Tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli aanze kasi ya kushughulikia kero mbalimbali za wananchi, kumekuwa na maoni mbalimbali kuhusu aina ya ufanyaji kazi wake.
Rais Magufuli alianza kasi hiyo kwa kuzitembelea idara mbalimbali za Serikali zikiwamo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pia ameshafika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kushuhudia namna huduma zinavyotolewa. Wananchi wameonekana kufurahishwa na kasi hiyo.
Kitendo cha kufuta sherehe za uhuru zinazofanyika kila Desemba 9 kila mwaka na kisha kuagiza mabilioni ya fedha yaliyotengwa kwa ajili ya sherehe hizi yaelekezwe katika mahitaji muhimu, kimewagusa Watanzania kiasi kwamba baadhi yao wameufananisha uongozi wa Dk Magufuli na ule wa Rais wa kwanza Mwalimu Julius Nyerere.
Miongoni mwa watu walioguswa na hatua za Rais Magufuli ni aliyewahi kuwa gavana wa kwanza wa Benki Kuu Tanzania (BoT) na mwasisi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edwin Mtei.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili juzi mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, Mtei anasema anamatumaini makubwa na kiongozi huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Swali: Unamtazamaje Rais Magufuli?
Jibu: Ni mtu mwenye shauku na maendeleo, ni mzuri kama atasimamia na kuishi maneno yake. Ni mtu ambaye atasimamia maendeleo yetu na ninaamini atasimamia ukuaji wa uchumi wetu.
Pamoja na kuridhishwa na kasi ya Rais Magufuli, naamini kwamba kwa sehemu kubwa anatekeleza sera na ilani ya Chadema.
Kile anachofanya kwa sasa kimekuwa ni kilio cha muda mrefu kwenye ilani na sera zetu na tutashirikiana naye katika kuisadia hii nchi yetu.
Swali: Je, ungepata nafasi ya kumshauri Rais Magufuli ungemwambia nini.
Jibu: (anavuta pumzi) Kwanza ningempongeza kwa kupata ushindi katika hali ngumu sana, lakini ningemshauri maliasili za taifa hili zitumike kwa ajili ya Watanzania wote na wananchi washirikishwe katika kuendeleza nchi yao.
Ningemwambia ahakikishe Watanzania wanashirikishwa katika umiliki wa ardhi na kuwekeza. Wao ndiyo wawe wahusika wakuu katika kusimamia rasilimali zao na siyo vinginevyo hata wageni wakiingia nchini wawe kama wabia tu.
Nashauri kwamba wageni wanaotaka kuwekeza katika sekta ya madini, wauze hisa zao kwa Serikali ambayo itakuwa ikimiliki hisa nyingi zaidi. Kwa kufanya hivyo, maliasili za Taifa zitatumiwa na wazawa wenyewe.
Ningemshauri Rais Magufuli ahakikishe Watanzania wananufaika na rasiliamali zao ambazo walipewa na Mwenyezi Mungu kwa kusudi la kuwakomboa na umaskini.
Swali: Unadhani Rais Magufuli anairejesha Tanzania ya Mwalimu Julius Nyerere?
Jibu: Kwanza unajua mimi napinga siku zote Azimio la Arusha kwa kuwa naamini liliturejesha katika umaskini, hivyo nisingependa Rais Magufuli airejeshe nchi yetu katika enzi za Mwalimu Nyerere.
Rais Magufuli anaweza kuchukua mambo machache kutoka kwa Mwalimu Nyerere ikiwamo ufufuaji wa viwanda vilivyokufa.
Ningependa airejeshe Tanzania kwa watu wake kufaidi matunda ya rasilimali zao kama wananchi wawe na ajira, mashamba na uchumi wa kuwatajirisha wote na siyo watu wachache.
Swali: Je, ni nini unaona kimebadilika tangu enzi za Mwalimu Nyerere hadi sasa.
Jibu: Mambo mengi yamebadilika sana kama uchumi umepaa na watu wanafaidika kupitia uchumi huo, lakini tatizo lililopo hapa ni kwamba wanaofaidi ni wachache kuliko wale wengi ambao ni maskini wa kutupwa.
Tanzania haina mfumo wa kuwabana matajiri kuhakikisha wanawasaidia maskini kuinua uchumi wao ili nchi ipige hatua kwenye maendeleo, lazima iweke mfumo huo.
Baraza la Mawaziri
Swali: Je una maoni gani kuhusu baraza jipya la mawaziri?
Jibu: (Anatabasamu) Kwanza hili siyo baraza dogo hata kidogo, laiti kama angekuwa na mawaziri 18 hadi 24 hapo tungesema baraza ni dogo. Hili nililiona wakati nikiwa gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT) na mshauri wa Rais katika masuala ya uchumi, Mwalimu Nyerere alikuwa na baraza dogo.
Naamini Rais Magufuli kabla ya kuteua baraza hilo alizingatia watu waadilifu na wenye uzoefu na siyo walafi, huku akidai hategemei mapya ndani ya baraza hilo kwa kuwa litatekeleza sera za CCM ambazo zile zile za miaka nenda rudi.
Mtei anasisitiza kwa kuwa Rais Magufuli analenga kuleta mabadiliko nchini kwa lengo la kuwafanya Watanzania wafaidi matunda ya rasilimali zao kama gesi, mafuta na madini, basi baraza hilo halina budi kuendana na kasi yake.
“Mawaziri hawana namna ni lazima waendane na kasi yake au waondoke. Ni lazima hili baraza lihakikishe linafanya kama aliyewateua anavyotaka kuwatumikia Watanzania wote, ” anasema.
Hali ya kisiasa Zanzibar
Swali Je unaitazama vipi hali ya kisiasa iliyoko Zanzibar hivi sasa?
Jibu: Hali iliyopo Zanzibar siyo ya kufurahisha, kinachotakiwa kifanyike pale ni kuhakikisha visiwa vya Pemba na Unguja vinaungana na kuwa huru, lakini baada ya hatua hiyo vitaunganishwa na Tanganyika kisha kuunda shirikisho.
Mtei anasema uamuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kufuta matokeo ya yalikuwa ni batili na kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Uamuzi wa Jecha (Salum Jecha, Mwenyekiti wa ZEC) kufuta uchaguzi ulikuwa ni batili na haukubaliki, tungemkamata huyu mwenyekiti na kumchukulia hatua kwa kuwa amefanya kinyume na katiba yetu, ”anasema.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa mgogoro wa Zanzibar unaathiri hali iliyopo Tanzania Bara kwa kuwa kuna vijana kutoka bara ambao wanafanya kazi visiwani humo kwa hali ya wasiwasi.
Anaongeza kuwa laiti kama kungekuwa na utulivu wa kisiasa, Jamhuri ya Muungano ingekuwa na utajiri wa kutosha kwa kuwa katika nchi hizo mbili kuna ugunduzi wa gesi na mafuta ambayo yangetumika kuzinufaisha nchi hizo.
“Maalimu Seif hakutaka damu imwagike ndiyo maana amekuwa mpole, lakini hii hali inatugharimu sote kwa sasa tunaingia gharama, ” anasema Mtei.
Tangu kufutwa kwa uchaguzi visiwani Zanzibar, vikao mbalimbali vimekuwa vikifanyika ili kupata suluhu ya mvutano ulioibuka kutokana na uamuzi huo wa ZEC.
No comments :
Post a Comment