Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, December 20, 2015

Mfumo dume ulivyowakandamiza wanawake wakati wa Uchaguzi Mkuu Zanzibar

Wanawake wakishiriki kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu uliofutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Picha ya Maktaba.
By Salma Said, Mwananchi
Licha ya wanaharakati mbalimbali Tanzania kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya unyanyasaji wanawake, vitendo hivyo vinaendelea.
Nchi inayoheshimu demokrasia na utawala bora haiwezi kuzuia  wananchi wake kuwa huru kuchagua na kufanya jambo wanalolipenda ilmrad hawavunji sheria.
Katiba zote mbili za Tanzania Bara na ile ya Zanzibar zinampa mwananchi uhuru wa kuamua, kuchagua na kuchaguliwa katika uchaguzi, lakini haki hiyo imekuwa ikiporwa na baadhi ya watu wanaofikiri wana haki kuliko wengine.
“Wanaume wanakuwa  ni waamuzi wa wanawake wakati wanawake wana haki ya kujiamulia,” anasema Hasina Mbarouk ambaye ni mwanaharakati.
Usawa wa kijinsia ni dhamira iliyowekwa miaka mingi katika dunia na upande wa Zanzibar, jitihada zake zilianza kuonekana zaidi miaka ya 1980 baada ya mkutano wa dunia wa wanawake uliofanyika Nairobi, Kenya na tangu hapo makundi ya wanaharakati yakaanza kupaza sauti kuwatetea wanawake.
Baada ya miongo mitatu sasa, bado tofauti ya upatikanaji haki, uamuzi na umiliki wa rasilimali baina ya mwanamke na mwanaume imekuwa ndogo, lakini juhudi za kuwatetea wanawake zinaendelea katika kila nyanja.
Wanawake wengi wamekuwa wakihamasishwa kujitokeza kwa wingi katika harakati za kujikomboa kwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika nchi zao, lakini bado kuna vikwazo wanakumbana navyo kabla ya kufikia kwenye mafanikio hayo.
Vikwazo hivyo ni pamoja na umaskini, kukithiri kwa rushwa, ukosefu wa elimu na kusongwa na majukumu ya kifamilia. 
Pia, tabia ya baadhi ya wanaume kuwalazimisha wanawake wafanye kazi za nyumbani pekee, bila ya kujishughulisha na masuala mengine  ya kijamii, nayo imekuwa kero.
Uchaguzi Mkuu 2015
Hali kama hiyo ilijitokeza wakati    wananchi walipokuwa wakishiriki Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu na kuahirishwa siku tatu baadaye. Katiba baadhi ya maeneo hapa nchini, hususan Zanzibar kumeripotiwa kesi kadhaa za udhalilishaji wanawake.
Baadhi ya wanawake hao walipewa talaka walipojaribu kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuwachagua viongozi wanaowataka.
Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Mzuri Issa Ali anasema suala la unyanyasaji wa kijinsia lipo katika jamii na linapaswa kupigwa vita na kila mwananchi.
Anasema katika utafiti mdogo walioufanya wamegundua kwamba kuna baadhi ya wanawake wamepewa talaka na wengine kutishiwa kuachwa baada ya kubainika walitaka kuwapigia kura wagombea waliokuwa wakipingwa na waume zao.
“Wanawake 47 walikatazwa kupiga kura lakini walikwenda na hivyo kupewa talaka, 24 walitishiwa talaka ikiwa watahudhuria mikutano ya kampeni au watapiga kura matokeo yake wote hawakupiga kura,” anasema Ali.
Baadhi ya wanawake ambao wanasema waliwekewa vikwazo na waume zao wasiende kupiga kura, wapo ambao walikatazwa wasipige kura, lakini hawakukubali kutii amri hizo na waliporejea nyumbani ingawa hawakupewa talaka lakini walitishiwa kuachwa.
Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wanawake 30 walijitokeza kugombea nafasi za uwakilishi kupitia vyama vyao, huku viti vya udiwani wakijitokeza wanawake 87.
Kati ya wanawake  hao, kumi waligombea kiti cha uwakilishi ambao ni sawa na asilimia 33.3.
Uchaguzi wa hivi karibuni, pamoja na dosari zilizojitokeza, umethibitisha kwa kiasi kikubwa tofauti hiyo ya nguvu kati ya wanawake na wanaume. Kwanza, katika kinyang’anyiro chenyewe cha kugombea nafasi, lakini pia katika upigaji wa kura zenyewe.
Tamwa kwa kushirikiana na wadau kadhaa likiwamo Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wanawake (UN Women) imetoa  mafunzo kwa wanawake na wanaume vijana 355 takriban vyama vya vya siasa 20.
Hata hivyo, wanawake waliojitokeza kuwania nafasi za uongozi ni wachache ikilinganishwa na idadi ya waliopewa mafunzo na pia idadi ya wanawake nchini.
“Ni mambo ya kusikitisha sana kuona wanawake wanatukanwa matusi makubwa na baadhi ya wagombea ndani ya vyama, kwa mfano mgombea ndani ya CCM (Mkoa wa) Kaskazini (Unguja) alitukanwa kwenye simu yake ya mkononi hadi alitaka kukata tamaa ya kugombea,” anasema mratibu huyo.
Aidha, katika upande wa upigaji kura baadhi ya wanawake walilazimishwa kupigia kura chama fulani kinyume na matakwa yao jambo ambalo ni kinyume na demokrasia.
Kwa mfano wakati wa kampeni, mwanamke mmoja hapa Zanzibar alijikuta katika wakati mgumu kutoka kwa mumewe baada ya kukataa amri aliyopewa ya kutohudhuria mkutano wa kampeni wa chama cha siasa.  
Pia, baadhi ya wanawake  wajasiliamali wamejikuta wakikimbiwa na wateja kutokana na kuwa na misimamo tofauti ya kisiasa. 
Ofisa wa Tamwa Zanzibar, Asha Abdi anasema matatizo ya udhalilishaji yanapaswa kuvaliwa njuga na kila mwanajamii ili yaweze kutoweka katika visiwa vya Zanzibar.
Anasema bado jitihada zaidi zinahitajika kuongezwa kwa kuwa jamii inazidi kuathirika kutokana na hali hiyo.
“Mmoja wao alidai yeye biashara zake hazinunuliwi kutokana na ushabiki wake wa chama cha CCM kule Pemba” anasema Abdi.
Tabia ya wananchi visiwani Zanzibar ya kutouziana bidhaa kwa tofauti za kisiasa ilianza siku nyingi.
Hata hivyo, hali hiyo ilikuwa imetoweka baada ya kupatikana mwafaka wa kisiasa uliofikiwa kati ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk Amani Abeid Karume chini ya kamati ya watu sita kutoka pande zote mbili iliyokuwa ikiongozwa na mzee Hassan Nassor Moyo.

No comments :

Post a Comment