Wanafunzi wa moja ya shule binafsi nchini wakiwa katika darasa la kompyuta.
Dar es Salaam. Maandalizi ya upangaji wa ada elekezi kwa shule binafsi nchini yameibua mvutano kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi na Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongsco) baada ya kulalamikia kutopewa nafasi ya ushiriki katika hatua za awali.
Katibu Mkuu wa Tamongsco, Benjamini Nkonya alisema jana kuwa chama hicho kiliwachagua mawakili wake wanne kwa ajili ya kutoa ushirikiano kwa wizara hiyo katika upangaji na uchambuzi wa ada elekezi, lakini haijawatumia.
Alisema Serikali imekuwa ikiwatumia wamiliki wa shule binafsi wasiokuwa na uwakilishi wa mawazo ya chama hicho.
Waliochaguliwa na chama hicho kuwakilisha maoni yao ni mwenyekiti wake, Mrinde Mnzava, makamu mwenyekiti Jeremiah Bwegenyeza, Katibu mkuu, Benjamin Nkonya na mhasibu, Mapenzi Yona.
Hata hivyo, Kamishina wa Elimu Wizara hiyo, Profesa Eusella Bhalalusesa alipinga ofisi yake kupokea majina ya wawakilishi wa chama hicho.
Alisema utafiti bado unaendelea, hivyo wanayo nafasi ya kuwasilisha maoni yao.
“Sijapata majina yao, lakini kwa nini tugombanie fito wakati nyumba ni moja? Wadau ni wengi na siyo rahisi kumfikia kila mmoja, wataalamu watakapokamilisha ripoti yao kabla ya mwaka wa masomo 2016, tutaichambua na wadau wote kabla ya kuanza majaribio yake.
“Lakini katibu huyo wa Tamongsco (Benjamini Nkonya) nilimuona kwenye televisheni akisema wameshiriki vizuri kutoa maoni yao,” alidai Profesa Bhalalusesa.
Profesa Bhalalusesa alitaja baadhi ya vigezo vitakavyotumika kupanga ada elekezi kuwa ni huduma zinazotolewa na shule, eneo la shule inakopatikana na mmiliki wa shule husika.
Alipoulizwa kuhusu kutenganisha mtoa huduma na mfanyabiashara ili kutoza kodi alisema:
“Ndiko tunaelekea huko, tutaangalia shule inayotoa huduma na inayofanya biashara ili iweze kutozwa kodi.”
No comments :
Post a Comment