Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
Serengeti. Waathirika wa mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Park Nyigoti na Pori la Akiba la Ikorongo wilayani Serengeti Mkoa wa Mara, uliodumu kwa zaidi ya miaka kumi, wamemuomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuutatua.
Tangu mwaka 2003 wananchi wamekuwa wakilalamikia mpaka huo unaodaiwa kuwekwa na wataalamu wa idara ya wanyamapori kinyume na Tangazo la Serikali GN NO214 Mwaka 1994.
Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Celestine Gesimba alisema juzi kuwa wanatambua kuwapo wa mgogoro huo lakini wanakwamishwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa sababu ndiyo yenye wataalamu.
“Tulishaomba mtaalamu wa kutafsiri GN kutoka kwenye vitabu kuja ardhini lakini kwa muda mrefu sasa hatujapewa mtaalamu kutoka Wizara ya Ardhi, inakuwa vigumu sisi wenyewe kuja huko,” alisema Gesimba.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Park Nyigoti, Mtiro Marinya alisema kwa kipindi chote hicho hawajawahi kupata msaada kwa sababu Wizara ya Maliasili na Utalii licha ya kutambua wamefanya makosa, hawataki kurekebisha.
“Walikiri kwa maandishi kupitia kwa kiongozi mmoja wa Pori la Ikorongo na wataalamu wa ardhi wa halmashauri walithibitisha makosa hayo kwa kuwa mpaka umewekwa hadi shuleni, GN hiyo inaonyesha walitakiwa kuweka kwenye vilima vya Robesunga lakini wao wameweka Romegunga, eneo ambalo ni kijiji,” alisema Marinya.
Mkazi wa kijijini hicho, Nyabakereti Machota alisema wanawake wanapata shida kwa sababu wanapokutwa wanatafuta kuni eneo ambalo wanaamini ni lao wanakamatwa, kupigwa na kuteswa ilhali Serikali ipo.
“Naamini Rais John Magufuli atatusaidia, maana tumenyanyasika, mifugo imeuawa, watu wanapigwa, wanafungwa, tunazidi kuwa maskini wakati wanajua eneo hilo ni mali ya wananchi,” alisema. Pori la Ikorongo lina ukubwa wa kilomita za mraba 558.9.
No comments :
Post a Comment