Mbunge wa Geita, Joseph Msukuma
Geita. Kikao cha wadau wa barabara mkoani Geita, kimelazimika kusitishwa kwa muda kwa ajili ya kwenda kukagua mitambo ya ujenzi iliyonunuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Uamuzi huo umetokana na tuhuma zilizotolewa na Mbunge wa Geita, Joseph Msukuma kuwa haikidhi viwango vya ubora.
Wadau hao wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Fatma Mwasa walitembelea mitambo hiyo inayotakiwa kulipiwa Sh1.2 bilioni, kwa lengo la kubaini wa tuhuma hizo.
Kabla ya kuikagua, Mwassa alisema pia kuna taarifa zilizotolewa kwenye vyombo vya habari hivi karibuni zikituhumu kuwa kuna ubadhirifu wa Sh400 milioni katika ununuzi wa mitambo hiyo.
Alisema timu ya wataalamu inafanya ukaguzi ili kutoa taarifa sahihi kuhusiana na hilo na tuhuma hizo, iwapo itabainika kuna udanganyifu itarudishwa kwa muuzaji na fedha kugawanywa kwenye kata ili wananchi wanufaike kwani zinazotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).
Mkuu huyo wa mkoa alimtaka Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Geita, Ali Kidwaka kutaja gharama zilizotumika kununulia mitambo hiyo ili kuwathibitishia wajumbe tuhuma zilizotolewa.
Kidwaka alisema mpaka sasa halmashauri hiyo haijalipa fedha zozote kwa kampuni iliyopeleka mitambo hiyo na kwamba, mafundi kutoka Wakala wa Mitambo na Umeme (Temesa), wanakagua kuangalia ubora wake kama imekidhi vigezo.
Alisema kwa utaratibu wa ununuzi, mitambo hiyo inapaswa kuhakikiwa ili hatua ya malipo ifuate, tayari ameunda timu ya wataalamu kutoka Temesa, ofisi ya mkuu wa mkoa na halmashauri kwa ajili ya kufanya ukaguzi.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie alisema ununuzi wa mitambo hiyo ulifuata utaratibu na baada ya kupata ushauri wa kitaalamu kutoka Wizara ya Ujenzi, ilipowasili ilikaguliwa na kuonekana ina ubora.
Fundi Mkuu wa Tamesa mkoani Geita, Mussa Mpagama alisema kulingana na utaratibu wa ununuzi, kama fundi mkuu aliitwa na kuikagua mitambo mitatu ya barabara iliyotolewa na Kampuni ya Mantrac na kubaini ina ubora.
Mbunge wa Nyang’hwale, Hussein Hamad maarufu Kassu, alisema mitambo hiyo haina dosari kwa kuwa ina uwezo wa kuonyesha kipimo cha mafuta na inazuia wizi wa mafuta na kuonyesha kilomita zilizotumika, hali itakayosaidia usimamizi.
No comments :
Post a Comment