kuwa huru kiuchumi kwa faida ya Watanzania wote.  
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment