Lowassa na Sumaye mbali na kukosoa mwenendo ulio kinyume na misingi iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere walipigia debe upinzani wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Akizungumza jana, Msuya alisema rushwa, uchakachuaji na matendo ya ovyo ya baadhi ya viongozi wake ndiyo yamesababisha kipoteze umaarufu kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita.
Ingawa mgombea wa CCM, Rais John Magufuli ndiye aliyeshinda katika uchaguzi huo kwa kupata zaidi ya asilimia 58 ya kura, Watanzania kwa kiasi kikubwa walivutiwa na rekodi yake ya utendaji kazi uliotukuka akiwa Waziri wa Ujenzi chini ya Kikwete.
Msuya amekitaka chama chake hicho kujitathimini na kisha kuchukua hatua dhidi ya viongozi na makada watakaotajwa kukihujumu katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Akizungumza wakati akifungua Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoani Kilimanjaro ambayo iliketi kwa ajili ya kupokea na kujadili taarifa ya Uchaguzi Mkuu uliopita, Msuya alisema:
“Msiwatazame vibaya wanachama wenu kama wasaliti maana wao wamekosa imani na matendo yenu, wanaonyesha kukichoka chama kwa sababu ya rushwa, uchakachuaji na ukiukwaji wa haki za zao za msingi.
“Viongozi lazima tukubali, tuache unafiki na undumilakuwili ili jamii hii hii iweze kutuamini na kutupa tena dhamana ya kuyakomboa majimbo yetu yaliyochukuliwa na wapinzani lakini pia tutwae majimbo mengine zaidi.”
Alisema viongozi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro lazima wajitathimini upya kutokana na kushindwa vibaya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na kuongeza kuwa iko haja kwa watakaobainika kukihujumu chama wachukuliwe hatua kali.
Msuya, 83, aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu kwa vipindi viwili Novemba 7, 1980 na Februari 24, 1983. Sumaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 mfululizo akiteuliwa Novemba 28, 1995 na Desemban 30, 2005 wakati Lowassa alidumu kwa muda mfupi kati ya Desemba 30, 2005 na Februari 7, 2008.
Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, CCM iliyapoteza majimbo matatu ya Siha, Same Mashariki na Moshi Vijijini ambayo ilikuwa ikiyashikilia.
Pia ilipoteza nafasi ya kuziongoza Halmashauri tano za Wilaya za Rombo, Moshi Mjini, Hai, Siha, Moshi Vijijini na Vunjo.
Akionyesha kutokubalina na utetezi unaotolewa mitaani na baadhi ya makada na viongozi wa CCM, Msuya alisema “Mkoa wa Kilimanjaro utabakia kuwa kambi ya upinzani kutokana na baadhi ya viongozi na wanachama kufanya mambo yasiyofaa katika jamii.
"Mambo hayo ni pamoja na kuwa undumilakuwili na kuendekeza vitendo vya rushwa.”
Aidha, Waziri Mkuu huyo wa zamani alisisitiza msimamo wake, akidai kuwa kama viongozi hao hawatakuwa makini na kukubali wana makosa na kutokiri kwa wanachama; ama kukubaliana kuanza safari mpya ya ukombozi, basi hakuna sababu ya kuendelea kukaa hapa Kilimanjaro.
Awali, akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu huyo wa zamani kuzungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya mkoa huo, Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro Deogratius Rutagumirwa alishangaa kushindwa vibaya huko.
“Binafsi siamini ni kwa nini tumeshindwa, tulijipanga vizuri, tena kwa nguvu zote na tuliona dalili zote za ushindi... mpaka sasa hatujui nini kilichotokea kwa CCM kupoteza majimo hayo kwa wakati moja,“ alisema Rutagumirwa.
Katibu huyo alisema kikao hicho cha tathimini, kinaweza kuwapa picha halisi ya nini kilichotokea, shida ilikuwa wapi na watajipangeje ili kuivunja ngome ya upinzani iliyosimikwa katika mkoa wa Kilimanjaro.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Iddi Juma alisema licha ya kuwepo kwa matatizo mbali mbali yaliyowakumba na kusababisha kupoteza majimbo hayo, pia aliwataka viongozi wake kuanzia ngazi ya matawi kuanza kujadili matatizo kwa uwazi ukweli na busara.
Imendikwa Na Mary Mosha na Rajabu Mmbughu
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment