Rais alitangaza Baraza hilo mbele ya waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam jana na kueleza kuwa mawaziri hao wapya ambao wataapishwa kesho saa 5:00 asubuhi Ikulu jijini Dar es Salaam, hawapaswi kufanya sherehe ya kufurahia uteuzi kwa kuwa kwake ni `Kazi tu’ na endapo watafanya sherere husika, basi pia wajiandae kufanya hivyo siku atakapowafuta kazi.
Yamekuwa ni mazoea anayeteuliwa kuwa waziri, kuchukulia kama fursa ya kujineemesha kwa kujirundikia utajiri wa kutisha kutokana na mianya kadhaa ya kupata fedha, mbali na mishahara ya kila mwezi.
Hata hivyo, akitangaza Baraza lake hilo ikiwa ni siku ya 35 tangu aapishwe kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk. Magufuli alisema nafasi ya uwaziri ni ‘mzigo mzito’ na hivyo hatarajii kusikia yeyote kati ya aliowatangaza watafanya sherehe za kujipongeza kama ilivyozoeleka.“Na kwa hakika, wasihangaike kufanya sherehe. Wamepata kazi ngumu, wakafanye kazi, lakini kama wapo ambao wanaopenda kufanya sherehe, pia wajiandae kufanya sherehe siku wakifukuzwa. Nataka kuwa na baraza dogo ambalo jukumu lake litakuwa ni kwenda kufanya kazi za Watanzania,” alisisitiza Rais Dk. Magufuli na kuongeza:
“Contract’ (mkataba) wetu ni miaka mitano, tukawafanyie Watanzania yale tuliyoyaahidi, bila kubagua rangi, dini, itikadi, ukanda, makabila, ndiyo maana siku zote nimekuwa nikisema Hapa ni Kazi tu…Nilijiridhisha pamoja na wenzangu kwamba baraza hili litafanya kazi kwa weledi bila kuwa na masuala ya mchakato, tutafanya hivi na vile.”
Rais Magufuli alisema kutokana na Baraza kuwa dogo, makatibu wakuu na naibu mawaziri, pia watapungua na hivyo kuendelea kupunguza matumizi ya serikali.
AWEKA KIPORO WIZARA NYETI
Katika Baraza hilo, Dk. Magufuli ameacha wazi nafasi za wizara nne kutokana na kile alichoeleza kuwa ‘bado anatafuta walio na sifa’, na hivyo Watanzania wawe na subira.
Alizitaja wizara hizo kuwa ni Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano; Fedha na Mipango, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Elimu.
“Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, waziri wake bado sijamtafuta; naendelea kumfikiria,” alisema.
Kadhalika, Dk. Magufuli amewateua naibu mawaziri 18 na hivyo kuwa na jumla ya mawaziri 30 na pindi atakapojaza nafasi za mawaziri katika wizara zilizosalia, atakuwa na baraza lenye mawaziri 34.
Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete, iliyomaliza muda wake Novemba 5, mwaka huu, ilikuwa na mawaziri 30 na naibu mawaziri 25, hivyo kuwa na jumla mawaziri na naibu wao 55.
Baada ya kutangaza majina ya wanaounda Baraza lake la Mawaziri na pia kuwataja naibu mawaziri, Rais Magufuli alisema ameamua kuteua baraza dogo kwa nia ya kuona kwamba wote wanafanya kazi kwa ufanisi ili kuhakikisha kuwa wanatimiza lengo la kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo.
WALIOTEULIWA
Mawaziri Ofisi ya Nchi Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene na Angela Kairuki, Naibu ni Jafo Suleiman; Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Waziri ni Januari Makamba, Naibu ni Luhaga Mpina.
Waziri wa Ofisi ya Nchi, Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, ni Jennista Mhagama, Naibu Mawaziri ni Profesa Possi Abdallah na Anthony Mavunde; Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba, Naibu ni William Tate Ole Nashe.
Wizara ya Katiba na Sheria, Waziri ni Dk. Harrison Mwakyembe; Dk. Augustine Mahiga, Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Naibu ni Dk. Susan Kolimba; Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Waziri ni Dk. Hussein Mwinyi; Wizara ya Nishati na Madini, Waziri ni Profesa Sospeter Muhongo na Naibu ni Medadi Kalemani.
Wizara ya Mambo ya Ndani, Waziri ni Charles Kitwanga; Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Naibu Angelina Mabula; Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Waziri ni Charles Mwijage; Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri ni Ummy Mwalimu, Naibu Dk. Hamis Kigwangala.
Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Waziri ni Nape Nnauye, Naibu ni Anastazia Wambura; Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Waziri ni Profesa Makame Mbarawa, Naibu Mhandisi Isaack Kamwela.
WIZARA ZILIZOKOSA MAWAZIRI
Katika uteuzi huo Wizara nne zimekosa mawaziri ambao alisema atawateua siku zijazo na kuteua manaibu pekee.
Wizara hizo ni Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi, Mawasiliano (haina Waziri), Naibu ni Injinia Edwin Ngonyani; Fedha na Mipango (haina Waziri), Naibu ni Dk. Ashantu Kijaji.
Nyingine ni Wizara ya Maliasili na Utalii (Haina Waziri), Naibu ni Mhandisi Lamo Makani; Wizara ya Elimu, Teknolojia na Ufundi (haina Waziri), Naibu ni Mhandisi Stellah Manyanya.
KUVUJA JASHO
Tofauti na miaka ya hivi karibuni ambapo nafasi za juu za uongozi zikiwamo za uwaziri zilikuwa zikichukuliwa kuwa ni ‘ulaji’ kiasi kwamba watu walikuwa wakipongezana, inaonekana wazi kuwa mawaziri wa Rais Magufuli watakuwa tofauti.
Mianya mingi iliyokuwa ikitajwa kuwapatia mawaziri mamilioni ya fedha inaelekea kuzibwa kutokana na amri kadhaa alizotangaza tangu aapishwe kuwa Rais, lengo likiwa ni kubana matumizi na kuwezesha fedha zinazopatikana zitumike kumaliza kero mbalimbali zinazowakabili Watanzania.
Baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakitajwa kuwaingizia fedha nyingi mawaziri, lakini sasa yameondoshwa na hivyo kubana matumizi holela ya serikali ni pamoja na hafla za kupongezana, safari za nje; posho za semina elekezi, kuchapisha kadi za Krismasi, Mwaka Mpya, Iddi na sikukuu nyingine, manunuzi ya bidhaa mbalimbali yenye fedha za ziada maarufu kama ‘cha juu’, posho za vikao vya kikazi mikoani, manunuzi ya kila mara ya samani za ofisi zilizokuwa zikitoka ughaibuni na pia posho za vikao vya kamati za Bunge.
Rais alisema serikali yake imechelewa kuteua Baraza la Mawaziri kwa muda wa mwezi mmoja kwa ajili ya kuokoa fedha za mishahara na marupurupu ya Mawaziri na Manaibu ambazo zingetumika kwenye shughuli nyingine za maendeleo ya taifa.
“Natambua siwezi kukaa hivi hivi bila Baraza la Mawaziri, katika Baraza hili Wizara nyingi tumeziunganisha, tutakuwa na Wizara 18 tu na katika wizara hizo kutakuwa na Mawaziri 19, baadhi zitakuwa na Naibu Mawziri na nyingine hazina, lengo kubwa kutimiza ahadi yetu ya kuwa na Baraza dogo na itasaidia kupunguza matumizi yasiyo ya lazima,” alisema na kuongeza:
Alisema wanataka Baraza dogo ambalo litafanya kazi kwa weledi.
“Kwa bahati mbaya hapatakuwepo semina elekezi, nafahamu zilitegwa Sh. bilioni mbili kutoka Utumishi, wamezitenga kwa ajili ya Baraza litakapoteuliwa,” alisema.
“Hakutakuwa na semina elekezi, wataelekezana wao kwa wao, humo kwa humo kwa kuwa wanajua wanafanya kazi ili fedha zaidi ya Shilingi bilioni mbili zilizotengwa na Utumishi zielekezwe kwenye kutengeneza madawati au kusaidia kwenye elimu kwa wanafunzi watakaosoma bure, tutapanga vizuri matumizi yake,” alisema.
HAPA KAZI TU
Alisema mawaziri na naibu waziri aliowachagua, wote ni wana-CCM na wengi wao ni wabunge ambao wakati wa kampeni walinadi falsafa ya hapa kazi tu hivyo kasi ya Rais wanaifahamu na ndiyo maana amefuta semina elekezi.
“Nimeunda Baraza dogo kwa kuwa nataka wakafanye kazi na hapa ni kazi tu, wakienda kule wakafanye kazi kweli kweli, sisi tulianza kwa kufanya kazi hivyo nina hakika wenzetu hawa wakafanye kazi kama sisi, ndiyo maana hatutakuwa na semina elekezi,” alisema na kuongeza:
“Waziri Mkuu hakwenda semina elekezi, semina yake ilianzia kwenye makontena, alijielekeza mwenyewe huko huko, Makamu wa Rais amejielekeza kwenye usafi, sasa na hawa ambao nimewateua, wasisubiri semina elekezi, wajielekeze kwenye maeneo yao,” alisisitiza Dk. Magufuli.
NCHI NYINGINE HALI IKOJE
Rais Dk. Magufuli alisema Baraza lake ni dogo na ukiangalia nchi nyingine zipo zenye mawaziri na naibu mawaziri 70, wizara 44.
Rais aliwaonyesha waandishi wa habari kitabu chenye orodha ya nchi mbalimbali duniani na idadi ya mawaziri na naibu mawaziri waliopo.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment