Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
Mwanza. Mbunge wa Nyamagana Stanslaus Mabula amemuomba Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kuishawishi Serikali kuitengea bajeti Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC) kwa asilimia 100 ili kuboresha huduma zake kwa wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mabula alitoa rai hiyo juzi alipotembelea hospitali hiyo pamoja na Kamati ya Afya ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Alisema huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo ni za kiwango cha juu, hivyo bajeti wanayopata haitoshi kuendesha hospitali hiyo.
“Kwa sasa hospitali inatengewa bajeti isiyozidi asilimia 50, hivyo umefika wakati Serikali kuitazama hospitali hii kwa kina kwani inahudumia watu wengi.
“Tunataka kuona huduma zinazotolewa hapa zinazidi kuwa bora na za kiwango cha hali ya juu, lakini hiyo itawezekana kama Serikali itaiongezea nguvu. Hapa kuna mashine za kisasa ambazo hazipatikani sehemu nyingine hilo ni jambo la kujivunia,” alisema.
Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire alisema halmashauri hiyo imejipanga kuzisaidia hospitali za kata na wilaya, ili kuipunguzia mzigo hospitali ya Bugando.
“Kwa kweli hospitali inafanya kazi kubwa ya kuhudumia mikoa mbalimbali ya Kanda ya Ziwa, Halmashauri ya Jiji la Mwanza tukipanga bajeti ya mwaka 2016/17 tutahakikisha tunaboresha huduma za afya katika hospitali za kata ili kuipunguzia mzigo Bugando,” alisema Bwire.
Alisema hospitali hiyo imejenga chumba cha kisasa cha kuhifadhia maiti ambacho kitakuwa na uwezo wa kuhifadhi miili 48 kwa pamoja.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Profesa Alfred Mteta alisema licha ya hospitali hiyo kuhakikisha inaboresha huduma, bado inakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu na vitendea kazi.
“Tumejitahidi kuhakikisha tunaboresha huduma na kupunguza malalamiko ya wananchi, lakini tuna changamoto ya uchakavu wa miundombinu na vitendea kazi, ingawa tumejipanga kuhakikisha tunaboresha iwezekanavyo,” alisema Profesa Mteta.
No comments :
Post a Comment